Pia, CAG Charles Kichere alibainisha takwimu hizo katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 aliyoikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 30, mwaka huu na kuwasilishwa bungeni jijini Dodoma Aprili 12, mwaka huu.
Alisema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia jumla ya hifadhi 22 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 104,170, kati yake ni Hifadhi za Taifa Mikumi, Serengeti, Tarangire na Ziwa Manyara.
CAG alisema Hifadhi ya Taifa ya Mikumi inapitiwa na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 45 huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikipitiwa na barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 12 ikitokea Mbalageti hadi Mto Robana.
Kwa mujibu wa CAG, mwaka 2020/21, wanyama 535 waliuawa kwenye ajali za barabarani katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kulinganishwa na wanyama 106 katika mwaka 2019/20.
Idadi hiyo ni ongezeko la wanyama 429, sawa na asilimia 405, huku wanyama 50 waliuawa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti; wanyama 18 waliuawa Hifadhi ya Taifa Tarangire; na wanyama 11 waliuawa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara.
Kwa maoni yake, ikiwa hatua madhubuti za usalama hazitachukuliwa kuzuia uzembe wa madereva ndani ya barabara zinazopita kwenye hifadhi za taifa, kuna uwezekano wa wanyamapori kuendelea kuuawa kwa ajali za barabarani.
Alipendekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kupitia upya taratibu za uendeshaji salama wa magari ndani ya hifadhi za taifa nchini ili kudhibiti ajali zinazoua wanyamapori hifadhini.
Idadi ya wanyamapori waliouawa ni hasara kwa taifa kwa kuwa uwapo wao unawezesha taifa kupata fedha za kigeni, kupitia watalii wanaokuja kwa ajili ya kuwaona.
Ni lazima wanyama watembee kutoka eneo moja kwenda jingine ndiyo maana kuna maeneo ya mtawanyiko na mapito ya wanyama maarufu kama shoroba.
Wanyamapori hutembea kutoka eneo moja hadi jingine kutafuta mahitaji muhimu kama udongo wenye madini, majani na maji, wengine kama nyumbu huwa na maeneo maalumu ya kuzalia ambayo husaidia ndama wao kupata chakula.
Ili Hifadhi za Taifa na maeneo yaliyohifadhiwa yawepo ni lazima kuwe na mapito ya wanyama ambayo yanapaswa kulindwa vinginevyo watabaki kwenye kisiwa na kuna uwezekano mkubwa aina ya wanyamapori kupotea au kuzaliana wao kwa wao ambao ni ndugu hali inayosababisha ugonjwa ukiingia ni rahisi kufa kwa pamoja au kupata aina inayodumaa kwa kuwa hakuna mchanganyiko kwenye uzazi.
Ili wanyamapori waendelee kuwapo ni lazima kutunza ikolojia ya maeneo husika inayowalinda, kuzaliana na kukua bila tatizo ili mtalii anapofunga safari kutoka Ulaya, Marekani na China kwa ajili ya kuona simba, tembo, faru, chui, twiga na wengine awaone bila kikwazo.
Katika maeneo yote yaliyopitiwa na barabara kuna alama za barabarani zinazoonyesha eneo husika linapitiwa na wanyamapori, dereva wanapaswa kuendesha kwa uangalifu mkubwa, lakini bado wameendesha kwa kasi hususan nyakati za usiku.
Barabara ya Mikumi-Morogoro kuna mabango yanayoonyesha gharama za kila mnyama atakayegongwa na kuwataka madereva kuendesha kwa kuzingatia vibao, lakini hawafanyi hivyo matokeo wanyama wanapotea kama CAG alivyobainisha.
Ni lazima kuchukua hatua madhubuti kama ni kuongeza matuta, kuweka kamera ya kutambua magari yanayogonga wanyama na kuchukua hatua au kuondoa barabara hizo.
Bila kuweka utaratibu wa kulinda raslimali hii, kusikiliza na kutekeleza ushauri wa CAG, huku kukiwa na ongezeko la watu, ni wazi itafika wakati maeneo yaliyohifadhiwa yatabaki machache hali itakayopunguza watalii










