Muda umefika wachezaji kulipwa malimbikizo yao

19Mar 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Muda umefika wachezaji kulipwa malimbikizo yao

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeanza kutoa fomu za leseni kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) na First League (Ligi Daraja la Pili), kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23.

Fomu hizo zilianza kutolewa Machi 15, mwaka huu na mwisho wa kuchukuliwa na kurejeshwa ni Aprili 25, mwaka huu.

Kikubwa zaidi TFF imesisitiza klabu yoyote itakayokuwa inadaiwa na mchezaji haitapatiwa leseni ya ushiriki wa ligi msimu ujao.

Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (SPUTANZA), kimekuwa cha kwanza kupongeza hatua hiyo, na hii ilitegemewa kwa sababu mara nyingi ndio kimekuwa kimbilio la wachezaji mara wanapoona wanazungushwa kupata stahiki zao.

"Nawapongeza sana TFF kwa kuliona hili, hiki kilikuwa ndio kilio chetu cha muda mrefu, tumepigana sana kuhakikisha kanuni hii iwekwe kwa klabu inapotaka kupewa leseni, leo wamesikia kilio chetu.

Ni jambo la kuhuzunisha na kusikitisha kuona mchezaji anaiacha familia yake, anakwenda kukaa kambini kwa muda mrefu na kuitumikia timu kwa nguvu na jasho lake, lakini baadhi yao wamekuwa wakimaliza mikataba yao wanakuwa bado wanadai, pamoja na hayo wanakuwa wanazungushwa kitu ambacho hakipendezi kwenye zama hizi za soka la kulipwa," alisema mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Kisoki.

Kwa tangazo hili la TFF, huu sasa ndiyo wakati wa wachezaji kuanza kudai malimbikizo yao na wala si mwingine. Wakisubiri watachelewa.

Nilisikia kuna baadhi ya wachezaji wa klabu kubwa tu za Simba na Yanga wanazidai timu hizo mishahara yao ya tangu mwaka 2004.

Huwa nashangaa kwa nini siku zote hizi hawadai? Ukweli ni kwamba baadhi ya wachezaji wa Kitanzania wanachukulia kama walikuwa wakicheza kwenye klabu hizo kwa kuzisaidia na haikuwa kazi.

Ndio maana wamekuwa hata wakimaliza mikataba yao hawadai, badala yake wananung'unika kichinichini, au linapotokea jambo lolote kwa kumkwaza ndipo wanapofunguka.

Ndiyo maana unaweza kukuta kipindi hiki hakutokuwa na mchezaji wa kwenda kudai fedha zake.

Najua TFF wana orodha ya wachezaji wanaozidai klabu. Inawezekana ndiyo watakazotumia kuzibana klabu hizo, lakini pia wapo wachezaji ambao hawajapeleka malalamiko TFF wala SPUTANZA lakini wana vielelezo vyote, huu ndiyo wakati sasa wa kufanya hivyo ili kupata stahiki zao.

Hakuna klabu itakayokubali kunyimwa leseni na kushindwa kucheza Ligi Kuu msimu ujao eti kwa sababu ya madeni ya wachezaji. Watatafuta popote pale ili wamalize tatizo hilo.

Wasisikilize ahadi na maneno matamu ya viongozi kuwa wasubiri, au kuahidiwa kupewa ofa ya kufundisha timu na nyinginezo.

Tatizo kuna baadhi ya wachezaji wanazidai klabu mbalimbali za Ligi Kuu zikiwamo zile zinazoitwa au kujiita kubwa, lakini viongozi wao ukifika wakati kama huu, wanawasiliana nao na kuwapiga maneno kwa lugha nzuri ya matumaini ya kuwalipa, wakiwataka kukaa kimya kwa ahadi ya kuwalipa baadaye, kuwapa umeneja, au ukocha kwa wale wanaodai kwa muda mrefu.

Kumbe nia ni kupitisha muda wa leseni. Viongozi hao wanapozipata leseni wanaanza kutopokea simu na hapo wachezaji ndipo wanapoibuka na kudai, wakati tayari leseni zimeshatoka na hakuna chochote kitakachowapata.

Kutokana na hilo, wale wachezaji wa zamani wanaozidai timu hizi ambazo bado zipo kwenye Ligi Kuu, Championship na Ligi Daraja la Pili au Ligi Kuu ya Wanawake kwa sasa, ndiyo muda wa kukusanya vielelezo na kuvipeleka TFF kuonyesha madai yao, na hapo hakutokuwa na namna yoyote ile ya kuepuka kutolipwa.

Kitakachokuwepo tu hapo, ni namna gani ya kulipwa, kama ni kukabidhiwa hapo hapo au klabu zitakuwa zinakatwa kwenye mechi zao zitakazokuwa zinacheza. Wakati ni sasa, wachezaji wasikubali ahadi na maneno matamu ya viongozi, watakuja kujuta baadaye zoezi hili litakapomalizika na leseni kuwa mikononi mwa klabu, Hapo wajue kabisa hawatolipwa.