Na ndiyo maana imekuwa ikitoa makocha, kuajiri wengine na baadaye kuwarudisha wale wale wa zamani.
Tayari imetangaza kumrejesha kocha wake wa zamani, Juma Mgunda. Huyu huyu ambaye ilimwondoa Agosti, mwaka jana na kumpa nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi, ikimwajiri Mmarekani Melis Medo kuongoza jahazi lao.
Lakini ni kocha huyu huyu Medo alitimuliwa miezi miwili iliyopita na Coastal ikawa kwenye mchakato wa kusaka kocha mwingine kwa miezi yote hii, ikiwa chini ya Joseph Lazaro, leo hii Mgunda amerudishwa tena pale pale.
Sasa najiuliza, kwa nini Coastal ilimwondoa Mgunda na sasa imeamua kumrudisha? Sababu zilizowafanya viongozi wamwondoe leo hazipo? Imetajwa ni kwa sababu timu ilikuwa inafanya vibaya, leo amebadilika nini hadi kumtegemea timu itafanya vizuri?
Je, kama timu itaendelea kufanya vibaya, itamtimua tena Mgunda? Haya ni maswali ya msingi ya kujiuliza. Na si kwa mashabiki wa Coastal Union, lakini pia kwa viongozi wao.
Zipo taarifa za ndani zinadai kulikuwa na mgawanyiko, wengine wakitaka kocha mpya, lakini wengine wakimtaka Mgunda kwa sababu ni mzoefu, anayelifahamu soka la Tanzania, mazingira ya klabu, anayeweza kufundisha kwenye mazingira hata magumu ambayo klabu inapitia, lakini kikubwa zaidi kocha ni mwanachama wa Coastal Union.
Nadhani wale waliomtaka Mgunda wameshinda kwa hoja na kusababisha arejeshwe, kwani hivi karubuni tuliwasikia baadhi ya viongozi wakijinasibu kuwa na maombi mengi ya makocha mbalimbali wakiwamo kocha wa zamani wa Simba, Goran Copunovic, lakini Bernard Mwalala ndiye kwa kiasi kikubwa alikuwa akitajwa huenda angekuwa mrithi wa Medo.
Tatizo katika klabu ya Coastal inaonekana kuwa si nani anaifundisha, ila viongozi hawajajua tatizo la msingi linaloitafuna ndiyo maana wamekuwa wakimtoa mara kwa mara Mgunda na kumrudisha.
Nionavyo Mgunda wala si tatizo klabuni hapo na ndiyo maana hata hao wanaokuja baada yake hali inakuwa ni ile ile.
Naweza kusema kuwa Coastal Union kwa misimu miwili imeshindwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuisaidia timu baada ya kuondokewa na nyota wake mbalimbali akiwamo Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Ame.
Katika namna ya kushangaza, bado ikamtoa kwa mkopo mchezaji, Abushehe Issa kwenda Dodoma Jiji, na kijana aliyeonekana kuwafungia mabao mengi, Hamadi Majimengi naye akitimkia Ruvu Shooting.
Ni kweli Coastal Union haijawa timu yenye uwezo wa kuwazuia wachezaji wake kuhama, hasa kwenda katika timu kubwa, lakini ikiamua inaweza kuwabakisha mastaa wake kujiunga na timu kama Ruvu Shooting, Dodoma Jiji, Biashara United au kwingineko.
Ule umoja ambao huwa unapatikana kwenye klabu hiyo kutoka kwa viongozi wa klabu, mkoa, wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakati timu ikiwa kwenye hali mbaya ya kushuka daraja kama ungekuwepo kipindi chote, ungeweza kusababisha kupata wachezaji imara na kuzuia nyota kuondoka.
Kwa sababu ni wakati ambapo nguvu kubwa hutumika kuhakikisha timu haishuki daraja. Na hpo ndipo utakapojua kuwa tatizo la Coastal Union wala si kocha.
Niseme tu, kama viongozi wataficha sababu kuu ya Coastal kufanya vibaya na kuwa na tabia ya kutoa na kuingiza makocha na kuwarudisha tena, ipo siku mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Waswahili wanasema kuchagua sana nazi, mwisho huchagua koroma. Kutoa makocha hakusaidii, bali ni kutafuta sababu kuu ya timu hiyo kufanya vibaya, ambayo wenyewe wanaijua nayo, pamoja na mambo mengine, ni vigisu za chinichini baina ya viongozi wenyewe kwa wenyewe, ambao huungana wanapoona timu inataka kushuka. Ipo siku watashindwa kuibakisha katika Ligi Kuu na ndipo watakapokuwa wanakumbuka shuka wakati kumekucha.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








