Kupitia tangazo la bodi hiyo lililochapishwa kwenye vyombo vya habari, wadaiwa wanakabiliwa na adhabu hizo ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha mfuko huo mwaka 2004.
HESLB inasema wakopaji ambao hawarejeshi mikopo yao watakabiliwa na hatua ya kisheria, na majina yao yatapelekwa kwa taasisi ya kuorodhesha wadaiwa sugu, hivyo watakuwa wamejinyima fursa ya kukopeshwa na taasisi zote za kifedha nchini, yakiwamo mabenki na Saccos.
Hatua nyingine dhidi ya wadaiwa kwa mujibu wa sheria, ni kupeleka taarifa zao za kina kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, Idara ya Uhamiaji na kwa balozi zote ili wanyimwe ruhusa ya kusafiri nje ya nchi. Kadhalika, watanyimwa udhamini wa Serikali au kudahiliwa kwa ajili ya kusomea shahada za uzamivu kwenye chuo chochote ndani na nje ya nchi.
Wadaiwa hao wanakabiliwa pia kuadhibiwa kwa kukamuliwa fedha zaidi ya kiwango cha deni la sasa, kwani watakuwa wakilipa riba ya kila mwezi ya asilimia tano ya deni la mkopo kwa kila mwaka, mbali na riba ya asilimia tano inayotozwa sasa.
Vilevile watabebeshwa gharama za kuwatafuta HESLB baada ya kukamatwa na wakala watakaopewa kazi ya kuwafuatilia.
Bodi imechukua hatua hiyo baada ya Serikali kutoa kauli za miaka mingi za kuwataka watu wote walionufaika na mkopo kulipa, bila wahusika kujitokeza.
Watu wengi walikuwa wanaziona kauli za Serikali kama utani, kwani walidhani izingeweza kuwapata waliokopa na kunufaika pengine kwa kudhani kuwa hapakuwapo na kumbukumbu.
Tunaunga mkono jitihada zinazofanywa na
HESLB kudai fedha hizo zirejeshwe ili kupanua wigo wa kukopesha idadi kubwa ya Watanzania wanaozihitaji kwa ajili ya kusoma.
Kutokana na fedha hizo kutorejeshwa kwa wakati, watu wengi waliathirika kutokana na kuomba bila mafanikio na wengine waliomba na kupewa kiwango kidogo ambacho hakikukidhi mahitaji yao.
Usumbufu uliotokana na hali hiyo ikiwamo migomo na maandamano ya wanafunzi katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu unapaswa kuwa fundisho; kwamba sasa HESLB iweke taratibu nzuri na endelevu zitakazowabana wakopaji wote kulipa fedha hizo kwa wakati mwafaka.
Watanzania tunapaswa kujenga utamaduni mpya wa kukopa fedha na kuzirejesha, badala ya kudhani kuwa mkopo ni zawadi. Wenzetu katika nchi zilizostarabika, wananchi wake wana utamaduni wa kulipa mikopo na kuirejesha, kwa kuwa kukwepa kirejesha ni kupoteza uaminifu na mtu wa aina hiyo hawezi kukopesheka tena kwa maisha yake yote.
Bila shaka wakopaji ambao majina yao yametolewa aktika vyombo vya habari watajitokeza kulipa fedha hizo ili kuepukana na usumbufu ambao wataupata kama hatua zilizotangazwa zitaanza kutekelezwa dhidi yao.
Tunasisitiza tena kwamba wanafunzi wote waliokwishakopa na watakaoendelea kukopa fedha za kusoma kutoka HESLB wajenge na kuendeleza utamaduni wa kurejesha fedha hizo ili ziwasaidie wahitaji wengine.
Bila kurejesha fedha hizo tusijidanganye kwamba sisi kama taifa tutaweza kuboresha kiwango cha elimu ambacho tunalalamika kila uchao kuwa kimeporomoka.










