Ni Ligi bora ya Simba na Yanga tu Bongo?

16Apr 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni Ligi bora ya Simba na Yanga tu Bongo?

NIMEKUWA nikisoma sehemu mbalimbali kuwa Ligi ya Tanzania Bara ni ya nane kwa ubora Afrika. Inawezekana ikawa ni kweli, lakini kwangu mimi ambaye nimeshawahi kuiona ligi ya Tanzania miaka ya 1980 hadi 1990, bado inanipa shida kuamini moja kwa moja kitu hicho.

Kwangu mimi ninachoona kuwa kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara ni ligi inayokua kati ya ligi mbalimbali za Afrika na imekuwa maarufu kutokana na kuonyeshwa kwenye televisheni ambapo imekuwa ikionekana maeneo makubwa ya Afrika Mashariki na Kati.

Kuwepo pia kwa baadhi ya wachezaji kutoka nje ya nchi, hasa kutoka kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kunawafanya hata mashabiki wa soka wa ukanda huo kuifuatilia sana ligi ya Tanzania, pia ushabiki uliokuwepo, na hamasa unaifanya ligi kuchangamka zaidi, tofauti na ligi za nchi nyingine za karibu kwa sasa kama vile Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

Yaani tunaweza kusema kuwa Ligi Tanzania Bara ni moja kati ya ligi pendwa Afrika na hata ikisemekana inashika nafasi ya nne, achilia mbali nane, hapo naweza kukubali kabisa.

Kwenye ubora inanipa shaka. Bado kama Watanzania tuna safari ndefu ninavyoona ili ligi iwe bora.

Naweza kuthubutu kusema zamani Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ambayo kwa sasa ndiyo Ligi Kuu ilikuwa bora zaidi ya sasa.

Haiwezekani Ligi Kuu inaanza, timu za Simba na Yanga tu ndizo zinazoonekana kuusaka ubingwa na si zingine. Zilizobaki zinausaka ubingwa kwa maneno tu, lakini huwezi kuona vitendo vyovyote uwanjani vinavyoonyesha ni kweli ni timu zinazopigania ubingwa.

Hata Azam FC, timu ambayo kwa miaka ya karibuni imeonekana kujipambanua kuusaka ubingwa, lakini huoni dalili hizo.
Timu inayosaka ubingwa haiwezi kushinda mechi leo, kesho inafungwa, kesho kutwa inatoka sare na timu ndogo tu, huku zingine zikishinda mfululizo.

Nikisema hivi sina maana kuwa timu zingine nazo ziwe mabingwa, la hasha. Hata miaka ya nyuma, Simba na Yanga zimekuwa zikipokezana ubingwa wa Tanzania Bara na Muungano, ingawa ulikuwa unaingiliwa na timu zingine katikati kama Coastal Union, Pamba, Tukuyu Stars, Prisons, Mseto, Cosmopolitan, Pan African, lakini kulikuwa na ushindani mkubwa tofauti na sasa.

Ukiangalia kwa sasa Simba na Yanga zinachukua ubingwa kirahisi zaidi. Zamani wakati mwingine zililazimika kusubiri hadi mechi za mwisho ndiyo ziamue.

Sababu zimekuwa ni nyingi, ikiwemo hata waamuzi wamekuwa wakizibeba mno timu hizo kubwa kwa sasa tofauti na zamani. Wakati ule hakuna TV, lakini waamuzi walikuwa makini, tofauti sasa, waamuzi wamekuwa wakivurunda huku wakimulikwa na televisheni, lakini wapi.

Ukitaka kujua hilo, angalia timu hizi za sasa zikicheza na Simba au Yanga, zinakaa nyuma, zinahitaji zaidi sare kuliko ushindi, zikibahatika kupata bao moja, basi ni hilo hilo.

Ndiyo maana zikipata sare , wachezaji wao wanashangilia, unaweza kudhani zimetwaa ubingwa. Timu inayosaka ubingwa haiwezi kushangilia sare dhidi ya Simba au Yanga. Jiulize Simba au Yanga, kufungwa mabao 2-0, 3-0, 3-1, ilikuwa lini?

Miaka ya nyuma, Simba au Yanga kupigwa idadi hiyo ya mabao ilikuwa ni kitu cha kawaida tu, tena ikiwa na wachezaji bora kabisa wanaochezea mpaka timu za taifa, Taifa Stars.

Mfano tu, Simba iliwahi kuchapwa mabao 4-2 na Reli ya Morogoro, Yanga ikabamizwa mabao 3-0 dhidi ya Pamba, tena kwenye Uwanja wa Taifa. Zinafungwa na zinachezewa mpira.

Na haikuwa mara ya kwanza mbili au tatu kufungwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu. Hii ndiyo unaweza kusema ligi bora. Kwa hizi timu zinazoshangilia sare, zikicheza kutaka kusalia Ligi Kuu, halafu tuseme ni ligi bora. Inanipa ukakasi.