Tusikilize bajeti, tutoe maoni kwa wawakilishi wetu

14Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusikilize bajeti, tutoe maoni kwa wawakilishi wetu

LEO bajeti ya serikali ya kwanza tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi 2021, inasomwa ambayo itaonyesha mwelekeo wa mwaka wa fedha 2022/23 kwenye mapato, matumizi na miradi ya maendeleo.

Wananchi watajielekeza jijini Dodoma kusikiliza wapi kutapunguzwa kodi, kutaongezwa au vyanzo vipya ambavyo vitaleta ahueni ya maisha kwa wananchi, hasa baada ya bidhaa nyingi kupaa bei kutokana na mafuta kupanda.

Bajeti hiyo ndiyo inabeba mwelekeo wa nchi katika kukusanya na kutumia kwenye matumizi ya kawaida, mishahara na miradi ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Kubwa linalosubiriwa ni kusikia nafuu ya maisha kupitia kuondolewa kodi mbalimbali, ambazo kimsingi zimechangia bei ya mafuta kuzidi kupaa, na tayari Rais Samia, aliahidi hatua zaidi za kikodi zitatangazwa kwenye bajeti ya leo.

Mwezi uliopita mafuta yalishuka kidogo baada ya serikali kuingiza Sh. bilioni 100, ambazo zilileta nafuu ambayo bado haikusaidia bidhaa kushuka bei jambo ambalo wananchi waliona halijawagusa moja kwa moja.

Kwa miaka mingi bajeti imekuwa ikitegemea vyanzo vya mapato vya vinywaji baridi na moto ambavyo vimekuwa vikipanda, magari yanayoagizwa kutoka nje kiasi cha wabunge na wataalamu kuitaka serikali kuja na ubunifu kwenye eneo hilo.

Ipo ripoti ya Chenge One iliyopendekeza vyanzo vipya vya mapato, ikiwamo kuweka kodi kwenye uvuvi bahari kuu, lakini kutokana na gharama za uwekezaji bado nchi haijanufaika ipasavyo na vyanzo hivyo.

Kiu ya wananchi ni kusikia kama ni kicheko au maumivu zaidi kutokana na kuongezeka kwa kodi kwenye bidhaa mbalimbali, namna gani bidhaa za ndani zinalindwa, ili kuvutia zaidi wazalishaji na uwekezaji.

Lakini kuona miradi ya kimkakati kama bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, reli ya mwendokasi (SGR) itakamilika, lakini ujenzi wa miundombinu mingine ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Bajeti hii itakwenda kuonyesha namna keki ya taifa itakusanywa na kugawanywa kwa usawa kwa Watanzania wote, ili kila mmoja ajisikie ni sehemu ya nchi kupitia miradi ya maendeleo na huduma za kijamii ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Lakini kodi anayolipa inakwenda kwenye mfumo sahihi na inarudi kwake kupitia ujenzi wa huduma za kijamii kama shule, hospitali, zahanati, miundombinu na maji ambayo ni vya msingi kwa kila mmoja.

Ni muhimu Watanzania wakaisikiliza bajeti hiyo kwa kina itakaposomwa saa 10 kamili alasiri, ili kujua serikali imejipangaje na kodi zimeongezeka wapi.

Wapate pia nafasi ya kuwashauri wawakilishi wao katika muhimili huo nini cha kuchangia wakati wa kuchambua bajeti hiyo kwa siku tano, ili wanaposimama wawe na la kuzungumza.

Pia ni vizuri wabunge wakawataka wananchi wa majimbo yao kusikiliza bajeti na kuwasiliana na wachache, ili kuwashauri ni hoja gani wazichambue kwa maslahi mapana ya wananchi wa jimbo na taifa kwa ujumla.

Naamini wabunge wana makundi ya mtandaoni ya wananchi wao, ni muhimu kuwahamasisha kusikiliza bajeti na kutoa maoni yao ili kwa siku mbili wanazopewa wabunge hao kwa ajili ya kutafakari kupata hoja za kuchangia ambazo zitasaidia maboresho ya bajeti.

Bajeti kikomo ya mwaka huu ni Sh. trilioni 41.063 kwa mwaka 2022/23, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na bajeti ya Sh. trilioni 37.980 mwaka 2021/2022.

Kati ya fedha hiyo Sh. trilioni 25.542 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia 62.2 ya bajeti yote, ikiwa ni Sh. trilioni 11.308 kwa ajili ya ulipaji deni la serikali na gharama nyingine.

Aidha, matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 15.521 sawa na asilimia 37.8 ya fedha yote, kati yake Sh. trilioni 12.22 fedha za ndani na Sh. trilioni 3.399 ni fedha za nje.