Lakini ajenda kubwa ambayo maamuzi yake yanasubiliwa kwa shauku kubwa na wadau mbalimbali wa soka nchini wakiwemo mashabiki wa timu hiyo,ni mustakabali wa aina ya mfumo wa kuiendesha timu hiyo.
Uongozi wa Simba uliunda Kamati maalum kwa ajili ya kufanya tathimini na na kukusanya maoni jinsi ya kuiendesha timu hiyo huku ikilenga timu kubadilika kuingia kwenye mfumo wa Kampuni hili kutoa fulsa kwa wanachama wenye uwezo kuwekaza kwenye timu hiyo kwa kununua hisa.
Kamati hiyo leo inakabidhi ripoti yake kwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo chini ya Rais wake Evance Aveva ambaye ataiwasilisha kwa wanachama wa klabu hiyo kesho kwa ajili ya kuijadili.
Nipashe inafahamu mkutano huo utakuwa na wanachama wenye mtazamo na hisia tofautofauti ambao watakuwa na mvutano upande mmoja na mwingine huku kila upande ukivutia kwake.
Tunaamini kila upande utakuwa na sababu kwa nini wanasimama upande huo, jambo kubwa ambalo wanachama na viongozi wa timu hiyo wanapaswa kuweka mbele ni kuwa chochote kitakachojadiliwa na kuamuliwa ni kwa manufaa ya klabu hiyo.
Hakuna mwanachama au kiongozi anayependa kuona Simba ikishindwa kupata mafanikio, kila wazo litakalotolewa ni kwa lengo la kuiinua Simba sasa ni vyema busara ikatumika katika kupata muafaka kwa kila jambo watakalojadiliana kesho.
Wanachama wapewe fulsa ya kutoa maoni yao juu ya suala la kuamua timu hiyo kujiendesha kwa mfumo wa kampuni na kusiwe na suala la ushabiki mbele badala yake maendeleo na manufaa ya klabu yaekwe mbele zaidi.
Kama muafaka utakuwa ni kuendelea na mfumo wa sasa au mfumo mpya basi suala hilo likubaliwe na wanachama wa klabu hiyo na viongozi waridhie pasipokuwa na utashi binafsi kuwekwa mbele.
Nguvu na maamuzi ya pamoja ndicho kitu cha msingi ambacho Nipashe inategemea kukiona kwenye mkutano huo ambao utafanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay.
Viongozi wa Simba waelewe na kufahamu mkutano huo ndio wenye maamuzi ya mwisho kwa jambo lolote la kikatiba ambalo linaihusu timu hivyo wanapaswa kuheshimu maamuzi yatakayochukuliwa na wanachama hao.
Lakini pia wanachama watumie busara na pia shauku ya maendeleo ya klabu hiyo iwaongoze katika kufanya maamuzi kwenye mjadala huo ambao Nipashe inaamini utavuta hisia za wanachama.
Lakini pia suala la kufanya vibaya kwenye ligi kwa kipindi cha miaka mine mfululizo iwe chachu ya kufanya maamuzi sahihi ili kuingia katika wimbi la mafanikio na kurejesha heshima ya klabu hiyo kongwe nchini na Afrika kwa ujumla.
Nipashe inawatakia kila heri wanachama, viongozi wa Simba katika mkutano huu muhimu kwa mustakabali wa klabu hiyo.










