Bila elimu ya maadili   ukatili utaumiza taifa

04Oct 2022
Golden Kisapile, TUDARCo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
    Bila elimu ya maadili   ukatili utaumiza taifa

NYAKATI hizi Watanzania wameshuhudia matukio mbalimbali ya ukatili wa kila aina ukiwamo wa kijinsia, kutoka mikoa karibu yote, ambayo huenda chanzo cha haya yote chaweza kuwa ukosefu wa maadili hasa kwa wanaotenda uovu huo.

Kuna matukio ya wazazi kuua watoto, wanandoa kuuana na hata kuangamiza familia zao, watu wazima kunajisi watoto na panyaroad kujeruhi, kuua na kupora mali za watu mijini.

Aidha, wapo wanaohusishwa na mauaji na wengine kwa madai ya kuwa na hasira kali au kujichukulia sheria mkononi kupiga mawe wahalifu na kuwaua lakini, watoto nao wakiwaua wazazi kwa madai ya kutaka urithi.

Pengine yafuatayo yanaweza kuwa suluhisho la ukatili huu ambao umekithiri mno katika taifa letu  ambalo pamoja na kuathiriwa na utandawazi pia lina kundi kubwa la watu wasiopenda kufanyakazi kwa bidii.

Nianze kwa kutoa rai kwa Wizara ya Elimu kuangalia uwezekano wa kuingiza somo la kuukabili ukatili wa kijinsia katika mitaala ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Ninaamini hili linaweza kusaidia watoto kuufahamu ukatili, vyanzo vyake na hivyo kupunguza uovu huo kwa sababu mtu anakuwa na uelewa wa madhara tangu akiwa mdogo.

Pili, kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu, kuboresha mikakati mbalimbali kama vile kutoa elimu kwa upana zaidi na kutumia wadau kuanzia viongozi wa vijiji, dini, makundi maalumu na kualika wageni mahsusi kutoa muhadhara.

Watafahamu athari za ukatili katika jamii, kupitia wataalamu wa wizara na wadau hivyo kupunguza ukatili wa aina zote ukiwamo wa kijinsia katika jamii kwa ngazi mbalimbali.

Kupitia mashirika ya kiserikali na ya kiraia serikali iongeze nguvu ikiwamo bajeti za kufunza wananchi katika ngazi mbalimbali ikitumia washa,  semina na makongamano hata mikutano  inayofikia ngazi zote kwa lengo la kufundisha na kubadilisha jamii ili kupunguza madhara ya ukatili wa kijinsia.

Uwe ni mkakati wa kitaifa, mikoani, wilayani, kata na vijijini ili kukomesha ukatili ambao kila mara unakua na kuota mizizi ambayo ni pamoja na kuangamiza maisha.

Viongozi wa dini wanatakiwa kutumia majukwaa yao ya kidini kufundisha na kukemea ukatili ambao unaendelea kutokea katika jamii, hii itasaidia kukemea na kurekebisha hali katika jamii na maeneo mengine.

Wanahabari na wadau wa mawasiliano nao wana jukumu kwenye kuandaa maudhui na vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari kuanzia redio, runinga, machapisho ya aina zote, mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp, Blog, redio na runinga za kijamii.

Aidha, watoe matangazo kwenye vipaza sauti vinavyozunguka mitaani ambavyo vinahusu kupinga, aina na athari za ukatili wa kijinsia katika jamii.

Yote yangesaidia watu kuelimika kwa kiwango kikubwa kwa sababu utandawazi umechangia kupotosha jamii pia, utafanikisha juhudi za kukomesha ukatili huo kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao ni utandawazi pia.

Aidha, Jeshi la Polisi nalo litumike pamoja na watu mashuhuri, viongozi wa kisiasa na wasanii, wafanyabiashara maarufu, wanamichezo na hata wageni wa kimataifa wasisahaulike kwani wanaweza kuwa chachu ya kupinga ukatili mbalimbali na kuwa na Tanzania yenye upendo.

Wazazi na walezi kutoa elimu ya ukatili katika familia zao, ni jambo jema pia, kuanzia baba, mama, mjomba, shangazi, bibi na babu wahusike  na malezi hayo.

Ninaamini  balozi wa kwanza kumwelimisha mtoto kuhusu madhara ya ukatili katika jamii ni mzazi, mlezi na familia anayoishi nayo, watimize wajibu wao.

Inamaana kila mmoja awe moto nyumbani na jamii wafunzwe, kupiga vita mambo kama vile vitendo vya ushawishi na ulaghai, lugha za vitisho dhidi ya mtu mwingine, ubakaji na unyanyasaji watoto wa kike na kiume, wazee, utumikishwaji wa watoto, vipigo hususan kwa mwanamke, ndoa umri mdogo, ukeketaji na mauaji ya wazee kuua wahalifu na  vitendo vyote vinavyoashiria ukatili ili Tanzania iwe salama kila mtu aishi kwa amani.