Kosa amefanya mwamuzi, Karia anahusika vipi hapo?

19Feb 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kosa amefanya mwamuzi, Karia anahusika vipi hapo?

MJADALA wa waamuzi nchini umeendelea kuwa mkali, na sasa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, naye akiibuka na kulizungumzia hilo.

Alipokuwa akifunga semina ya waamuzi, Karia amewataka kushirikiana na kutimiza majukumu yao ya uwanjani kwa pamoja kwa sababu wao ndiyo wamesababisha kilio cha kutaka kuletwa hapa nchini kifaa au mashine ya msaada iitwayo VAR.

Akashangazwa kuona waamuzi wako watatu mpaka wanne uwanjani, lakini kazi hiyo inaonekana anaachiwa mmoja tu ambaye ni mwamuzi wa kati.

"Kuna maamuzi mengine yanafanyika ambapo mwamuzi wa kati hajaona, je wengine watatu hawajaona, wakaambiana? Au wanachunguzana au wanataka mmoja aingie kwenye lawama peke yake?" Akawauliza na kuongeza.

"Mafunzo yanakuja wakati muafaka wakati ambapo kuna taharuki kuhusu uchezeshaji wenu. Baadhi ya makosa ni ya kibinadamu, mengine ya uzembe au makusudi, yanapofanyika mimi ndiyo mhanga na tangu nimekuwa kiongozi sijawahi kumfuata mwamuzi kutoa maelekezo zaidi ya kuwaambia wachezeshe kwa haki," alisema Karia wakati akifunga semina hiyo.

Hata hivyo Karia alisema waamuzi wanatakiwa kulindwa na wasiingizwe kwenye matatizo ambayo si ya kwao, ingawa anakiri kuna baadhi si waaminifu.

Hili limekuja, baada ya mjadala wa takribani wiki mbili za waamuzi kushtumiwa kwa kile kinachosemekana kuchezesha vibaya.

Baadhi ya viongozi wa serikali, wadau wa soka, watangazaji wa wachambuzi wameonekana kuingia kati na kusababisha mjadala mkubwa.

Hata hivyo kwa uzoefu wangu kwenye masuala ya michezo, ni kwamba mhemko huu umekuja baada ya timu moja kuonekana inabebwa na nyingine inaonewa. Kama zote zingenufaika na maamuzi mabaya ya waamuzi wala haya yasingekuwepo.

Simba na Yanga kwa miaka mingi zimekuwa zikinufaika mno na makosa yanayoitwa ya kibinadamu. Na tumekuwa tukiandika sana ni kwa nini makosa ya kibinadamu yanazinufaisha zaidi timu hizo kongwe? Sijawahi kuona au kusikia mihemko kama hii ya sasa, kwa sababu tu timu moja ni kama haikunufaika na makosa hayo kama wenzao.

Ifike wakati sasa waamuzi wanapokosea, basi kosa libaki kwa waamuzi na si Rais wa TFF kwa sababu hahusiki na lolote. Hahusiki kuendesha ligi, kupanga waamuzi au kuchezesha.

Baadhi ya wadau wa soka wamekuwa na lawama za jumla yanapotokea matatizo kama hayo. Wanakosea waamuzi, lawama kwa Karia. Anakosea mwamuzi wa kati, lawama kwa waamuzi wote. Hata anapokosea mwamuzi wa pembeni, bado lawama zinaenda kwa waamuzi wote.

Nadhani sasa kila mtu abebe kosa lake. Kama ni la mwamuzi wa kati liwe lake peke yake, na kama wa pembeni alaumiwe yeye tu.

Namuunga mkono Karia anaposema kunakosekana ushirikiano baina ya waamuzi kusaidiana na kuamua kitu kimoja. Ni kama wote wanamtegemea mwamuzi wa kati. Asipoona yeye basi. Wa pembeni wao hudhani kazi yao ni kuonyesha mpira unatoka, au kosa. Kuna wakati mchezaji anafanyiwa rafu pembeni, lakini hanyooshi kibendera hadi mwamuzi apulize kipenga. Unashangaa kazi yake ni nini? Amewekwa kule kwa kazi gani?

Hebu wawaige waamuzi wa Zanzibar waliochezesha mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, mwaka huu.

Mwamuzi hakuliona tukio la kipa, Mathias Kigonya wa Azam kumrukia mguu, Pape Sakho, lakini aliitwa na mwamuzi wa pembeni akaifanya kazi iliyomfanya kuwa pale. Akamwambia kipa amefanya kitendo hicho kwani alikishuhudia, hivyo kumsaidia mwamuzi wa kati kufanya uamuzi wa kuamuru pigo la penalti.

Mwamuzi wa kati alishaonyesha kuchanganyikiwa, kwani hakujua nini afanye, maana hajaona tukio, lakini uwajibikaji wa pamoja ukafanya kazi. Waamuzi wa Tanzania Bara wanakwama wapi?