Ajali hizo ni mfululizo wa zile zilizotokea tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2022, hali ambayo nadhani kwamba sasa kuna haja ya kuwapo elimu ya kutosha kwa madereva na watumiaji barabara na abiria kwa ujumla.
Inasikitisha kuona ajali hizo zikiendelea kuleta simanzi kwa Watanzania kutokana na ukweli kwamba, zinaondoa nguvu kazi ambayo ni tegemeo kwa familia na kwa maendeleo ya nchi.
Ingawa siku za nyuma ni kama zilianza kupungua kwa kiwango kikubwa, lakini ghafla zimeibuka kwa kasi ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Askari wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, wamekuwa wakifanya kazi nzuri kukabiliana na madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani, hata kuwapa adhabu waogope na kufanya kazi yao kwa umakini.
Hata hivyo, inaonekana wapo baadhi ya madereva ambao bado wamekuwa wagumu kuzingatia sheria hizo na badala yake kuendelea kusababisha ajali zinazogharimu maisha ya watu wasio na hatia.
Ninaamini, bado madereva wengi wanaendelea kufanya makosa wawapo barabarani, hali inayoonyesha kuwa ipo haja ya kuwekeza nguvu katika utoaji wa elimu, ili kuwasaidia wabadilike.
Kwanini? Kitendo cha Jeshi la Polisi kukusanya faini ya Sh. bilioni 50.1 kama faini kutoka kwa madereva wanaofanya makosa ndani ya kipindi cha miezi 10, ni wazi elimu zaidi inahitajika kuliko faini.
Hiyo ni taarifa ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro aliyoitoa Mei mwaka jana, kwenye uzinduzi wa kiwanda cha ushonaji katika bohari kuu ya jeshi hilo kilichoko eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Usalama Barabarani, kinafanya kazi nzuri, lakini pamoja na hayo, ninadhani ukusanyaji wa fedha nyingi za faini uwe kiashiria kuwa hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa ili kupunguza makosa yanayoweza kusababisha ajali.
Makusanyo ya fedha za faini zitokanazo na makosa mbalimbali ya barabarani yanapopungua, ni wazi kwamba elimu imewaingia vizuri, lakini yanapokuwa makubwa, hiyo inatosha kuelewa kuwa elimu zaidi inahitajika.
Kukusanya fedha nyingi za faini za makosa mbalimbali ni wazi kwamba usalama barabarani nao ni mdogo na inawezekana baadhi ya vyombo vya moto vilivyoko barabarani havistahili kuwapo.
Inawezekana madereva wa vyombo hivyo, hawajui sheria za barabarani, hivyo kwa mantiki hiyo, suala la utoaji wa elimu ya kutosha kwa watu hao ni muhimu kunusuru maisha yao na abiria.
Hivyo, ukusanyaji fedha nyingi zinazotokana na faini za makosa mbalimbali ninaliona kama ishara ya kuwapo tatizo.
Pia ni wazi fedha nyingi za faini zinapokusanywa kutokana na makosa mbalimbali ni wazi usalama barabarani nao ni mdogo, ina maana kuna uwezekano baadhi ya vyombo vya moto havistahili kuwapo barabarani.
Imekuwa kawaida kusikia ajali imetokea huku chanzo chake kikitajwa kuwa ni uzembe wa madereva na kama ndivyo, basi badala ya kukazania kuwatoza faini, mkazo zaidi uwe ni kuwaelimisha ili waone umuhimu wa kubadilika.
Nieleweke kuwa sipingi faini, bali waendelee kutozwa, lakini elimu inaweza kuwabadilishia hatua, kwani nguvu kubwa ikiwa kwenye faini wanaweza kuendelea kusababisha ajali wakijua watalipa faini na kisha madereva wanaendelea na tabia yao.
Kwa mfano, wapo baadhi ya madereva ambao hutumia kilevi kisha wakaendesha vyombo vya moto hali ambayo ni hatari kwao na hata kwa abiria, hivyo ingekuwa ni vyema wakaelimishwa kikamilifu.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







