Mrema ameshafunga ndoa yaliyoko mitandaoni ni wivu

27Mar 2022
Thobias Mwanakatwe
Nipashe Jumapili
Kisima cha ukweli
Mrema ameshafunga ndoa yaliyoko mitandaoni ni wivu

​​​​​​​WIKI hii Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alijadiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutangaza kuwa anataka kuoa binti mdogo na mweupe.

Wabongo kama kawaida yao, baada ya kusikia taarifa hizo, walianza kujadili ndoa ya Mrema huku wengine wakiweka hata picha za msichana waliyedai anataka kumuoa ambazo hazikuwa za kweli.

Katika mijadala, baadhi walifikia hatua ya kuanza kumchonganisha Mrema na familia yake kwamba watoto wake walikuwa wamekataa baba yao kuoa mwanamke mwingine. Mrema alichukua uamuzi wa kuoa baada ya mke wake, Rose, kufariki dunia Septemba, mwaka jana.

Watu hao ambao nawaita ni wanafiki, kwenye mitandao ya kijamii waliendelea kusema kama Mrema atafunga ndoa katika kipindi hiki cha Kwaresma, atakuwa amekiuka taratibu za Kanisa Katoliki ambazo kwa mujibu wa wao, hairuhusiwi.

Mijadala yote hiyo ilikuwa ikiendelea hata kabla ndoa haijafungwa lakini mzee Mrema hakukatishwa tamaa, akaendelea na maandalizi ya harusi yake kama kawaida.

Ilipofika Alhamisi, Machi 24, 2022, Mrema na mke wake mtarajiwa, Doreen Kimbi, wakajitokeza katika Kanisa Katoliki Parokia ya Uomboni, wakafunga ndoa kama kawaida, hivyo kuwaacha midomo wazi waliokuwa wakijadili suala hilo.

Kutokana na ndoa hiyo, waliokuwa wakijadili na kufukunyua mambo, wakabaki kama wamepigwa na kitu kizito kichwani kwa sababu picha ya mwanamke waliyekuwa wakimweka mitandaoni kwamba ndiye anaolewa na Mrema, ikawa tofauti na aliyejitokeza kanisani.

Baada ya ndoa kufungwa tu, wakaanza kuzua jambo jipya kwamba eti huyo mwanamke alikwishaolewa na mwanamume fulani na akaachika. Wakaenda mbali kwa kusambaza picha za mwanamke huyo akiwa na mwanamume ambaye walidai ni mume wake wa zamani.

Pia wakazusha kuwa mwanamke huyo amefuata hela kwa Mrema na kwamba mzee huyo kashamkabidhi hata kadi za benki. Lakini yote hayo Mrema akayapuuza na kuyaona ni uzushi tu.

Hivi sasa mzee Mrema anaendelea kula bata na mke wake.  Waliokuwa  wakishobokea ndoa hiyo kwa kuzusha kila jambo, wamebaki na umbeya wao mifukoni.

Uzushi ulioenezwa kabla na baada ya Mrema kufunga ndoa, hauleti afya kwa jamii ya kitanzania ambayo inatambua ustaarabu. Sote tunatambua kuwa Mrema ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali za uongozi hapa nchini, ikiwamo ya Naibu Waziri Mkuu, ni mtu makini.

Kwa anayemjua Mrema, hawezi kukurupuka na kuanza kumshutumu kuwa eti ameoa mke wa mtu. Wako wanaoweza kufanya hivyo lakini si kwa Mrema. Pengine  waliokuwa wakizusha yote hayo kabla na hata baada ya kufungwa ndoa, walidhani watamdhoofisha Mrema kisiasa na ndoa yake huku wakisahau kuwa walichokuwa wakikifanya ni kuzidi kumpaisha kwa umaarufu.

Nilifurahishwa na Mrema alivyowapa 'dongo' kiaina waliokuwa wakiendelea kuijadili ndoa yake pale alisema wanaoendelea kueneza uzushi na upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii, wanapoteza muda wao na vijiba vyao vya roho.

Mrema alisema uvumi wa mambo yote hayo unatokana na kwamba watu hawajazoea mtu akipendwa kwa dhati na mtu mwingine bali wamezoea rushwa wanahonga watu, wananunua watu, kwa hiyo wanafikiri kila mtu ananunulika.

Mrema awali alikwisha weka wazi kuwa alifuata taratibu zote zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na kulipa mahari na taratibu nyingine za kimila zinazostahili. Alisema sababu zilizomfanya aoe tena ni baada ya mke wake kufariki dunia na kumwacha katika mazingira magumu,  hivyo alimwomba Mungu amsaidie ili apate msaidizi mwingine.

Sasa kama Doreen na Mrema walikaa pamoja wakajadiliana na kukubaliana wafunge ndoa wawe mwili mmoja, wewe ni nani hadi uanze kutokwa na mishipa kuzusha umbeya kwenye mitandao ya kijamii. Ona sasa aibu imekushika.

Ifike wakati tunaotumia mitandao ya kijamii tuwe wazalendo wa kweli kwa kuitumia vizuri. Tusipende kuzusha mambo yasiyo ya kweli ambayo hayana faida zaidi ya kuvuna dhambi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Kwa maoni na ushauri tumia baruapepe: mwanakatwe2005@yahoo.com au 0692-276999