Biashara kwenye mazingira safi ni heri, Mabibo sokoni muamke

29Apr 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Biashara kwenye mazingira safi ni heri, Mabibo sokoni muamke

SUALA la usafi lina maana kubwa na inatakiwa jamii ielewe nini mantiki yake kwa undani na uelewa wa kina.

Usafi unapofanyika ipasavyo, ni wazi jamii inakuwa salama na kinyume chake, jamii hiyo inaweza kupata madhara, kwani inajulikana vyema aina ya shida inayoiangukia jamii husika.

Suala la usafi wa mazingira, linalenga katika mbinu za kuzuia kupanuka maradhi hasa kwa kupitia majitaka na uchafu kama vile kinyesi, jamii inabaki na maji aina zote safi na salama.

Maji yanapokuwa machafu na yanapatikana katika mazingira yetu, ni wazi bakteria zinazotokana na mazingira machafu yenye taka yanatuingiza katika maeneo hatarishi na kutusababishia madhara pasipo kutarajia .

Pia, uchafu wa kinyesi cha binadamu, hata cha wanyama, taka ngumu, maji machafu, taka za viwandani, shambani, nazo si salama hata kidogo kwa uhai wake binadamu.

Hapo ndipo inapojenga hoja ya haja ya udhibiti wa maji taka na kinyesi, kwa sababu kuna viini vinavyosabisha magonjwa ya binadamu katika vitu hivyo na kusababisha maambukizo kutoka kwa mtu mmoja kumuendea mwingine.

Usafi ukiwa ni njia ya kuzuia maradhi, namna ya kuufanikisha huwa ni kwa kuengua hatari yake ambayo ni uchafu. Njia inayotumika ni kwa ufumbuzi halisi, kama vile utiririshaji majitaka na tiba ya maji machafu kwa dawa.

Teknolojia rahisi kama ya kutumia vyoo, au matendo ya usafi binafsi, ikiwamo kuosha mikono kwa sabuni inaweeza kuleta majibu sahihi.

Usafi wa mazingira kama unavyoelezwa kwa ujumla wake na Shirika la Afya Duniani (WHO), unahusu utoaji vifaa na huduma ya usalama wa mkojo na kinyesi cha binadamu, kunusuru athari zake.

Mapungufu katika matendo ya usafi mbalimbali na wa mazingira, ndiyo sababu kuu ya maradhi kuibuka kwa wingi duniani kote.

Hapo inazaa hoja kwamba uboreshaji mazingira una manufaa makubwa kwa afya ya wote katika kaya na jamii kwa ujumla.

Pia, kunahusika mbinu ya kudumisha ratiba ya usafi, kwa matendo kama ya ukusanyaji taka ngumu na maji machafu.

Sasa kwa kutumia nadharia hiyo, nawarejea hawa wafanyabiashara walio nje na ndani ya Soko la Mabibo maarufu Soko la Ndizi, jijini Dar es Salaam, namna wanavyopanga bidhaa zao chini, katika mazingira machafu hata kwa kuangalia yanakiuka wazi kanuni za usafi.

Kuna baadhi yao wameweka bidhaa wanazouza kwenye matope, huku wengine nao wakiuza katika maeneo jirani kabisa na maji machafu, ambayo yanajulikana vyema katika afya ndio wakala wa maradhi.

Sasa kama hao wafanyabiashara wanashindwa kufanya biashara katika maeneo rafiki, wajue bayana wanafanya makosa kwa watumiaji bidhaa zao. Wanatakiwa kujali afya za walaji na sio tu kuwaza kupokea tu kutoka wa wanunuzi.

Hivi sasa mvua zinaendelea katika sehemu nyingi za nchi, huu uchafu umechukua nafasi kubwa sehemu hiyo ya biashara.

Hakuna ubishi kwamba kuna kila aina ya haja watu hao watengenezewe miundombinu sahihi, ili waweze kufanya biashara katika maeneo yaliyo na usafi.