Mkandala asitishwe kujiunga Simba, Yanga

28Mar 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mkandala asitishwe kujiunga Simba, Yanga

UMEKUWA sasa ni kama ugonjwa au utamaduni kwa baadhi ya mashabiki wa soka, viongozi na hata makocha kuwatisha wachezaji wa Kitanzania kutoka timu zinazoitwa au kujiita ndogo kujiunga na Klabu za Simba na Yanga.

Tayari baadhi ya wadau wa soka wameshaanza kumtisha kiungo mshambuliaji Cleophace Mkandala kuwa eti asiharakishe kujiunga na timu yoyote ile kubwa iwe Simba au Yanga kwa sababu tu umri wake mdogo.

"Namshauri Mkandala, asiharakishe kwenda kwenye timu kubwa, atulie kwanza. Hizi timu zina upinzani mkubwa, hazina muda wa kumsubiri mchezaji kijana akue kwanza, na siyo yeye tu, nashauri wengine, tamaa hizi kubwa zisiwaponze." Haya ni maneno yaliyosemwa juzi tu kutoka kwa mmoja wa makocha wakubwa tu.

Sina haja ya kumtaja jina hapa kwa sababu lengo si jina lake, ila ni kuangalia ni kwa nini wadau wengi wa soka siku hizi wamekuwa na ushauri mbaya kwa wachezaji wa Kitanzania, wakitaka wazeeke wakiwa na timu zinazoitwa za mikoani.

Kwa sababu si yeye tu, bali kumezuka na wimbi kubwa la wadau wa soka, kutoa ushauri wa kuwataka wachezaji wasikimbilie Klabu za Simba au Yanga kwa sababu wataua vipaji vyao.

Ukisikiliza, kuangalia na kufuatilia, au hoja zao wanaleta mifano ya baadhi ya wachezaji ambao wametoka kwenye klabu hizo na kujiunga na klabu kubwa na hawakufanya vema. Ni kweli hutokea dunia kote, lakini si kwa wote.

Hata hivyo, wachezaji wengi wa Kitanzania wanaotoka kwenye klabu ndogo na kwenda Simba au Yanga hushindwa kung'aa kutokana na sababu zao binafsi na wala si kwa sababu ya klabu.

Wengi baada ya kupata pesa za usajili, kupata jina na umaarufu, wanabweteka na kuanza kuingia kwenye mambo mengine ambayo hayatakiwi kwa mchezaji, pia kuwa wavivu wa mazoezi.

Kuna mchezaji mmoja wa zamani aliniambia mchezaji kutoka nje ya Simba na Yanga anaposajiliwa na timu hizo anatakiwa afanye mazoezi mara mbili zaidi ya avyokuwa akifanya kwenye timu yake ya awali kwa sababu awali akiwa kwenye timu za chini huwa hakamiwi na anaweza kucheza mpira kirahisi, lakini anapoingia klabu hizo kubwa kila mpira anaogusa anakutana na watu ambao wanamkabili kisawasawa, hivyo lazima awe imara kwa mazoezi, na umakini zaidi, huku akili ikitakiwa kufanya kazi haraka sana.

Akasema hicho ndicho kinachowashinda wachezaji wengi. Hili ndilo linalotakiwa lihubiriwe na wadau wa soka, kuwataka kujiandaa kwenda kuwa mchezaji wa timu kubwa, kama vile mwanafunzi wa shule ya msingi anavyotakiwa kuandaliwa kuingia sekondari na si kumtisha kuwa huko sekondari au chuo hakuwezi kwa sababu kuna masomo magumu sana.

Cha kushangaza ni kwamba wakati wanawatisha wachezaji wa Kibongo, Simba na Yanga zinapokea wachezaji kutoka nje ya nchi ambao hawaogopi chochote, na wanaingia na kucheza soka kwa uwezo na mafanikio makubwa.

Vilevile klabu hizo pia zina wachezaji wa Kitanzania ambao nao wana uwezo mkubwa. Kina Feisal Salum, Aishi Manula, Bakari Mwamnyeto, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Dickson Job, Aboutwalib Mshery, hawa wote hawakuzaliwa Simba wala Yanga, wametoka kwenye timu zingine na wanacheza, tena kwa viwango vikubwa tu, mbona vipaji vyao havikufa? Tena wamejiunga wakiwa vijana wadogo tu.

Mbwana Samatta asingejiunga na Simba leo hii angekuwa hapo alipo? Alijiunga akiwa mdogo sana, je angeogopa kwa sababu kulikuwa na 'mafaza' kina Mussa Hassan Mgosi, angekuwa wapi?

Aboubakar Salum 'Sure Boy', baba yake Salum Aboubakar alijiunga na Yanga kutoka Sigara akiwa bado kijana mdogo, ikiwa na mastaa wakubwa, lakini hakujali, alijiamini na akawa staa kuliko mastaa aliowakuta.

Hata Mrisho Ngassa alisajiliwa kutoka Kagera Sugar, akiwa kijana mdogo, akawika kwa miaka mingi sana.

Ulimboka Mwakingwe akiwa bwana mdogo tu, alisajiliwa na Simba akitokea Reli ya Morogoro iliyokuwa imeshuka daraja, kwa namna ya kushangaza kuingia tu kwenye timu hiyo akaibuka kuwa staa mkubwa, mechi ya kwanza tu alimshangaza kila mtu, na akawa mrithi wa Steven Mapunda 'Garincha' .

Kapombe alitokea Polisi Morogoro na kusajiliwa na Simba kwenye kikosi cha pili, lakini alipojaribiwa mechi moja tu ya Ligi Kuu, ikawa ndiyo moja kwa moja hadi leo.

Mpira ni kujiamini na kufuata miiko yake tu basi, siyo kudanganyana kuwa bado mdogo, ina maana watu wanataka wachezaji wajiunge na Simba na Yanga wakiwa wana miaka kuanzia 30? Mbona hata Ulaya wachezaji wa miaka 19 wanachezea timu kuwa tena kwa kiwango cha juu? Haya leo Kelvin John yupo KRC Genk, kafanya kosa kuwahi kwenda kuichezea?

Tuache kuwatisha wachezaji, cha kufanya ni kuwakumbusha kuwa na nidhamu ya mazoezi na kufuta miiko. Kwa sasa Mkandala anatafutwa na klabu nyingi, asiogope, badala yake aende tu kusajiliwa kwa kiasi anachohitaji, ila anachotakiwa kufanya ni kwamba ajiandae na ushindani wa namba, kwani anachotakiwa kufanya ni mazoezi zaidi ya yale anayofanya Dodoma Jiji, ajitume na kuwa na nidhamu kwani Jiji la Dar es Salaam lina mambo mengi.