Mastraika Bongo bebeni alichokifanya Mane

18Apr 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mastraika Bongo bebeni alichokifanya Mane

ILIKUWA ni dakika ya 18, kipa wa Manchester City, Zack Steffen alipokuwa na mpira mguuni, akiwa hana hili wala lile. Alidhani wachezaji wote 21 waliokuwa mbele yake wanamsubiri apige mpira mbele.

Macho yake hayakumuona Sadio Mane aliyekuwa anamnyemelea, na baada ya kuwa na uhakika kwamba akili ya kipa huyo ilikuwa kwa atakayempigia kuliko mpira wenyewe aliongeza kasi.

Wakati kipa akishtukia Mane yuko karibu, akahamaki na kabla ya kuwa na akili ya kutaka kumpiga chenga, aliserereka mguu wake ukifuata mpira na alipogusa, ukambabatiza mwenyewe na kutinga wavuni, likiwa ni bao la pili kwa Liverpool.

Ni bao ambalo halikutegemewa. Na wala si bao ambalo limetengenezwa au kocha amefundisha mazoezini. Pamoja na kwamba alifunga lingine, lakini hilo lilichangia Liverpool kushinda 3-2 kwenye nusu fainali Kombe la FA.

Ni utayari, kujituma na kasi ya straika, ambaye muda wote anatakiwa awe na mbinu ya kufunga mabao kwa njia yoyote ile. Nimelielezea bao hilo kwa sababu nataka kutoa somo kwa mastraika wetu Tanzania. Kwa miaka ya hivi karibuni huwezi kuliona bao kama lile, labda kwa mtu mmoja tu, Meddie Kagere.

Yeye pekee ndiye straika anayeweza kumfuata kipa kwa namna ambayo inawafanya wakati mwingine wafanye makosa.
Rejea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Mbabane Swallows ya Eswatini Novemba 28, 2018, iliposhinda mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Moja ya bao lililofungwa ni kwamba, kipa wa wageni alipokea mpira hakujua kama atafuatwa na mchezaji yeyote.

Kagere alipomfuata na ghafla alipotambua hilo, akashtuka. Chochote alichotaka kukifanya hakikuwa, kwani aliteleza na kumpa nafasi straika huyo kuufikia mpira kabla ya kuujaza wavuni.

Kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, iliyochezwa Aprili 3, mwaka huu kati ya Simba na US Gendarmerie, Kagere alisababisha kipa wa timu hiyo kujichanganya na kujifunga mwenyewe kutokana na mbio alizokuwa akija nazo kumfuata.

Ukiacha straika huyo, sijawahi kuona straika yeyote Mtanzania, au mgeni anayecheza kwenye ardhi ya Tanzania mwenye uthubutu huo. Si kama hawafuati, la hasha. Wengi wanawafuata makipa kivivu au ili mradi tu na kupigwa chenga kirahisi.

Kagere humkimbiza kipa kwa kasi na nguvu. Si mara zote anafanikiwa, lakini inavyoonekana kama angeweza kupata wenzake ambao wanaweza kufanya kazi kama yeye, angekuwa anafanikiwa sana.

Kwa sasa umri umeenda, kama angekuwa straika kijana na tabia ile aliyonayo, basi angekuwa hatari mno kwa makipa.

Wala isidhaniwe kuwa ni Mane tu kwa sababu anacheza Ulaya, zamani Tanzania kulikuwa na mastraika wenye tabia hizo na walifunga sana mabao ya aina ile, wakiongozwa na Victor Mkanwa, Abdallah Buruani, Adam Sabu, na wengineo.

Hawa walikuwa ni hatari kwa mipira ambayo kipa anakuwa nayo miguuni, au amerudishiwa. Hawapigwi chenga kirahisi, mabao yao mengi yalikuwa ya aina hiyo.

Kwa alichokifanya Mane Ijumaa nchini Uingereza, ni funzo kwa mastraika wetu wa sasa hasa wa Kitanzania kuwa ili ufunge bao inabidi ujitume na kupambana.

Mastraika wa Kibongo wanataka kufunga mabao rahisi, ya kutafuniwa, na si ya kujituma kwa kupambana kama alivyofanya Mane.

Ukiangalia si wengi wanaopiga mashuti makali nje ya eneo la hatari, anaweza kuingia ndani ya 18 badala ya kutafuta kila njia apate nafasi ya kupiga shuti, anageuka tena nyuma kumtafuta mtu mwingine.

Ni kweli kuna makipa nchini ni wazuri wakiwa na mpira miguuni, lakini wanaweza kufanya makosa muda wowote. Na hiyo ni kama watakutana na mastraika jasiri, wenye uchu wa kutaka kufunga mabao, wenye uthubutu na kujituma.

Kama Mane ameweza kwenye uwanja mzuri wa Wembley, je kama mastraika wa Bongo wanafanya kwenye viwanja hivi vya kwetu ambavyo haviko vizuri. Wanachotakiwa ni kuacha uvivu na kufanya mazoezi sana, ili wawe na pumzi na fiziki ya kutosha.