Maandalizi Ligi Kuu Bara yaendane na uhitaji halisi

30Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Maandalizi Ligi Kuu Bara yaendane na uhitaji halisi

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu mpya wa 2022/ 2023 linatarajiwa kufunguliwa rasmi ifikapo Agosti 17, mwaka huu kwa timu zote 16 zinazoshiriki kuanza mbio za kuwania taji hilo linaloshikiliwa na Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Yanga ilitwaa ubingwa huo kwa kuwavua watani zao, Simba ambao walikuwa wanaushikilia ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Mshindi wa taji hilo na timu inayoshika nafasi ya pili, zinapata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Msimu uliopita, Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, raia wa Tunisia ilitwaa ubingwa huo kwa kuweka rekodi ya kutofungwa, lakini ikijihakikishia ubingwa ikiwa imebakiza mechi tatu mkononi.

Hata hivyo, kazi kwa Yanga haikuwa nyepesi, ilikutana na changamoto mbalimbali katika mbio hizo za kutimiza malengo yake.

Yanga ilipambana katika kila mechi, ikiweka msimamo kwamba kila mchezo kwake ni fainali na kauli mbiu hiyo ilichangia kuongeza morari kwa wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki.

Hata hivyo Yanga haikufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya CAF kwa kutolewa kwenye hatua za mapema wakati wapinzani wao, Simba wakiishia hatua ya robo fainali.

Ili kila timu ifike malengo, huu ni wakati wa kuhakikisha zinafanya maandalizi kwa mujibu wa programu zilizoandaliwa na viongozi wa benchi la ufundi.

Mpira wa miguu ni mchezo wa wazi na usiohitaji au usiotegemea miujiza, unatakiwa kuiandaa vyema timu yako ili kutarajia kupata matokeo chanya na si vinginevyo.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuzikumbusha timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake Nchini kufanya maandalizi sahihi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ushindi na hatimaye kuwania mataji.

Ukiondoa vita ya kuwania ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, lakini klabu zikumbuke kumaliza kwenye nafasi za juu na hatimaye kuondoka na fedha 'nono' zinazotolewa na mdhamini mkuu, Benki ya Taifa ya Biashara pamoja na Kampuni ya Azam Media inayotoa motisha hadi kwa klabu inayoshuka daraja.

Kama timu zilikuwa zikijiandaa na kufanya usajili wake bila ya kuwa na zawadi hiyo kutoka Azam Media, je sasa zinapopokea fedha hizo, ni vyema viongozi wakazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Ni wazi timu inayokosa maandalizi, hujiweka katika janga la kukaa mkiani lakini pia kuwa kwenye presha ya kushuka daraja.

Ilishatangazwa dirisha la usajili  litafungwa rasmi ifikapo Agosti 31, mwaka huu, tunawakumbusha mwezi mmoja uliobakia utumike vyema kukamilisha mchakato wa usajili lakini wiki mbili kuelekea msimu mpya ukamilishe maandalizi ambayo yanatarajiwa yataimarisha vikosi vyenu.

Ni wazi ubora wa vikosi husaidia kuongeza ushindani kwenye ligi na kumpa nafasi kubwa Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, wepesi wa kuteua wachezaji kwa ajili ya timu yake.

Tunafahamu ili maandalizi yafanyike kwa kiwango bora, kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika na baadhi ya timu hazina wadhamini wa kusaidia kugharamia huduma hizo muhimu, lakini hilo halihalalishi wasimamizi wa timu kupeleka mambo kwa mazoea.

Wachezaji pia kuweni makini katika kusaini mikataba na timu ambazo hazina uhakika wa kupata nafasi ya kucheza.

Wachezaji mnatakiwa kuwahusisha mawakala au wanasheria wenu nakala za mikataba kabla ya kusaini mikataba ili kujiweka mahali salama na kujiepushia uonevu kwa kuvielewa vyema vipengele vilivyokuwa kwenye mikataba hiyo.

Viongozi wa klabu watendeeni haki wachezaji wenu kwa kuwapa vifaa bora lakini pia kuwalipa haki zao kwa wakati ili akili zao zitulie na kujikita katika mazoezi pekee ili kutorudisha nyuma vipaji vyao.