CAG hukagua fedha za umma ambazo serikali inawajibika kuzisimamia ipasavyo ili zitumike kwa manufaa ya wananchi wote, badala ya wajanja wachache kujipatia kwa manufaa yao binafsi.
Kila mwaka CAG huonyesha mianya iliyopo kwenye mashirika,taasisi, serikali kuu na serikali za mitaa pamoja na hutoa mapendekezo ya nini kifanyike, lakini hali imeendelea kuwa ile ile na wakati mwingine mbaya zaidi kwa baadhi ya maeneo,jambo ambalo linaonyesha kuna kazi kubwa ya kufanya.
Baadhi ya mamlaka zimeshindwa kutengeneza taarifa zake inavyotakiwa au kukosekana viambatanisho na nyaraka muhimu za matumizi ya fedha ya Watanzania.
Kila Mtanzania analipa kodi kwa namna yake, kwamba kuna mwenye biashara, kampuni,mfanyakazi au mjasiriamali ambao viwango vya kodi hutofautiana kutoka mmoja kwenda mwingine, lakini unaponunua bidhaa lazima utalipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT); maana yake kila mmoja anawajibika kulipa kodi na ana haki ya kunufaika na kodi hiyo kupitia huduma bora za kijamii.
Katika ukaguzi huo, kati ya taasisi za umma 999 zilizokaguliwa mwaka 2020/21, zipo zilizopata hati zenye shaka na zingine CAG alishindwa kutoa maoni.
Alimweleza Rais Samia kuwa walikagua mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSSSF wakabaini mafao ya pensheni yanazidi mapato yatokanayo na michango ya wanachama.
Aidha,vyama vya siasa vilivyokaguliwa vilivyopata hati zenye shaka ni CUF ,UDP, SAU huku hati chafu ni ADC,CHAUMMA,UMD,TLP na Chama Cha Demokrasia Makini huku akishindwa kutoa maoni kwenye hesabu za AFP.
Kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, walibaini Sh.bil 47.07 zilizokopeshwa kwa wanawake,vijana na wenye ulemavu hazikurejeshwa.
Hili ni jambo la kusikitisha kwa kuwa fedha hizi kama hazikutumika basi zilipaswa kurejeshwa ili wakopeshwe wengine na kuona thamani ya fedha kwa kuangalia mabadiliko kwa waliokopeshwa, lakini kwa kutorejeshwa inaonyesha kuna tatizo mahali, hivyo lazima lishughulikiwe.
Mathalani,wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge, baadhi ya wabunge walisema mikopo hiyo inashindikana kurejeshwa kwa kuwa waliokopeshwa siyo wanufaika, bali kuna watu wameunda vikundi na kuzichukua huku wakitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza.
Fedha hizo zinatukumbusha mabilioni ya JK (Jakaya Kikwete) ambazo zilitolewa kwa kila mkoa kukopesha makundi maalum ziliishia ‘kupigwa’ kiasi cha lengo kutofikiwa.
Aidha, CAG alisema halmashauri 83 hazikuchangia Sh. bilioni 6.68 ya asilimia 10 ya bajeti yao kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kusaidia makundi hayo kubadilisha maisha yao.
Pia,alibaini halmashauri zilifanya malipo ya Sh. milioni 556.84 kwa wastaafu waliofariki,kutoroka,kuacha kazi na waliokuwa likizo.
Aidha,alibaini matumizi yasiyo na manufaa yaliyofanyika kwa bidhaa ambazo hazijawahi kutolewa, huku kukiwa na matumizi ya fedha mbichi (fedha ambazo hazijapelekwa benki) zaidi ya Sh. bilioni 17 kwa halmashauri 147.
Kwa ujumla huu ni upigaji ambao kimsingi unakatisha tamaa walipakodi wa nchi hii, ambao wanataka kuona fedha wanazolipa zinasimamiwa vyema, zinafanya kazi zinazotakiwa na siyo watu wachache kuzifanyia ubadhirifu na kunufaika wakati wengi wanaumia.
Fedha zilizoibwa zingeweza kununua vifaa tiba, dawa na kujenga majengo ya zahanati, vituo vya afya na hospitali. Pia zingeongeza miundombinu ya shule na barabara, ili Watanzania wote wanufaike na keki ya taifa, lakini zinapigwa na wachache kwa manufaa ya wachache.
Ni muhimu walipakodi wakaona uwajibikaji wa wazi wa kila shilingi yao; kwamba watu wakamatwe na kufikishwa mahakamani, lakini mali walizozipata kwa njia haramu zifilisiwe kwa kuwa wametudhulumu Watanzania licha ya imani tuliyokuwa nayo kwao.
Bila hatua madhubuti kuziba mianya ya upotevu wa mapato, hali itaendelea kuwa hii ambayo itakatisha tamaa, itaonekana serikalini ni shamba la bibi kwamba mtu anaweza kuingia kwa ujanja wake akachota fedha akazitumia na kuendelea na maisha kama kawaida.
Bila kudhibiti mchwa hawa, Watanzanja watakata tamaa itaonekana fedha za umma ni shamba la bibi kila mtu anavuna atakavyo, hivyo ni muhimu kuona uwajibikaji kwa waliopewa dhamana ya kusimamia fedha na rasilimali za umma kwa niaba ya watu takribani milioni 60.
Lazima kujenga misingi imara ya kukomesha upigaji wa mali za Watanzania ambayo ingepaswa kuwanufaisha kupitia huduma za kijamii kama afya,elimu,maji na miundombinu.
Kila kikao cha Bunge,kwenye maswali na majibu wabunge huwasilisha kilio cha wananchi wao mengi hujikita kwenye Wizara inayohudumia wananchi moja kwa moja TAMISEMI, wakitaka kujua lini barabara fulani itakamilika, lini zahanati,kituo cha afya au hospitali itapata vifaa tiba na dawa, lakini majibu huwa fedha zinatafutwa au mchakato unaendelea.
Kama kuna fedha zinapotea ambazo zingeweza kutatua changamoto hizo inamaanisha kwamba lazima hatua zichukuliwe kuhakikisha mianya ya wizi, ubadhirifu na ufujaji wa rasilimali za umma inazibwa, ili kila Mtanzania afurahie kulipa kodi kwa kuwa fedha yake itakuwa salama na inaonekana inafanya nini.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








