Hongera TFF, wadhamini kwa kuchagiza ushindani

09Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hongera TFF, wadhamini kwa kuchagiza ushindani

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/2022 ulimalizika Juni 29, mwaka huu kwa timu zote 16 zilizokuwa zinachuana kushuka dimbani kumalizia ngwe yake kwa mujibu wa kanuni, kwa sababu tayari mshindi bingwa aliyekuwa anatafutwa alishajulikana.

Bingwa huyo si mwingine, ni Yanga ya jijini Dar es Salaam ambayo imemaliza msimu bila ya kufungwa mechi hata moja.

Kama ilivyo kanuni, msimu mpya hufunguliwa na mechi ya Ngao ya Jamii, basi pazia la msimu husika hukamilishwa na hafla ya kukabidhi tuzo kwa wachezaji, waamuzi, wadau na viongozi mbalimbali waliofanya vizuri.

Sherehe hizo zilifanyika jijini juzi usiku na kuhitimisha rasmi safari ya msimu uliopita kwa kukabidhi tuzo kwa waliofanya vizuri lakini pia walioutendea haki mchezo wa soka nao walipata Tuzo za Heshima kutoka kwa Rais wa TFF, Wallace Karia.

Utolewaji wa tuzo hizo unaweza kuonekana kama hauna maana kwa baadhi ya wadau kwa sababu majibu yake hujulikana wakati tayari wameshamaliza msimu lakini ni kweli tuzo hizo zinachangia katika kukuza maendeleo ya mchezo huo unaopendwa zaidi duniani.

Wachezaji wamekuwa wakipambana kufanya vizuri kwa sababu wanafahamu mwisho wa msimu watapata tuzo na zawadi kutoka kwa wadhamini mbalimbali waliopo kwenye mashindano wanayoshiriki.

Tuzo zimekuwa ni moja ya kichocheo muhimu katika kuongeza na kukuza viwango vya wachezaji kwa sababu wanaamini mbali na kujiongezea soko kuelekea dirisha la usajili, lakini heshima wanayopata baada ya kutangazwa washindi imesaidia kuwaimarisha kwa ajili ya msimu unaofuata.

Wakati msimu unaanza, wachezaji kila mmoja huzungumza amejipanga kuisaidia timu yake kufanya vizuri huku wengine wakiweka wazi wanahitaji kumaliza msimu kwa kutwaa ubingwa au kwenye nafasi nne za juu, lakini kadri mechi zinavyozidi kuchezwa, fikra na malengo hubadilika na hapo ndio ushindani huonekana.

Kwa mfano katika tuzo ya Mfungaji Bora iliyochukuliwa na mshambuliaji wa Geita Gold FC ya mkoani Geita, George Mpole aliyepachika wavuni mabao 17, awali ilionekana kama itabebwa na staa wa Yanga, Fiston Mayele, mafanikio ya mshindi huyo wa tuzo, kuliwafanya wachezaji hao wawili kuongeza juhudi kila waliposhuka dimbani na ushindani huo ulichangia kuiongezea thamani Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ni ukweli usiofichika, idadi ya mashabiki waliokuwa wanaifuatilia Geita Gold ikicheza, iliongezeka kwa sababu tu walikuwa na mchezaji anayeshindana na nyota kutoka kwa waliokuwa vinara wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Lakini kubwa lililoifanya ligi iliyomalizika kuwa tamu ni zawadi ya fedha zilizotangazwa kutolewa na Kampuni ya Azam Media, ambayo imepewa haki za matangazo ya televisheni. Msimu huu timu zote zimevuna fedha, lakini kiasi kikitofautiana kulingana na nafasi ambayo timu yao imemaliza kwenye msimamo wa ligi.

Licha ya mafanikio yanayoonekana kupitia tuzo hizo, TFF kupitia Kamati ya Tuzo, msisahau kuyafanyia kazi maoni mbalimbali yanayotolewa na wadau ambao kwa kiasi kikubwa yanalenga kuzifanya tuzo hizo kuwa bora na kufikia kule walipokusudia.

Hata hivyo, msimu huu bila kuelezwa chochote, tuzo ya Mhamasishaji Bora ambayo msimu uliopita ilitolewa kwa mdau, Bongozozo aliyeshinda, haikuwa moja kati ya tuzo 43 zilizotolewa mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa.

Inaweza kuwa ni maboresho kama ambavyo tumeshuhudia kwa mara ya kwanza tuzo mpya wachezaji waliofanya vizuri katika Ligi ya Championship na First League. Tunaamini mabadiliko hayo yamefanyika kwa maslahi na afya ya soka na si vinginevyo.

Tunahitaji kuona msimu ujao wachezaji, timu na maofisa wote wanaoshiriki katika ligi zote zinazosimamiwa na TFF wanaendelea kujipanga kufanya vizuri kwa sababu wanaamini mwisho wa msimu watakabidhiwa tuzo ambazo baadhi yake zinafuatana na zawadi ya fedha.

Tunaamini ushindani huu wa kuwania tuzo za TFF, si tu unasaidia kukuza kiwango cha soka cha hapa nchini, lakini unakuwa ni sehemu ya kuziimarisha timu zetu zinazokwenda kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Hongera kwa washindi wote waliopata tuzo za msimu wa 2021/2022.