Simba imebakia peke yake katika michuano hiyo ya CAF baada ya Yanga na Azam FC za jijini pia kutolewa mapema sawa na KMKM na JKU kutoka Zanzibar kuaga michuano ya kimataifa kwenye hatua ya awali.
Timu hizo zitakutana katika mchezo wa Kundi D wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakati mchezo mwingine wa kundi hilo utakuwa ni kati ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast dhidi ya US Gendarmerie ya Niger.
Katika msimamo wa kundi hilo, Simba iko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne sawa na Asec Mimosas wakati vinara ni RS Berkane yenye pointi sita huku US Gendarmerie yenye pointi moja ikiburuza mkia.
Ikiwa nyumbani katika mechi yake ya kwanza dhidi ya ASEC Mimosas, Simba ilipata ushindi wa mabao 3-1 na ililazimisha sare ya ugenini ya bao 1-1, lakini mchezo uliopita ikivaana na RS Berkane huko Morocco ililala kwa magoli 2-0.
Ili Simba ijiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, licha ya kubakiwa na mechi mbili mkononi (baada ya kesho), inatakiwa kupata matokeo chanya katika mchezo huo kwa sababu itaongoza kundi hilo au endapo itapata sare basi itaendelea kukaa kwenye nafasi mbili za juu.
Wachezaji wa Simba na benchi la ufundi, huu ni wakati muhimu wa kuongeza umakini katika mechi hiyo ili timu yenu iweze kufikia malengo yake ya kucheza hatua ya nusu fainali au kubeba kombe la michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Hakuna kisichowezekana katika mpira wa miguu, kikubwa ni wachezaji kuongeza utulivu pale wanapokuwa na mipira lakini pia kujipanga kuirudisha kwenye himaya yao wapinzani wanapokuwa wameukamata.
Kama ambavyo walipambana katika mechi ya kwanza, wachezaji wa Simba wanatakiwa kuendelea kujituma kwa sababu ya kusaka ushindi, lakini pia kuendelea kutangaza vipaji vyao kupitia mawakala na makocha kutoka sehemu mbalimbali wanaofuatilia mechi za michuano hiyo.
Kila mchezaji afahamu mechi hiyo inaweza kubadilisha maisha na thamani yake kwa sababu, endapo watapata ushindi au mchezaji ataonyesha kiwango bora, ni wazi watajiweka kwenye nafasi nzuri sokoni.
Tunawakumbusha matokeo mazuri huja pale timu itakapofanya vizuri na maana yake ni wachezaji kupunguza makosa ya kizembe, nyota wa Simba wanatakiwa wafahamu wanakutana na wachezaji wenye uzoefu na michuano hiyo, timu yenye uzoefu na mashindano hayo, moja ya klabu yenye nguvu katika soka la Afrika.
Kama timu kutoka Afrika Magharibi na Kaskazini zimefanikiwa kutawala soka barani, huu ni wakati wa wachezaji walioko Afrika Mashariki kumaliza ubabe wa Waarabu na wao kujitengenezea ufalme mpya kwenye ramani ya mchezo huo unaopendwa na wenye mashabiki wengi zaidi duniani.
Watanzania huu ni wakati muhimu wa kuwa pamoja na Simba kwa sababu ikifanikiwa kusonga mbele, Tanzania itakuwa imepata pointi zaidi ambazo zitasaidia msimu ujao kupata wawakilishi wanne (wawili katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wawili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika), hivyo tuache itikadi zetu za ndani na kuwa kitu kimoja.
Ujumbe huu pia umekumbushwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ambaye amewakaribisha mashabiki wa soka kutoka ndani na nje ya jiji hili kujitokeza kuishangilia Simba ili iendelee kuvuna pointi kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Kila la kheri Simba, kila la kheri Afrika Mashariki.










