Simba msitumie mechi za kimataifa kujaribu wachezaji

12Sep 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba msitumie mechi za kimataifa kujaribu wachezaji

KWENYE mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC, wanachama na mashabiki wa Simba walichachamaa na kucharuka, wakitaka Kocha Msaidizi Selemani Matola ajiuzulu kwa madai kuwa hawana imani naye.

Hapa naomba nieleweke, nilivyowasikia na kuwasoma wanachama na mashabiki wa timu hiyo siyo kwamba Matola si kocha mzuri, la hasha, ila hawana imani naye.

Hali ilikuwa mbaya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC kwenye mechi ambayo wachezaji walicheza kana kwamba walishacheza soka miaka mingi iliyopita na wamestaafu na hiyo ilikuwa ni bonanza wakijikumbushia enzi zao tu.

Hakuwakuwa na ari, nguvu, kasi, wala kitu chochote kile ambacho kinaweza kukupa picha kama wanaoonekana uwanjani ni wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tena wa timu kubwa kama Simba.

Ndiyo maana wengi walikata tamaa hata kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets kama timu itafanya vizuri.

Labda kwa kuliona hilo na mengineyo, viongozi wa Simba wakamchukua kocha mkongwe Juma Mgunda kuchukua kijiti hicho kwani ilikuwa ni siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na kocha wake, Zoran Maki.

Hiki ni kipindi kigumu na cha mpito kwa klabu hiyo, kwani Mgunda ni kocha wa muda wakati ikisaka kocha mwingine atakayekuja kuwa kocha mkuu.

Mimi si mtabiri, lakini nadhani atakapokuja kocha, Mgunda ana nafasi kubwa ya kuwa kocha msaidizi kwenye kikosi hicho.

Kama alivyowahi kusema Kocha wa sasa wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge kuwa linapokuja suala la mechi za Ligi ya Mabingwa, Simba inakuwa ni timu nyingine kabisa na si ile inayoonekana kwenye Ligi Kuu.

Alisema ukiipeleleza Simba ili kujua jinsi gani ya kuidhibiti tafuta video zake za mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ili ukabiliane nayo, lakini ukichukua za Ligi Kuu itakula kwako, kwani haipo kama vile inavyokuwa kimataifa. Kwenye Ligi Kuu inacheza kawaida, sana lakini ikiwa kimataifa inabadilika na kuwa timu ya kutisha.

Na ndivyo ilivyokuwa, kwani ikiwa ugenini nchini Malawi ilishinda mabao 2-0.

Nilichokiona ndicho kilichonifanya niandike hili. Baada ya mechi dhidi ya KMC, baadhi ya madai ya mashabiki ni kwamba kwa sasa kwa sababu Matola ana nguvu baada ya Zoran kuondoka, basi tutaona baadhi ya wachezaji ambao hawajacheza hata siku moja wanacheza. Tunaona hata wachezaji ambao hawako fiti sasa watacheza.

Nikajua tu ni wale ambao wanaongea tu bila kujua wanachokisema, au wanafuata mkumbo, lakini kwenye mechi dhidi ya Nyasa Big Bullets nikamkumbuka shabiki yule.

Moja ya mabadiliko ambayo yaliiumiza Simba na kusababisha kushambuliwa sana kipindi cha pili ni kuingia kwa Erasto Nyoni baada ya kutoka Sadio Kanoute. Ilinishangaza. Hata wale tuliokuwa nao tunaangalia mpira kabla hata hawajaingia walianza kuwa na wasiwasi na mabadiliko hayo, pamoja na ya John Bocco.

Kilichotokea ni kile kile ambacho watu walikuwa na wasiwasi nacho. Hakuna chochote alichofanya Nyoni kwenye mechi hiyo. Hakuonekana kwenye tukio lolote muhimu zaidi ya kukimbia kivivu uwanjani, kuchukua mpira na kutoa pasi. Aliingia kama kiungo mkabaji, lakini hakukaba mtu yeyote. Kazi ya ziada sasa ilifanywa na Mzamiru Yassin aliyeanza mechi tangu mwanzo alikuwa uwanjani muda wote lakini alionekana kufanya vema kuliko aliyeingia kumsaidia.

Kwa bahati nzuri Bocco alifunga bao kwa msaada mkubwa wa Clatous Chama, lakini ukiondoa hilo hakuwa na madhara sana.

Naweza kusema kuingia kwa Nyoni kuliwafanya wenyeji kupata mwanya wa kulishambulia lango la Simba kama nyuki, kiasi cha kuwafanya kina Mohamed Ouattara, Henock Inonga ambaye aliacha kabisa masihara yake kwenye mechi hiyo, Israel Mwenda aliyekuwa kwenye kiwango cha juu, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' na kipa wao Aishi Manula kufanya kazi kubwa kuzuia hatari zote.

Hapa kuna swali. Unamtoaje Kanoute ambaye alikuwa mchezoni vilivyo huku akiwa hana hata kadi ya njano na kumwingiza Nyoni asiye na kasi na hana asili ya kiungo mkabaji mpambanaji kwenye mechi kama hiyo ya ugenini na timu imezidiwa? Nyoni ambaye hakucheza mechi yoyote hata ya ligi akaingizwa kwenye mechi ya kimataifa ngumu kama ile?

Ukweli ni kwamba kuwaingia wachezaji ambao hawajacheza hata mechi za Ligi Kuu kwa dakika 90 mechi za kimataifa ni hatari na ni kama kujitoa muhanga.

Kocha Mgunda na Matola wanapaswa waliangalie sana hili kwenye mechi zijazo kama wanataka kulinda heshima yao. Imeonekana kabisa kuwa Simba ina mapungufu makubwa kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na anayeonekana mwenye kiwango ambacho mashabiki wanaridhika nacho ni Kanoute peke yake. Kuna siku Zoran alituonyesha kuwa mbali na Nassor Kapama na Victor Akpan, Peter Banda anaweza pia kutumika kwenye nafasi hiyo, kwa nini hakuingizwa kusaidiana na Kanoute au Mzamiru? Na alipoingizwa akapelekwa pembeni?

Nadhani makocha wa Simba kwa wakati huu wawe makini sana hasa Matola ambaye ninaamini ndiye anayeijua timu zaidi na mshauri mkubwa wa Mgunda, kwani inaweza kuonekana ni kweli kama baadhi ya watu wanavyosema kuwa ana wachezaji wake. Kwa sasa mashabiki watavumilia tu kwa sababu wameshinda, ila matokeo yangekuwa tofauti!!! Sijui.