Yanga, Simba tunatarajia mchezo wa kiwango bora

28May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Simba tunatarajia mchezo wa kiwango bora

MIAMBA ya soka Tanzania, Yanga na Simba leo Jumamosi inashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza kuwania kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam maarufu kama FA.

Mchezo huo wa hatua ya nusu fainali unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kuhitaji kutinga fainali na hatimaye kulitwaa taji hilo.

Timu hizo zinaingia kwenye mchezo huo, wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la msimu huu.

Nipashe tukiwa kama wadau wakuu wa michezo hapa Tanzania, tunaamini mchezo huo utakuwa wa kiwango bora na cha juu kwa timu zote mbili hasa ikizingatiwa kwamba, hizo ndio kama baba na mama wa soka la hapa nchini.

Tunaamini timu zote zimejipanga vizuri kuelekea mchezo huo na kwa namna yoyote utakuwa na burudani nzuri na kutosha kwa mashabiki wao.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwategemea zaidi wachezaji wake kama kipa Djigui Diarra safu yake ya ulinzi chini ya nahodha Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, Djuma Shabani na Kibwana Shomari.

Wakati katika eneo la kiungo atakuwepo Khalid Aucho, Salum Abubakary 'Sure Boy' na Feisal Salum 'Fei Toto' huku Fiston Mayele akitarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji sambamba na Jesus Moloko.

Kwa upande wa Simba kuna shaka ya uwepo wa golikipa wao namba moja, Aishi Manula na huenda ikampa nafasi Beno Kakolanya ambaye ni kipa wa zamani wa Yanga, kuanza au kuingia kwenye mchezo huo huku Hennock Inonga na Joash Onyango wakitarajiwa kuanza kwenye beki ya kati.

Sehemu ya kiungo ya Simba huenda ikaanza na Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute na viungo wa pembeni akawatumia Pape Sakho, Larry Bwalya na kwenye eneo la ushambuliaji akaanza na nahodha John Bocco na Kibu Denis.

Kutokana na uimara wa vikosi vyote vya timu hizo, sisi tuna imani kubwa utakuwa mchezo wa kutumia mbinu, akili na ubunifu wa hali ya juu katika kuhakikisha kwamba, mmoja anaibuka na ushindi.

Uzuri wa mchezo wa leo ni kwamba, kwa namna yoyote lazima mshindi apatikane, kwani hapa inatafutwa timu itakayotinga fainali.

Hivyo, tunaamini kabisa kwa jinsi makocha na mabenchi yao ya ufundi walivyojipanga, tunatarajia kutakuwa na burudani ya ina yake wakati dakika 90 au muda wa ziada au penalti zitakapomalizika.

Hatutarajii lawama za namna yoyote kwa kuwanyoshea kidole waamuzi au maofisa mara baada ya mchezo huo, kwani kila timu ilikuwa na nafasi ya kujifua kabla ya kuingia kwenye mchezo huo na maana yake ni kwamba walikuwa wamejiandaa vya kutosha.

Mshindi wa mchezo wa leo atakutana kwenye fainali na mshindi kati ya Azam FC na Coastal Union ambao wao watakipiga kesho Jumapili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid kule jijini Arusha.

Hivyo basi, tunawatakia Yanga na Simba kila la heri katika mchezo huo ambao tunaamini utakuwa bora na wenye ushindani ambao matokeo yake yataamuliwa uwanjani kutokana na kiwango bora cha timu itakachokionesha.