Ufinyu mabao Ligi Kuu tatizo lipo hapa

21Feb 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ufinyu mabao Ligi Kuu tatizo lipo hapa

UKIACHANA na Kombe la FA ambapo timu zinabugizwa mabao sita mpaka saba, bado idadi ya mabao kwenye mechi nyingi za Ligi Kuu haziridhishi.

Matokeo ya bao moja au mbili, ndiyo yametawala kwenye mechi nyingi za Ligi Kuu. Ni mara chache sana kuona timu ikipata ushindi wa mabao kuanzia matatu kwenda mbele msimu huu.

Tuliona msimu uliopita, timu kama Simba ikipata ushindi wa mabao mengi kwenye mechi kadhaa za Ligi Kuu. Na haikuwa msimu uliopita tu, karibuni misimu minne, Simba ilikuwa timu ambayo ilikuwa ikipata ushindi wa mabao mengi kwenye baadhi ya mechi zake.

Ushindi mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu msimu huu, Simba iliupata Desemba 24, mwaka jana ilipoichakaza KMC mabao 4-1 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora, na pia ilipoichapa Ruvu Shooting 3-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Hata Yanga nao, pamoja na kwamba msimu huu iko vizuri kuliko misimu mingine iliyopita, lakini bado haipati ushindi ambao wanachama na mashabiki wao inautarajia kutokana na ubora wa michuano hiyo.

Mpaka sasa ushindi mkubwa wa Yanga kwenye Ligi Kuu ni ule wa Desemba 31, mwaka jana, ilipoichapa Dodoma Jiji mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, na unaokaribiana na huo ni ule wa Novemba 2, ikiibamiza Ruvu Shooting 3-1.

Angalau Azam, ambayo imepata ushindi wa mabao manne kwenye mechi mbili mpaka sasa, ilipoibamiza Ruvu Shooting mabao 4-1 Desemba 23, mwaka jana na 4-0 dhidi ya Prisons Januari 22, mwaka huu.

Ukiacha timu hizo kubwa, matokeo ya timu zingine zikicheza zenyewe kwa zenyewe ndiyo hayaridhishi kabisa. Huwa kama si suluhu, sare ya bao 1-1, basi zitafungana 1-0, 2-1, ikizidi sana mabao 2-0.

Huwezi kukuta mechi kama ya msimu uliopita, ambapo JKT Tanzania iliichakaza Mwadui mabao 6-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Oktoba 28, 2020, au mechi zingine ambazo zilikuwa na idadi kubwa ya mabao.

Kwa sasa ni za kuhesabu, tena kwa timu kubwa, ambazo pia nazo ni kama nazo zimeanza kupungua, ingawa ligi haijamalizika. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa mzunguko wa pili ndiyo huwa mgumu zaidi kuliko wa kwanza.

Tatizo ni nini? Inawezekana ikawa ni viwanja, hasa vya mikoani havipo kwenye hali nzuri, hali inayosababisha wachezaji kuwa na kazi ngumu ya kuuweka mpira wavuni. Yupo mtu anaweza akahoji, mbona viwanja ni vibovu hata wakati timu zinashinda mabao mengi huko nyuma.

Ni kweli, lakini inavyoonekana kila muda unavyozidi kwenda viwanja hivyo navyo vinazidi kuwa vibovu zaidi. Na kwa sasa tumeona kuna baadhi ya mikoa mvua kubwa inanyesha, huku mechi zikiendelea, wachezaji wakipata tabu hata kupiga tu mpira, achilia mbali kukokota.

Tatizo la viwanja nalo linapunguza uhondo wa kuona mabao mengi yakifungwa kwenye Ligi Kuu. Pili ni kwamba msimu huu timu nyingi zimejizatiti. Wadhamini wa Ligi Kuu, wamewekeza pesa, ambazo zimefanya timu nyingi kulipa mishahara na posho za uhakika, hivyo wachezaji kujituma.

Kingine ni kupungua kwa timu za Ligi Kuu. Kwa sasa kuna timu 16 tu. Wachezaji wa timu nne zilizopunguzwa misimu miwili nyuma kulipokuwa na timu 20, tunawaona wameenda kuziongezea nguvu timu zilizobaki, hivyo kuwa imara.

Mwisho ni ukweli mchungu kwamba, kuna tatizo kubwa la ufungaji kwa wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu. Ukiangalia zinapatikana nafasi nyingi, lakini wanashindwa kuweka mpira ndani ya wavu. Ni wachezaji wachache sana kwenye Ligi Kuu wenye uwezo wa kutumia nafasi chache zinazopatikana kufunga mabao.