Ukiangalia hali ilivyo nchini,unaweza kudhani watu wanasikia lakini ujumbe unaingia sikio la kulia, unatokea sikio la kushoto, hakuna anayeona kuwa tumbaku ni kitisho. Ikimaanisha hakuna, kujali wala kutilia maanani.
Ni kawaida kuwakuta watu wanavuta sokoni, stendi za daladala, barabarani, shuleni na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa.
Katika mazingira hayo, hata wale wasiovuta, wanakula moshi wa sigara bila ridhaa yao na kuwa kwenye hatari ya kupata maradhi yanayosababishwa na uvutaji wa tumbaku. Wakati huu wa kilele inashangaza kuona kuwa jamii inazidi kupofuka kuhusu athari za tumbaku.
Moja ya malengo ya maadhimisho haya ni kuifanya jamii kutambua madhara ya tumbaku na kuwa makini na uvutaji wake ambao unachangia ongezeko la saratani na magonjwa sugu.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za kutaka kuinusuru jamii dhidi ya uvutaji au uvutishwaji wa tumbaku, inaonekana baadhi ya watu hawajaelewa umuhimu wake.
Hilo linatokana na ukweli kwamba, licha ya kuwapo kwa maelekezo ya kutovuta sigara kwenye mkusanyiko wa watu, uvutaji unazidi kuwa endelevu.
Juhudi zaidi zinahitajika kuelimisha umma tena kwa kuwafikia watu kwenye mikusanyiko na kuwaelezea madhara ya kutumia tumbaku ili waachane nayo.
Jitihada za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), za kulinda afya za Watanzania, ikiwakumbusha kuwa uvutaji wa tumbaku kwenye maeneo yanayotumiwa na watu wengi hairuhusiwi zinafanyika lakini hazizingatiwi ipasavyo.
Kifungu cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, sura 121 kimetafsiri maeneo ya umma kama mahali ambapo inatolewa huduma ya afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii.
Kwingineko ni katika shughuli za michezo au burudani, sehemu za huduma ya chakula, ofisi, vyombo vya usafiri wa aina zote, mabanda ya maonyesho, masoko na maduka makubwa.
TMDA inasema, katika sehemu za umma sheria inakataza uvutaji wa aina yoyote wa bidhaa za tumbaku na kuelekeza bango lenye maneno yanayosomeka,“hairuhusiwi kuvuta sigara".
Aidha, TMDA inafafanua kuwa, kifungu cha 13 cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, kimeruhusu uvutaji kwenye baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu ya juu, majengo ya ofisi, hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani ambayo yanapaswa kutenganisha vyumba au maeneo maalum ya kuvutia na kutovutia tumbaku.
Aidha, katika ufafanuzi wake, mamlaka hiyo inasema, kanuni ndogo ya 7 (1) na (2) ya Kanuni za Bidhaa za Tumbaku za mwaka 2014, inawataka wamiliki wa majengo yanayotumiwa na watu wengi kuweka vifaa vya kubaini moshi wa tumbaku na kuweka alama zinazosomeka, ‘jengo hili limefungwa mtambo wa kubaini moshi wa tumbaku’.
Hivyo, TMDA inawaagiza wamiliki, wapangaji na waendesha biashara ya majengo yanayotumiwa na watu wengi kuzingatia masharti yasheria na kanuni ilizoanisha.
Pamoja na hatua hizo, wapo baadhi ya wazazi na walezi ambao huwavutisha watoto wao moshi wa sigara, nao ingefaa waelimishwe.
Ni jambo la kawaida kuwapakata watoto huku wakivuta sigara au kuwa ndani ya magari yao huku wakivuta bila kutambua kuwa wanawaumiza.
Kwa hali hiyo, ni wazi kwamba elimu zaidi inahitajika kwa umma kuongeza uelewa wa madhara ya tumbaku.
Ni muhimu wauza sigara kutambua kuwa kila anayeuza naye ni mtumiaji, hata jirani yake naye anavutishwa pia.
Ukweli huo unatokana na mazoea ya kuuza sigara kwani kwa kila anayeziuza awe kwenye vituo vya mabasi, barabarani au dukani lazima awe na kibiriti, kwa ajili ya wateja wao wanaowahudumia na kuwarudishia wauzaji, watoto wao na walio karibu na muuzaji.
Uraibu huo sasa udhibitiwe usiumize wengine, hivyo suala la kutenga maeneo ya kuvutia tumbaku linahitaji kupewa Msukumo mpya.
Shirika la Afya Dunia (WHO) linataja mambo hatari kuhusu kuvuta tumbaku kuwa ni pamoja na kuua nusu ya watumiaji wake, hivi una haja nayo?



.jpg?itok=nfwjwDzv)







