Tunachukua hatua zipi kukabili sumu kutoka vipisi vya sigara?

02Jun 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tunachukua hatua zipi kukabili sumu kutoka vipisi vya sigara?

NI kawaida katika mazingira nchini, jamii imekuwa na kawaida kuona vipisi vya sigara vinavyotupwa kwenye maji au barabarani, hatujui madhara yake kwa afya za umma.

Tunaviona vipisi vya sigara vikiwa maeneo mbalimbali vimetupwa, lakini madhara yake hayajulikani kwa kina.

Kinachotakiwa sasa ni elimu hiyo iendelee kutolewa kwa watumiaji sigara pale wanapomaliza kutumia sigara zao, pia usahihi wa mahali pa kuhifadhi.

Hata kuhamia penye matumizi ya uvutaji holela wa sigara, napo kuna changamoto za kiafya kwa wanaouvuta moshi wa sigara hizo.

Wapo watu wenye tabia, wanavuta sigara katika kwenye kumbi za starehe, katika magari na majumbani. Kwa kufanya hivyo, ni hali inayowaathiri kiafya wote wanaoingiwa na moshi huo wa tumbaku.

Sigara imedumu kihistoria ni moja ya starehe, ambayo anayetumia anafurahi kwa kila anachokipata kupitia sigara hiyo.

Hata hivvyo, inaelezwa kwamba vishungi vyake ni kati ya vitu vyenye uchafuzi na sumu kubwa inayopatikana katika vyanzo vya maji. 

Katika hilo nina la kumrejea Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, wakati akitoa tamko kwenye maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani yenye kaulimbiu "Tumbaku: Tishio la Mazingira Yetu".

Waziri Ummy anasema kwamba, inamchukua muda mrefu kwa kitako cha sigara kuoza, hivyo kuruhusu nikotini na kemikali kuingia kwenye mifumo ya ikolojia inayozunguka, inayoathiri maisha ya binadamu. 

"Tafiti zinaonyesha kwamba vishungi vya sigara vinapowekwa kwenye maji, vinaweza kutoa kemikali ambazo huweza kusababisha vifo vya viumbe wa majini, wakiwamo samaki," anatamka waziri huyo mwenye dhamana.

Pia, ana la kuongozea kuwa ni takribani asilimia 65 ya wavutaji hutupa vishungi vya sigara barabarani, kwenye fukwe baharini, pia ziwani.

Vilevile, inatajwa plastiki zinazohusiana na sigara za kielektroniki ambazo zaidi ziko katika mataifa yaliyopiga hatua, huishia kutupwa kwenye mifereji ya maji na barabarani, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Nini kifanyike? Waziri Ummy ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), akitaka ifanye utafiti wa shisha kuwekwa dawa za kulevya kwa kushirikiana na Tume ya Dawa za Kulevya nchini.

"Maelekezo yangu ni kufanya tathmini ya bidhaa hizi ili kulinda afya za jamii, kwani kufanya biashara ya shisha ujue unafanya kosa la jinai, Sheria ya Kudhibiti  Matumizi ya Bidhaa ya Tumbaku nchini Sura ya 121 haijatekelezwa kikamilifu, TMDA mfanye tathmini kwa kina," akasema.

Pia Waziri Ummy anasema magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza, yamekuwa yakiongezeka kila siku, yakileta maradhi mbalimbali yanayosababishwa na matumizi holela ya bidhaa za tumbaku.

"Jamii inatakiwa kupunguza au kuacha  kabisa matumizi ya tumbaku au bidhaa zake kwa ajili ya afya zetu, kwani wanaotumia bidhaa ya tumbaku zaidi ya asilimia  50 wanafariki," anasema.

Kwa sasa nchini, kuna takribani vifo 14,700 kila mwaka vinavyotokana na matumizi ya tumbaku na asilimia 8.7 ya Watanzania sawa na milioni 2.6 wanatajwa kutumia tumbaku.

Anasema wengi huathirika na moshi wa sigara katika maeneo ya kazi, kwenye baa, kumbi za starehe na migahawa na utafiti umeonyesha asilimia 77 ya watu hao huvutishwa sigara kwenye baa, asilimia 31.1 kwenye migahawa na asilimia 13.8 majumbani.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaeleza bidhaa tumbaku husababisha vifo kwa takribana nusu ya watumiaji wake na zaidi ya watu takribani milioni nane hufa kila mwaka duniani kwa sababu ya kutumia tumbaku.

Anaeleza, jumla ya watu milioni saba ni zao la vifo vya matumizi ya moja kwa moja, wakati wengine milioni 1.2 wanatokana na utumiaji bidhaa za tumbaku usio wa moja kwa moja.