Kila la heri Taifa Stars

04Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la heri Taifa Stars

TIMU ya Taifa ya Soka ya Tanzania, Taifa Stars, leo usiku inatatupa karata yake ya kwanza kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast mwakani, ikicheza na Niger.

Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa L'amitie jijini Cotonou nchini Benin kutokana na Niger viwanja vyake kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Stars inaingia kwenye mchezo huo ikiwania kuhakikisha inashinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi katika mechi nyingine za kundi lake la F.

Kama ambavyo nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta alivyosema wakiwa wanaondoka nchini juzi kuelekea Benin kuwa wamejiandaa vizuri kupata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri na morali ya kuendelea kufanya vizuri kwenye kundi lake, sisi pia tuna imani watafanya vizuri.

"Tunataka kuanza vizuri, na kwa bahati mbaya tunaanzia ugenini, lakini bahati nzuri pia ni kwamba iwapo tutashinda ugenini itakuwa imetupa morali kubwa ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi zinazofuata,” ilikuwa kauli ya Samatta wakati wakiondoka nchini.

Sisi tunajua kuwa mchezo huo hautakuwa rahisi kwa sababu hata Niger nao wanatamani kushiriki fainali za AFCON mwakani.

Hivyo ili kuhakikisha tunaipata nafasi hiyo, Stars lazima ipambane kwa nguvu zote kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini, ili watakapocheza hapa nyumbani iwe rahisi zaidi kwao.

Ikumbukwe kwamba, ukiwa unacheza ugenini unatakiwa kupambana kwelikweli kwa sababu ukipata matokeo mazuri ina maana kwamba, upo kwenye nafasi nzuri ya kufanya vyema zaidi nyumbani.

Hakuna kinachoshindikana kwa Stars kushinda ugenini, kwani wakati tukicheza kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Dunia tulishinda mechi ugenini, kwa hiyo imetupa kujiamini kuwa tunaweza kushinda popote hata kwenye michuano hii.

Stars itakuwa inacheza kwenye uwanja iliouzoea kwani Oktoba 10, mwaka jana, ilicheza dhidi ya wenyeji Benin na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Simom Msuva kwenye michuano ya kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Qatar.

Hivyo, Nipashe tunaimani kwamba, Stars haitakuwa mgeni sana wa uwanja huo hivyo inaweza kutumia mbinu walizotumia kwenye mchezo wa Oktoba 10, mwaka jana, kuweza kupata ushindi.

Stras ipo kundi F, pamoja na timu za Niger, Algeria, na Uganda ambazo zote sio za kubezwa, kwani zina wachezaji wakubwa na wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa, hivyo lazima wapambane kuhakikisha hawafungwi ugenini.

Stars ikifuzu michuano ya Afcon ya mwakani itayofanyika nchini Ivory Coast, itakuwa ni mara ya tatu, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na mara ya pili katika mashindano yaliyofanyika nchini Misri.

Hivyo kama uzoefu tayari Stars imeupata na hiyo maana yake ni kwamba, wanaweza kupambana vizuri na kupata ushindi kwenye mchezo huu wa kwanza na kujiweka kwenye mazingira mazuri kwa mechi zinazokuja.

Ushindi wa kwanza una faida kubwa kwa timu katika kuipa morali na kujiamini, hivyo kama Stars itapa ushindi kwenye mchezo wa leo, imani yetu ni kubwa kwamba, ina nafasi ya kusonga mbele kwenye mashindano haya makubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya nchi.

Ombo letu kwa wachezaji ni kuzingatia maelekezo waliyopewa na benchi la ufundi pomoja na kutumia ufiti na utimamu woa walioupata kwenye mazoezi ili kujiweka kwenye nfasi nzuri ya kushinda mchezo huo.

Hivyo, sisi tuna imani kubwa na Stars kwamba, inaweza kufanya vizuri na kuiwakilisha vyema nchi kwenye mashindano hayo ambayo yatafanyika kuanzia Juni 23 hadi Julai 23 mwakani.

Kila la heri Taifa Stars.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars.