Ikumbukwe miamba hiyo tayari ina tiketi mkononi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao, michuano ambayo huandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Yanga ambayo inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 64 inafuatiwa na Simba yenye alama 51, pointi hizo zikiwa haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye msimamo ligi hiyo msimu huu, hivyo timu hizo zina uhakika wa kumaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili.
Hivyo, kwa kuzingatia ukweli kwamba msimu ujao Tanzania itawakilishwa na timu nne; mbili zitakazomaliza nafasi ya kwanza na ya pili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika, kwa itakayoshika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu kupata nafasi hiyo huku mshindi wa nne ikitegemea na endapo bingwa wa Ligi Kuu ndiye atatwaa Kombe la FA.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka nchini (TFF), mshindi wa Kombe la FA huiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kutokana na msimu huu Yanga ambayo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kutinga fainali ya FA Cup ikitarajiwa kucheza dhidi ya Coastal Union, endapo Coastal haitabeba taji hilo, basi timu itakayomaliza nafasi ya nne itaiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo ya CAF.
Hivyo, kutokana na wakongwe hao wa soka nchini, Simba na Yanga kuwa na uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa, zimekuwa zikihusishwa na wachezaji wengi huku jina la nyota wa Asec Mimosas ya Ivory Coast raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, likizidi kugonganisha vichwa vya habari kwa klabu hizo kubwa nchini.
Presha imekuwa kubwa kuanzia kwa mashabiki hadi viongozi wa klabu hiyo, kila mmoja akitaka kuona wanafanya usajili mkubwa wakuvutia kuelekea msimu ujao ambao miamba hiyo inaeleza kupania kufanya vizuri kimataifa.
Kutokana na presha hiyo, Nipashe tunaona kunauwezekano ikawapoteza viongozi wa klabu na wote waliopewa jukumu la kufanya usajili, wakajikuta wakisajili kwa ushindani wa nani zaidi badala ya kufuata maoni na mapendekezo ya mabenchi yao ya ufundi ili mwisho wa siku waweze kutimiza malengo waliowekewa.
Tumelazimika kukumbusha hilo hasa kutokana na uzoefu mkubwa tulionao katika kipindi cha usajili hususan kwa klabu hizo mbili, ambazo huishia kushindana katika mbio za usajili na mwisho wa siku kujikutana zikisajili wachezaji wengi wa nafasi moja na kusahau mapendekezo muhimu kutoka kwa makocha wao.
Ikumbukwe pia nafasi za kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi ni 12 tu, ambazo ni chache sana, hivyo viongozi wa Simba na Yanga hawana budi kuwa makini kwa kusajili wachezaji katika nafasi muhimu ambao wanaona ni nadra kupata wazawa wakukidhi viwango wanavyohitaji.
Tunataka kuona wachezaji wanaosajili kutoka nje wanakuja kutoa mchango mkubwa kwa klabu hizo na si kusajili wakuja kukaa benchi kutokana na kuzidiwa ama kuwa na ubora sawa na wazawa.
Hivyo, hiki si kipindi cha Simba na Yanga kuanza kukimbizana katika kuonyeshana jeuri ya fedha kuelekea dirisha la usajili, badala yake tunataka kuona kila klabu ikisajili kutokana na mapendekezo ya mabenchi yao ya ufundi ikiwa ni pamoja na wachezaji waliowafuatilia kwa muda mrefu.
Aidha, viongozi wa klabu hizo hawana budi kutumia vema nafasi hizo 12 kwa umakini mkubwa kwa kusajili wachezaji wenye viwango vya juu huku wakimulika kwa umakini historia yao ya majeraha ili kuepuka wale wakucheza mechi moja inayofuata wanakuwa nje ya uwanja wakijiuguza kwa kipindi kirefu.
Tunaamini kama klabu hizo kongwe nchini, zitaacha mashindano katika mbio za usajili na kufuata kile ambacho mabenchi yao ya ufundi yamependekeza, zinaweza kupata wachezaji wazuri watakaowasaidia kwenye michuano ijayo ya kimataifa na kufika mbali.
Lakini lengo letu ni kuona usajili unaofanywa unakuwa wa tija na kuzaa matunda kwa angalau msimu huu tushuhudie timu zaidi ya moja zikitinga hatua ya robo fainali, nusu na hatimaye fainali kwenye michuano hiyo ya CAF, na hilo litawezekana tu kama zitatuliza kichwa kuelekea kipindi hiki cha usajili na si kusajili kwa mashindano.










