Tuhuma  kujikopesha PSSF zinawashtua wanachaama 

14Sep 2022
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuhuma  kujikopesha PSSF zinawashtua wanachaama 

KWENYE uwanja wa habari zipo taarifa za madai ya  kuhojiwa  kwa  Mkurugenzi wa Ununuzi  na  Ugavi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF), akihusishwa na matumizi mabaya ya Shilingi  milioni 193.

Baraza  la Maadili la Taifa ndilo limemhoji kiongozi huyo  kutokana na matumizi hayo ambayo kati ya fedha hizo Shilingi  milioni 193 amejikopesha milioni 117.88 hatua ambayo inatajwa kuwa ni kinyume cha sera ya mkopo wa PSSSF, huku ikidaiwa kuwa ametumia  fedha hizo kununua gari binafsi.

Inaelezwa kuwa alipewa fedha kwa ridhaa ya  Kamati ya Mikopo ambayo mkurugenzi huyo ni mjumbe wa kamati hiyo  ya sera ya mikopo ya PSSSF ya mwaka 2018 .

Wakili wa Serikali Hassan Mayunga anahoji iweje mkopo huo uidhinishwe na kupitishwa haraka bila kufuata taratibu? Kwa upande wake kiongozi huyo   akiongozwa na wakili wake amezikana tuhuma hizo akidai kuwa alifuata utaratibu ili kupata mkopo huo.

Hizo ni taarifa ambazo pengine kutokana na  jukumu ambalo PSSSF inahusika nalo kwenye jamii hasa kwa  wanachama wake linaongeza mapigo ya moyo. Ni  kwa kuwa ni wazi kunazuka maswali mengi ikiwamo ni namna gani fedha zao zipo salama kama  mtu mwenye dhamana  hiyo anatuhumiwa kuzitumia pengine kwa njia inayohitaji kuhojiwa.

Kuanzishwa kwa PSSSF Oktoba 20,  2017  kunakuja baada ya serikali kupitisha uamuzi wa kuunganisha Mifuko ya Pensheni ya PSPF, LAPF, GEPF na PPF na kuunda mfuko mmoja wa PSSSF kwa ajili ya watumishi wa umma, na sheria inayoanzisha taasisi hiyo kupitishwa na bunge Januari 2018.

Wanachama wa mfuko huu wapo kwenye sekta mbalimbali ni kulingana na utumishi wao, ambapo  serikali kwa nia njema  iliona ni vyema kuanzishwa kwa mfuko huo ili kuwajengea mazingira ya kuishi kwa utulivu mara baada ya kustaafu ama wanapokumbana na changamoto nyinginezo zinaweza kufuata baada ya maisha ya kazi.   

Kuibuka kwa tuhuma kama hizo siyo habari njema  maana zinazusha hofu na maswali kadhaa, pengine hata kusababisha manung’uniko miongoni mwa wanachama wastaafu wanaosaka mafao yao kwa muda mrefu na hata wanachama wanaoendelea kuchangia fedha zao.

Lakini pia,  inaweza kuyumbisha nia njema ya serikali ya uhifadhi salama wa fedha hizo, hivyo  inapaswa ifuatiliwe  kwa umakini na ukweli ujulikane ili sheria ifuate mkondo wake.

Lakini, pamoja na utaratibu wa kisera na kisheria wa kuchukua mikopo ni jambo la hekima na busara kuwa na miiko na maelekezo ya kupata mikopo hiyo ambayo wanachama wenye fedha zao hawatajihisi vibaya au kulalamikia kile kinachofanyika kwenye akiba zao.

Ni jambo jema kwa Baraza  la Maadili la Taifa kuchukua hatua  hiyo kudhibiti na kuhakiki mienendo ya viongozi. Baraza lipo chini ya  Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo inafanya kazi kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama inavyoelekezwa na Katiba ya Tanzania ya 1977.

Katiba  inalipa bunge mamlaka ya kuweka misingi ya maadili ambayo yatafafanua nafasi za madaraka ambazo watu wenye kushika nyadhifa  hizo watahusika nayo, aidha itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao.

Pia kipo kipengele  cha kupiga marufuku mienendo na tabia inayosabababisha  kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au anaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au anahatarisha maslahi au ustawi wa jamii na kingine kinataka kufafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi ya maadili.

Wakati katika kipengele kimojawapo kinabainisha kuwa  baraza hilo litaweka masharti mengine yoyote yanayofaa au ambayo ni muhimu kwa madhumuni ya kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali nyinginezo za Umma.