Agizo hilo limetolewa ikiwa ni takribani wiki moja tangu alipoweka bayana kwamba taasisi hiyo inapaswa kusukwa upya, ikiwa ni pamoja na kufumua uongozi mzima na kuweka watu wapya.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo pamoja na mambo mengine, ilionyesha upungufu katika utendaji kwenye taasisi hiyo.
Kila kikao cha bunge halikosekani swali kwenda Wizara ya Afya, kutaka kujua lini serikali itahakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana, huku wakitoa mifano ya wananchi kutakiwa kununua dawa kwenye maduka binafsi, kwa kuwa hakuna dawa kwenye zahanati, kituo cha afya na hospitali.
Wapo wanaokwenda kutibiwa wanaandikiwa dawa, lakini hawajui pa kuzipata kwa kuwa wanatakiwa kutembea umbali mrefu kuzitafuta kwa gharama kubwa, na mbaya zaidi zinapatikana kwenye maduka binafsi kuliko serikalini.
Katika kukabili hali hiyo, Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, aliagiza MSD kuwa na maduka yake karibu na hospitali ili wananchi wapate huduma kirahisi kwa zile ambazo haziko kwenye orodha ya kugharamiwa na serikali.
Ni muhimu kufanya uchunguzi wa mifumo ili kubaini wapi dawa zinapotelea, kwa kuwa siyo jambo la karibuni bali limeongelewa kwa miaka mingi linahitaji kufanyiwa kazi kubwa.
Pia, kuna wakati Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliagiza maduka yaliyopo umbali wa mita 500 kutoka kwenye hospitali kuondolewa, kwa kuwa kuna uwezekano wa kutoroshwa dawa kutoka hospitalini.
Licha ya serikali kueleza kuwa maboresho makubwa yamefanyika kuhakikisha hakuna upotevu wa dawa,lakini bado hazifiki kwa watumiaji kama inavyotakiwa na imekuwa kawaida kuandikiwa dawa za kwenda kununua.
Ni muhimu serikali ikafanya uchunguzi wa kina kwa kuwa yapo malalamiko mengi ya kukosekana kwa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali, kwa kuwa badala ya wananchi kunufaika wachache ni wanufaikaji wakubwa jambo ambalo ni hatari sana.
Ni kawaida kukuta majengo mazuri na wakati mwingine yana hadi vifaa tiba vizuri lakini mgonjwa anaambiwa hakuna dawa, anatakiwa kwenda kununua kwenye maduka binafsi ambayo mengi yamejengwa karibu na maeneo ya tiba.
Kwa sasa maduka ya dawa baridi na dawa muhimu yanamea kwa wingi ambayo yanakuwa na kila aina ya dawa, lakini kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma hazipatikani.
Kama ambavyo CAG amependekeza kufumuliwa kwa taasisi hiyo na sasa Rais ameona umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mfumo wa dawa tangu inatoka MSD, basi ni muhimu sana ili wananchi waridhike kuwa asilimia 80 ya dawa zinazoelezwa kusambazwa zimewafikia.
Hotuba ya wizara hiyo mwaka 2021/22 ilisema serikali kupitia MSD hununua, hutunza na kusambaza aina 2,545 za dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Kati ya hizo, dawa aina 1,865 ni dawa zilizo katika utaratibu wa Miradi Msonge na aina ya dawa 680 ni dawa muhimu.
Aidha, dawa za aina 312 ndizo zimeainishwa kuwa ni dawa muhimu na za kipaumbele cha wizara kwa lengo la kuhakikisha
kuwa zinapatikana nyakati zote katika MSD.
Ilisema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, hali ya upatikanaji wa aina hizo 312 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ilifika asilimia 75.6 na katika maghala ya MSD ni asilimia 21 ikilinganishwa na hali ya upatikanaji
wa dawa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2019/20, ulikuwa ni asilimia 80 katika vituo vya kutolea huduma na asilimia 56 kwa MSD.










