Tofauti na Ligi Kuu ambayo mpaka timu ipande daraja, michuano hii inazishirikisha kuanzia madaraja ya chini kuliko hata za juu.
Karibuni kila mwaka huwa tunaona kuna baadhi ya timu za madaraja ya chini zinajitutumua wakati mwingine kufanya maajabu kwenye michuano hii, ikiwa ni pamoja na kuwaangusha wakongwe, lakini mbele ya safari zinatolewa kutokana na kukosa uzoefu pamoja na viwango vidogo vya wachezaji wao.
Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, amewataka mashabiki wa soka walio karibu na maeneo ambayo michuano hiyo inachezwa kujitokeza kwa wingi kwenda kuangalia mechi hizo.
Ndimbo aliongeza tayari wameshawapa semina waamuzi kwa ajili ya kuwapiga msasa ili pamoja na mechi zingine, lakini wachezeshe kwa haki na kwa viwango vinavyotakiwa michuano ya Kombe la FA.
Licha ya kuwa waamuzi wamekuwa wakifanya makosa mengi yanayoitwa ya kibinadamu hata kwenye Ligi Kuu, lakini hatutarajii sasa kuona yanajirudia katika michuano hiyo hasa kwa timu ndogo ambazo ndizo zinajitutumua.
Kuna dhana timu ndogo zinajaza kwani hata kama zikisonga mbele hazina uwezo wa kucheza michuano yoyote ya kimataifa, si kwa viwango tu bali hata uwezo wa kumudu kusafiri.
Kwa maana hiyo baadhi wanaona kama zifanyiwe njama, zifungwe zibaki timu zenye uwezo zitakazoweza kumudu kusafiri kwenda nje ya nchi.
Huu utakuwa ni uonevu mkubwa. Waamuzi wanatakiwa kuchezesha kwa haki bila kuzibeba timu kubwa, kongwe, zenye uwezo wa kifedha, au za Ligi Kuu dhidi ya timu ndogo.
Ushindi unatakiwa uende kwa timu zilizojipanga vema kwenye mechi husika na si kuangalia jina la timu.
Hii ni michuano ambayo pia huleta wachezaji wapya kwenye tasnia ya soka nchini kutoka mitaani na kusajiliwa kwenye timu mbalimbali za Championship na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ndiyo michuano iliyobaki kuwapata wachezaji chipukizi, wenye vipaji ambavyo vimejificha badala ya Kombe la Taifa ambalo kwa sasa halipo na kama lipo halina umaarufu kama zamani.
Na kwa kuwa ni kipindi cha dirisha dogo, timu za Ligi Kuu ukiondoa labda Simba, Yanga na Azam, zinaweza zikawaona baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kuwaongeza kwenye vikosi vyao.
Kutokana na hilo nawaomba tu waamuzi wachezeshe kwa haki ili tuone vipaji murua, badala ya 'kuzinyonga'.
Timu ndogo inaweza kuwa na wachezaji wazuri, lakini kutendo cha kutoichezesha kwa haki kinaitoa timu hiyo mapema wakati watu walitaka kutazama tena uwezo wa wachezaji, kinaweza kuwakera na kuwapa msongo wa mawazo wachezajivijana wakaona kumbe soka si mchezo wa haki unaoweza kuwapa maendeleo, hivyo kuamua kuachana nao wakaenda kufanya kazi zingine.
Ni ukweli usiopingika kuwa wapo wachezaji wengi vijana wameachana na soka kutokana na tabia ya waamuzi kuzionea timu zao, wakati wao wanataka kuonekana na 'kutoka', lakini wanabaniwa kwa kutochezeshwa kwa haki.
Afadhali kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Championship, kuna wachezaji wazoefu na waliokomaa kiakili, hivyo hata wakikutana na mambo haya wanajua jinsi gani ya kufanya kwa sababu wanakutana nayo sana kwenye mazingira tofauti.
Haki ni haki, hata kama ushindi unakwenda kwa timu ambayo haiwezi kusafiri kwenda hata Kenya, lakini ipate haki yake na viongozi wao ndiyo waseme kuwa hawawezi kucheza michuano ya kimataifa na kusafiri, siyo wengine kuwasemea kwa kuwachezesha vibaya, kuwahujumu ili wafungwe. Timu zote ni sawa, na zichezeshwe kwa haki ili apatikane mshindi halali.