Lengo la kutolewa kwa angalizo hilo ni kuhakikisha kwamba makao makuu hayo ya Serikali hayapatwi na tatizo hilo la kuwa na makazi holela.
Katika mahojiano maalumu yaliyochapishwa na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), Paskas Muragili, alisema kuwa hadi sasa, tayari wameshapima maeneo ya kutosha kwa ajili ya makazi na kwamba, yeyote anayetaka kujenga anapaswa kuhakikisha kuwa anapata eneo lililopimwa.
Aidha, habari njema kwa wote wanaotarajiwa kuhamia Dodoma kuanzia mwezi ujao ili kutekeleza amari ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (ya kuhamia mjini humo kufikia Septemba), ni kwamba viwanja rasmi hupatikana kwa bei nafuu.
Sisi tunadhani kwamba ni muhimu kwa wale wote watakaohamia mjini Dodoma kuzingatia kwa vitendo maelekezo ya CDA.
Sisi, Nipashe, tunasisitiza jambo hili kutokana na athari kadhaa zitokanazo na ujenzi holela. Ni kwa sababu, kama ilivyojidhihirisha katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini, ujenzi usiozingatia matakwa ya mipango miji husababisha adha kubwa katika jamii.
Maeneo kama ya Tandale na Mburahati katika Manispaa ya Kinondoni, Buguruni na Vingunguti (Ilala) na Mbagala na Buza wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, ni mfano mmojawapo wa kile kinachohofiwa kuhusiana na athari za ujenzi holela wa nyumba za makazi na majengo mengine.
Maeneo ya aina hiyo hukosa mvuto, ijapokuwa nyumba zake zaweza kuwa nzuri na za kiwango bora. Nyumba hufuatana pasi na mpangilio kiasi kwamba, katika baadhi ya maeneo hayo, eneo la choo cha nyumba moja ndilo pia huwa baraza ya nyumba nyingine.
Zipo nyumba nyingi pia hutenganishwa kwa mipaka ya kuta zao, kwa maana ya kukosekana walau upenyo wa kumuwezesha hata mtoto mdogo kupita.
Athari nyingine za ujenzi holela ni pamoja na miundombinu kwa ajili ya huduma muhimu za kijamii kwa wakazi wake kukosekana.
Siyo rahisi kushuhudia mfumo thabiti wa majitaka wala majisafi. Barabara huwa ni ndoto ya mchana na hivyo siyo rahisi pia kwa wakazi wa maeneo husika kufikiwa na magari ya zimamoto pindi janga hilo linapotokea.
Hata panapotokea misiba, wahusika hulazimika kufanya kazi ya ziada kufanikisha shughuli za mazishi. Utambuzi wa nyumba katika maeneo yaliyojengwa bila mpangilio huwa ni kazi iliyoshindikana pia kwa sababu ni vigumu kujua mahala pa kuanzia na kumalizia ili hatimaye kuzipatia anuani.
Kwa ufupi, athari za kuwapo kwa ujenzi usiozingatia ramani za mipango miji ni nyingi. Ni kwa kuzingatia hilo, ndipo sisi tunapoona kwamba ni kweli, kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa kila anayehamia Dodoma na kuwa na ndoto za kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba ya kuishi yeye na familia yake, ni lazima ahakikishe kuwa anafanya hivyo katika maeneo rasmi yaliyopimwa.
Muhimu kuliko yote, ni kwa CDA na mamlaka nyingine zinazosimamia ustawi wa makao makuu Dodoma kuhakikisha kuwa sheria na kanuni zilizopo zinafuatwa kwa kila anayetaka kujenga mjini humo. Ikumbukwe, hata mbuyu ulianza kama mchicha.
Wala haitashangaza kuona kuwa Dodoma ikiwa kama Tandale, Vingunguti Kiembe Mbuzi na Mbagala Maji Matitu ikiwa usimamizi makini hautafanyika katika hatua hii ya awali ya ujio wa maelfu ya watu watokanao na uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Hilo lizingatiwe.










