Tuache vyombo vya sheria vifanye kazi yake

06Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuache vyombo vya sheria vifanye kazi yake

WIKI hii kumeibuka mambo makubwa mawili kwenye klabu ya Simba ambayo kwa nyakati tofauti yameteka hisia za mashabiki na wanachama wa klabu hiyo pamoja na wadau mbalimbali wa soka.

Suala la kwanza, Simba iliandika historia baada ya wanachama wake kukubali kufanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo kongwe nchini ambayo imeanzishwa miaka 80 iliyopita.

Tukio hilo la kwanza wiki hii la klabu hiyo lilichombezwa zaidi na mfanyabiashara bilionea, Mohamed Dewji ambaye alitangaza kununua hisa za asilimia 51 na kutaka kuwekeza kiasi cha shilingi Bilioni 20 katika mpango huo wa kuibadili

Simba kuwa Kampuni, mbali na hilo pia alitoa kiasi cha Sh. milioni 100 kwa viongozi ili kisaidie kufanya usajili wa wachezaji wa kimataifa katika hatua hii ya mwisho kuelekea kwenye ligi kuu msimu huu iliyopangwa kuanza Agosti 20.

Wakati mashabiki wa Simba wakisherehekea hatua hiyo na kuwafanya wapinzani wao kuwa kimya, limeibuka suala la Rais wa klabu hiyo Evans Aveva kukamatwa na kuwekwa ndani kwa mahojiano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa

(Takukuru) akituhumiwa kuchepusha fedha za mauzo ya mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Emmanuel Okwi aliyeuzwa mwaka 2013 kwa klabu ya Etoel du Sahel ya Tunisia kutoka kwenye akaunti ya klabu na kuingia kwenye akaunti binafsi ya Rais huyo.

Mengi yanazungumzwa juu ya suala hili huku wengine wakielekeza shutuma zao moja kwa moja kwa Rais Aveva na wapo ambao kwenye mitandao ya kijamii wamefanya hukumu na kumuita Aveva kuwa ni mwizi.

Nipashe inaamini suala hili ni la kisheria na lipo mikononi mwa taasisi za kisheria wakifanya uchunguzi wao.

Bado hakuna taarifa rasmi ya hatma ya jambo hilo iliyotolewa na Takukuru au jeshi la Polisi na hii inatokana na ukweli kuwa vyombo hivyo bado vipo kwenye uchunguzi wa jambo hili na ndio maana bado wanaendelea kuwahoji wahusika wote.

Tunafahamu jambo hili limeteka hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, lakini si vizuri kutoa shutuma na kufanya hukumu moja kwa moja wakati bado uchunguzi ukiendelea kwa vyombo husika.

Nipashe inawashauri mashabiki, wanachama wa Simba pamoja na wadau mbalimbali wa soka kuacha sheria ifanye kazi yake kwanza kwa vyombo hivi kuendelea na upepelezi wao.

Tunaamini baada ya upelelezi kukamilika ukweli wa jambo hili utajulikana hivyo ni vyema tukazuia mihemko katika sakata hili na kupisha uchunguzi ufanyike.

Kwa sasa hakuna haja ya kuwaita wahusika majina ya ajabu kama wezi, wapigani na mengine kama hayo wakati uchunguzi haujakamilika.

Nipashe haitetei mtu lakini tunashauri tusubiri majibu ya mwisho ya taasisi zinazofuatilia jambo hili na baada ya hapo ndipo mashabiki, wadau wa soka watakuwa na wigo mpana wa kulizungumzia.

Tayari wahusika wanaendelea kuhojiwa mmoja mmoja tunashauri kuwe na subira katika jambo hili kwa kuwa Nipashe inaamini ukweli utajulikana kwa sababu kwenye ukweli uongo ukaa pembeni.

Wapenda soka tuache vyombo vya sheria vifanye kazi yake, tuwe na subira kwa kuwa mwisho wa siku ukweli wa mambo yote utajulikana.