Busara itumike kuepusha vurugu Polisi, Chadema

31Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Busara itumike kuepusha vurugu Polisi, Chadema

KUMEIBUKA tishio kubwa la kuwapo kwa vurugu baina ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Jeshi la Polisi.

Viongozi wakuu wa chama hicho kinachoshikilia nafasi ya pili kwa kuwa na wabunge wengi nchini wamesisitiza juu ya utekelezaji wa operesheni yao maalumu ya kisiasa iitwayo Ukuta huku vyombo vya dola vikipinga.

Kwa mujibu wa maelezo ya Chadema, operesheni hiyo inayotarajiwa kuambatana na mikutano ya hadhara na maandamano itafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao kama ilivyopangwa na kamwe hawatarudi nyuma. Kigezo cha Chadema katika kusisitiza juu ya jambo hilo kiko wazi. Kwamba, wanazingatia katiba na sheria za nchi zinazotoa fursa hiyo kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi limesisitiza mara kadhaa kuwa kamwe halitaruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano pasi na kujiridhisha juu ya kuwapo kwa usalama wa raia na mali zao.

Aidha, akiwa Manyoni mkoani Singida juzi, Rais John Magufuli amekuwa akikazia jambo hilo kwa kueleza kuwa kamwe, Serikali yake haitaruhusu kufanyika kwa siasa za aina hiyo.

Rais Magufuli alienda mbali kwa kusisitiza kuwa yeyote atakayekiuka maelekezo ya vyombo vya dola kuhusiana na kutifanyika kwa mikutano ya siasa wala maandamano, atadhibitiwa ipasavyo na hivyo, akawasihi wale wote wenye dhamira hiyo kuacha mara moja.

Siyo nia yetu, Nipashe, kutaka kujadili undani wa mvutano uliopo. Bali, tunadhani kwamba iko haja kwa pande zote kuhakikisha kwamba amani na utulivu uliopo nchini unadumishwa kwa mustakabali mwema wa taifa letu.

Kwamba, badala ya kusubiri Septemba ifike na kisha kutunishiana misuli, tunadhani kuwa upo muhimu wa pande zote kuketi chini na kutanguliza busara katika kutafuta namna bora ya kuepusha shari ya aina yoyote ile.

Na katika kutekeleza hilo, tafsiri za sheria pia zipewe nafasi yake, tena katika namna isiyotanguliza maslahi binafsi bali ya umma.

Hakika, haikubaliki hata kidogo kuona kuwa watu wakiumizwa kwa sababu tu ya kuwapo kwa malumbani haya.

Haitapendeza pia kuona kuwa baadhi ya watu wakikamatwa na kuwekwa ndani kwa sababu tu ya kuwapo kwa sintofahamu iliyopo.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kiuchumi, Tanzania bado ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani. Hadi sasa, ikiwa ni zaidi ya miaka 50 ya uhuru, Tanzania bado inakabiliwa na maadui wakubwa watatu -- ambao ni ujinga, umasikini na maradhi.

Hadi sasa, maeneo mengi nchini bado yanakabiliwa na matatizo yanayohusiana moja kwa moja na athari za maadui hao watatu. Zipo shule nyingi za msingi ambazo wanafunzi wake huketi sakafuni kwa sababu ya kukosekana kwa madawati; kuna uhaba mkubwa wa nyumba za walimu na maabara kwa ajili ya masomo ya

Sayansi; kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa afya wakiwamo madaktari na wauguzi; bado kuna idadi ndogo ya zahanati na vituo vya afya na pia kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama. Kama hiyo haitoshi, hadi sasa kuna kaya huwa hazina uhakika wa walau mlo mmoja kwa siku. Kwingineko njaa bado ingali ikitamalaki.

Kwa ujumla, yapo matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii yanayopaswa kushughulikiwa kwa nguvu ya pamoja badala ya kuwapo kwa mfarakano wa aina yoyote ile.

Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa ipo sababu ya kutangulizwa busara katika kumaliza mvutano unaojitokeza sasa baina ya vyombo vya dola na vyama vya siasa vya upinzani, hususani Chadema. Tahadhari ni bora kuliko kinyume chake.