Nakumbuka wakati nakua, nilikuwa namwona mama na dada zangu wakienda bondeni na mitungi na vibuyu na kurudi na maji ambayo tulikunywa bila kuchemsha na mengine wakipikia chakula.
Sikupata kuona hata siku moja nguo zikifuliwa nyumbani au mtu akiogea nyumbani. Kila aliyetaka kuoga au kufua, aliteremka bondeni mtoni na kufua na kuoga huko huko. Huo ndio ulikuwa utaratibu.
Nilipokua kidogo na kutambua hili na lile, siku moja nikaenda na kaka zangu bondeni kuoga, ndipo nikabaini kuwa kumbe wanawake na wanaume walitengwa na kichaka kilichokuwa mtoni na kila upande ulifanya yake na kuondoka.
Hakukuwa na tabia mbaya ya watu kuingiliana kama yanayofanyika leo hii kwani kosa hilo lingesababisha kesi nyingi za ubakaji na udhalilishaji mwingine wa kijinsia.
Jinsi miaka ilivyosonga mbele, tukahamia mjini ambako hakukuwa na mabonde na vijito vya watu kuoga na kufua bali kulikuwa na mabomba ya maji tiririka. Kwangu mimi ulikuwa mshangao, lakini nikazoea kidogo kidogo.
Nikaambiwa kuwa maji hayo yanatoka ziwani lakini yanapitia kwenye matangi kusafishwa na kisha kuingia kwenye mabomba ambapo hata kunywa tulikunywa hivyo hivyo kutoka kwenye bomba, hatukusikia madhara yoyote.
Lakini kubwa lililonishangaza zaidi ni kwamba kulikuwa na mabomba ambamo tulipenyeza sarafu na maji kutoka. Hizo ni enzi za Mwalimu Julius Nyerere.
Ghafla maisha yaliposonga zaidi mbele, mabomba hayo ya kuingiza sarafu yakatoweka, yakaja haya ya mita. Hata mitaa enzi hizo mingi ilikuwa na lami, lakini nayo katikati hapa ikatoweka.
Sasa kinachonishangaza mimi hivi karibuni nikiangalia luninga, nikamwona Chifu Hangaya akifungua nadhani huduma ya maji bila shaka Chalinze, nikaona jinsi kinamama walivyofurahi, utadhani nchi inazaliwa.
Nilijiuliza kwa nini kinamama hawa wanapagawa hivi kwa kupata maji ya bomba? Leo zaidi ya miaka 60 ya Uhuru kinamama zetu wanafurahia hivi utadhani leo ni mwaka 1961 kwamba mkoloni leo kaondoka!
Mi nadhani kuna mahali tumekwama kujitambua kwamba ni kwa nini zamani mambo mengi yalikuwa mazuri lakini jinsi tunavyosonga mbele yanaharibika na viongozi baadhi yao wanafunga macho?
Hivi wakati ule mabomba yanatoa maji kwa kuchomeka tu sarafu kama ilivyokuwa kwenye muziki kwamba unaweka pesa muziki unapigwa, au unaingiza sarafu soda ya kopo inadondoka, au kwenye ATM ya pesa au ya maziwa huko Uchagani.
Teknolojia hiyo kumbe ilikuwapo miaka mingi, lakini kwa uzembe wetu na sababu zetu tukaiua na sasa tunashangilia maji kutoka kwenye bomba la kawaida, tena umbali mrefu kutoka majumbani ikilinganishwa na zamani ambao ulikuwa mrefu zaidi.
Maendeleo anayoyasimia Chifu Hangaya leo, si ajabu baada ya miaka kadhaa tukayachezea na kujikuta tunaanza upya kama tunavyofanya hivi sasa. Tulikuwa na vitu vizuri lakini leo utadhani hatukupata kuwa navyo.
Watanzania imekuwa ni kawaida yetu kuchukulia mambo kimazoea na kutotafakari kuwa huko mbele yatakuwaje na kujikuta tunafuja maendeleo na kulaumiana, lakini ni kutokana na uzembe wetu.
Nani hakumbuki kuwa wakati ule tunasoma, elimu ilikuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu? Leo akija mtu akasema tunatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu itakuwa sawa na nchi kuanza upya.
Nakumbuka enzi hizo wazazi walichokuwa wanajali ni kununua sare tu, kwa sababu hata masuala ya nauli hayakuwapo, tulikanyaga kwa mguu kutoka nyumbani hadi shuleni na kurudi, huku tukipata kifungua kinywa cha uji au bulga. Madaftari, penseli na peni bure.
Chuo kikuu hakukuwa na malipo zaidi ya kulipwa posho kila mwisho wa mwezi huku chakula tukifakamia bure, kuanzia asubuhi, mchana mpaka usiku, kumbuka na jioni kukiwa na chai tena ya maziwa au maziwa yenyewe. Tumetoka mbali, twendako pia ni mbali. Alamsiki!



.jpg?itok=nfwjwDzv)








