Serikali ifuatilie kwa karibu mafanikio kuondolewa tozo

02Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali ifuatilie kwa karibu mafanikio kuondolewa tozo

JUMATATU serikali ilitanga kuondoa tozo ya Sh. 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa kwa watumiaji kwa miezi mitatu kuanzia Machi hadi Mei mwaka huu, ili kupunguza mzigo na kuwarahisishia wananchi maisha.

Aidha, Waziri wa Nishati, Januari Makamba, alisaini kuridhia mabadiliko ya kanuni, huku utekelezaji rasmi wa mabadiliko hayo ukianza leo.

Uamuzi huo utaikosesha serikali mapato ya Sh. bilioni 30 kila mwezi, lakini lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi hawapati shida hasa katika kipindi hiki ambacho kuna vita ya Ukrein na Urusi, ambayo tayari imesababisha bei ya mafuta ulimwenguni kuongezeka.

Tunaipongeza serikali kwa uamuzi huu ambao ni muhimu kwa manufaa ya wananchi wa kawaida, matarajio ya wengi ni kuwa bei za bidhaa mbalimbali zitashuka kwa kuwa mafuta yameshuka.

Kupanda kwa bei ya mafuta kuna athari kubwa kwa bidhaa mbalimbali ambazo zinagusa maisha ya mwananchi moja kwa moja, inapotokea bidhaa zimeshuka faida siyo kwa waendesha magari pekee bali kwa wananchi wa kawaida.

Mfano anayeuza bidhaa za vyakula anasafirisha kwa gari kutoka shambani hadi sokoni, inapotokea bei ya mafuta imepanda bei ya kusafirisha huongezeka maana yake inabidi muuzaji wa bidhaa aongeze bei, ili faida yake iendelee kupatikana.

Tunaamini bei za mafuta kuanzia leo zimeshuka, ili mwananchi wa kawaida kabisa anufaike ni muhimu sasa serikali kufuatilia bei ya bidhaa mbalimbali.

Tunatambua kuwa biashara ni huria na serikali haipangi bei ya bidhaa lakini inasimamia kuhakikisha wananchi hawaumizwi sana, na katika kuona hali hiyo imeamua kuondoa tozo ili kusaidia zaidi.

Ili mwananchi wa kawaida aone ahueni iliyolengwa na serikali ni lazima bei za bidhaa zishuke, isipokuwa hivyo itakuwa hakuna tofauti kwake, kwa kuwa maisha ni yale yale.

Kama alikuwa ananunua mkate mkubwa Sh. 3,000 sasa bei irudi Sh. 2,500 ya awali, kwa kuwa sasa zimepanda kwa madai kuwa mafuta yamezidi kupaa, hali inayofanya maisha kuwa magumu na wengi kushindwa kumudu gharama za maisha.

Itapendeza kama baada ya miezi mitatu serikali itafanya tathmini kuona ahueni kwenye maisha ya kila na kuendelea kuondoa tozo hiyo, ili maisha yawe rahisi zaidi.

Tunatambua kuwa fedha hii iliongezwa kwa ajili ya Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), ambaye anawajibu wa kusimamia barabara hizo.

Kwenye kila mkutano wa bunge, wabunge wengi wanapaza sauti juu ya hali mbaya ya barabara kila mmoja akieleza ni muhimu kwa maendeleo ya maeneo husika, huku madaraja na makalavati yakiharibika kiasi cha kukatisha mawasiliano baina ya eneo moja na jingine.

Kwa mabadiliko haya maana yake fedha hizo hazitapatikana, lakini tunaamini serikali imejipanga vyema hasa kutumia fedha za mikopo mbalimbali ambayo nchi imekuwa ikipata kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwamo miundombinu.

Tunaamini kwamba kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu ikiwamo utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya kupanda kwa bidhaa za vyakula na ujenzi ambako kumelalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu.

Ni muhimu kufanya hivyo kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu hupandisha bei kwa lengo la kujipatia faida kubwa, huku wananchi wakiumia.