Dunia duara, vita vilivyoko ughaibuni vinatuhusu tuliko

04Mar 2022
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Dunia duara, vita vilivyoko ughaibuni vinatuhusu tuliko

DUNIA pamoja na nchi moja au nyingine kuwa na tofauti za umbali wa maelfu ya maili na kijiografia, hilo halimaanishi hatutegemeani.

Unapokuja katika masuala mbalimbali ya kimataifa, kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa na kijamii utabaini dunia ni kitu kimoja.

Anza kuangalia namna viwanda na bidhaa zake ambazo zinatengenezwa na kusambaa duniani kote, mfano magari, televisheni, simu, kompyuta, nguo za dukani na mtumba na vyakula mbalimbali vinaingia na kutoka mabara yote saba.

Afrika, tukiwa sehemu ya dunia pamoja na kwamba hatujainuka zaidi kiuchumi hasa kusini mwa jangwa la Sahara, kama nchi zilizoendelea tunategemewa kutoa malighafi zinazotegemewa uko nchi za mbali zitokanazo hasa shambani.

Bidhaa hizo zinahitaji kukusanywa huko zinakolimwa  zaidi yaani vijijini na kisha kuletwa mjini, ukiangalia kinachohitajika ni usafiri wa vyombo vya moto ambavyo hutumia mafuta iwe dizeli au petroli.

Ndio maana linapokuja suala la mgogoro hasa vita athari zipo za moja kwa moja na ambazo si za moja kwa moja, na kusababisha uchumi kuyumba.

Vita inapotokea jambo la kwanza ambalo litaanza kuiumiza Afrika ni kupanda kwa bei za mafuta.

Baada ya Russia kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine, bei ya mafuta ikapanda kufikia kwenye soko zaidi ya dola 100 kwa pipa moja.

Kiwango hicho ni kikubwa zaidi cha kupanda kwa bei tangu ilipotokea mwaka 2014.

Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya itapata pia athari za kiuchumi kwa kuwa ni mwagizaji mkuu wa ngano, kutoka Russia.

Pia Kenya katika ukanda huu ni muuzaji mkubwa wa chai kwenda Russia.

Mwaka jana pekee, Kenya iliuza chai yenye thamani ya shilingi za Kenya bilioni 6.2 kwa kipindi cha kati ya Januari hadi Novemba, lakini biashara hiyo sasa inaingia mashakani kutokana na vita hiyo.

Masuala ya kijeshi, Diplomasia na Usalama kwa Afrika pia yanaweza kuyumba kutoka na vita Russia na Ukraine, na kuiweka Afrika katika nafasi ngumu kwenye uhusiano wake na nchi kubwa duniani. Ingawa inaonekana kama ni mgogoro baina ya nchi mbili.

Ni kwamba hivi karibuni Russia imeanza kujitanua Afrika na imeanza kutoa misaada ya kijeshi kwa nchi za Afrika, kuanzia eneo la Mashariki, Pembe ya Afrika na Afrika ya Kati.

Maeneo hayo ni Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Mali, Msumbiji na kwingineko ambako kulianza kutazamwa kwa kina, sasa kutapunguzwa umuhimu wakati jamii ya kimataifa ikitazama Ukraine.

Russia ni miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa nishati ya gesi na mafuta duniani na mgogoro huu utaathiri uzalishaji wake ama kwa vikwazo ambavyo tayari vimewekwa na taifa moja kama vile Marekani na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).

Afrika tayari inapitia katika kipindi kigumu kiuchumi. Wiki iliyopita, ni wazi kupanda kwa bei ya mafuta kutaongeza bei zaidi ya bidhaa mbalimbali na kufanya hali kuwa ngumu zaidi.

Kupanda kwa bei ya mafuta huanzisha mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.

Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi zitalazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza mafuta kuliko kawaida na hili huathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi na kupunguza matumizi ya ambayo ingetumika kwenye mambo mengine.

Russia na Ukraine ndiyo wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani.

Misri, nchi yenye watu wengi na ushawishi mkubwa zaidi katika eneo la Kaskazini mwa Afrika ndiyo mwagizaji mkuu wa ngano duniani.

Ngano ni muhimu kwa taifa hilo kiasi kwamba waandamanaji waliomng'oa madarakani Rais Hosni Mubarak, walikuwa wakililia zaidi mambo mawili tu; mkate na uhuru.

Tayari Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeonya kwamba mgogoro huo utaathiri bei za vyakula na kusababisha njaa kwa maskini katika eneo la Kaskazini mwa Afrika.