Mkazo uwe kukomesha vikwazo kwa wanawake

03Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mkazo uwe kukomesha vikwazo kwa wanawake

MAADHISHO ya Siku ya Wanawake Duniani yameanza na yanatarajiwa kufikia kilele chake Machi 8, mwaka huu, huku Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, akiagiza uhamasishaji katika jamii ili kufanikisha maadhimisho hayo.

Waziri Gwajima anasema, yapo mengi ambayo yanataraji kujili kwenye kilele cha maadhimisho hayo, ikiwamo taarifa ya utekelezaji wa ulingo wa Beijing, kuimarisha zaidi hamasa na kuleta usawa wa kiijinsia.

Itakumbukwa kuwa ulingo wa Beijing kwa maneno mengine Mkutabo wa Nne wa Dunia wa Wanawake uliofanyika jijini Beijing, China mwaka 1995, ndio ulioweka msingi imara katika jitihada za wanawake kudai haki zao, ikiwamo kutaka usawa kati yao na wanaume.

Baada ya mkutano huo, nchi nyingi duniani zilianza kutekeleza maazimio ya mkutano huo ya kupunguza vikwazo dhidi ya wanawake pamoja na kuleta usawa wa kijinsia, hususani suala la kuweka usawa katika vyombo vya uamuzi.

Usawa wa kijinsia ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo wanawake wameendelea kupigania kwa lengo la kutaka kuwe na uwiano kati ya wanaume na wanawake kwenye suala la uongozi.

Wanapoelekea kwenye kilele cha maadhimisho hayo, tuwashauri kuondolewa kwa vikwazo vyote ambavyo vimekuwa vikichangia kuwafanya waendelee kubaki nyuma na kusababisha kuwapo kwa malalamiko.

Lakini tunaendelea kushuhudia jinsi gani serikali ya Tanzania imeonyesha utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa maazimio ya Beijing pamoja na mikataba mbalimbali iliyoridhia hususan ya kikanda ya kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake.

Mikataba na itifaki zilizoridhiwa na kutekelezwa kama za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) baada ya Mkutano wa Beijing tunaridhishwa jinsi Tanzania inavyoitekeleza. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akijitahidi kuhakikisha anamwinua mwanamke kwa kuwateua wengi katika nafasi mbalimbali za uongozi tangu aingie madarakani takribani mwaka mmoja uliopita.

Hatua hiyo inaonyesha ni jinsi gani Rais amedhamiria kumwinua mwanamke ili asiendelee kuwa mnyonge bali afanye kazi kama mwanaume, kutokana na ukweli kwamba, uongozi si mzigo bali na akili na uwezo wa kuongoza.

Kwa mantiki hiyo, tunawashauri wanawake ambao tayari wamepata nafasi za uongozi, watekeleze majukumu yao kikamilifu ili kujijengea sifa za kuwawezesha kuteuliwe katika ngazi nyingine za juu zaidi.

Tunaamini kwamba, uongozi si kwa kundi fulani au jinsi fulani bali awe mwanaume au mwanamke anaweza kuongoza ili mradi awe na sifa na vigezo vinavyotakiwa, hivyo suala la usawa wa kijinsia haliepukiki.

Kwenye suala hili la usawa wa kijinsia, tunadhani ni wakati sasa kwa watunga sera na wale walioko katika ngazi za maamuzi kuondoa vikwazo vyote ambavyo vimekuwa vikimfanya mwanamke kubaki nyuma.

Tunashauri hivyo kwani vikwazo kwa wanawake haviko katika uongozi tu, bali hata kwenye mikopo ya halmashauri nako kuna sintofahamu inayotokana na tuhuma za baadhi ya watumishi kujineemesha na kuacha walengwa.

Ikumbukwe kuwa wanawake ndiyo wanaobeba majukumu makubwa nyumbani kuanzia kwenye kulisha familia, hivyo tunadhani ingependeza kama wigo wa utoaji wa mikopo utapanuliwa na kuongeza fursa zaidi za kukopa bila riba au kwa riba ndogo.

Lakini kwenye suala la nishati, wanabeba mizigo mikubwa ya kuni kwa ajili ya kupikia nyumbani, hivyo tunashauri hata gharama ya gesi ishushwe ili wengi zaidi waweze kutumia nishati hiyo majumbani badala ya kusaka kuni na kuchangia uharibifu wa mazingira.

Iwapo hayo na mengine ambayo hatukuyataja na yamekuwa yakilalamikiwa na wanawake yakitekelezwa, dhana nzima ya Rais ya kutaka kumnyanyua mwanamke kuanzia msomi na asiye msomi, tunadhani itakuwa imetimia.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ya mwaka huu inasema; 'Kizazi cha Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu;

Tujitokeze Kuhesabiwa', inaonyesha maendeleo endelevu yanaletwa na jinsi zote.

Watunga sera na walio katika ngazi za maamuzi, tunawashauri waangalie jinsi ya kuondoa vikwazo vinavyowabagua wanawake katika uongozi, ili kuharakisha nchini kuwa na maendeleo endelevu.