Aidha, sheria hiyo imeainisha mambo ambayo yatahesabika ni ugaidi kuwa ni kusababisha hofu, vitisho na maandamano ambayo yatasababisha kifo au vifo basi mhusika atashtakiwa kwa ugaidi.
Licha ya wadau kuitwa kutoa maoni yao waliojitokeza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, waliofika Jumamosi ni Kituo Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jambo linalozua maswali kuwa wadau wengine wako wapi na kwanini hawakuja mbele ya kamati kutoa maoni yao.
Ni kawaida watu wanaitwa kutoa maoni hawajitokezi au wanajitokeza wachache, sheria inapopitishwa ndipo malalamiko hujitokeza kwa wingi kuwa ni mbovu au haikujali maslahi ya umma.
Wanapojitokeza wadau au wananchi wengi kutoa maoni inasaidia kuboresha sheria husika, ili inapoanza kutumika inakuwa haina makandokando mengi ambayo yataleta utata kwenye utekelezaji.
Ni muhimu sana wadau wanapoitwa kutoa maoni kuitikia wito, lakini muda wa kutoa maoni uwepo wa kutosha, ikiwamo njia mbalimbali zitakazohakikisha wananchi wengi wanasoma na kutoa maoni yao.
Wabunge ni wawakilishi wa wananchi, lakini muswada unapoletwa na serikali wanaujadili kwa kadri ya uelewa wao, ndiyo maana wananchi wanashirikishwa kupitia makundi yao kupeleka maoni ili sheria iwe shirikishi.
Mathalani, LHRC imebainisha kasoro nyingi kiasi cha kupendekeza kufutwa kwa kifungu kizima cha masuala ya ugaidi kwa kuwa itawapa shida sana Mahakama kutafsiri sheria huku ikitoa nafasi kwa watu kuonewa au kuumizwa baada ya kutangazwa kuwa ni magaidi na kuwekwa kwenye gazeti la serikali.
Pia walisema kuacha ilivyo kuitaipa Mahakama wakati mgumu kupima hofu au kutishika kwa umma, kwamba itatakiwa kuita mtu mmoja mmoja kumuhoji kama alitishika.
Walisema kama mtu akiwasha moto kwenye mtaa na kuzua taharuki kwa sheria hiyo atashtakiwa kama gaidi, na kwamba tatizo kubwa itakuwa kwenye utekelezaji.
Wadau hao wanasema sheria imeangalia maandamano ya kisiasa na kusahau kuwa kuna ya kidini na mengine ambayo ni ya taasisi husika, lakini sheria inakizana na katiba ambayo inaruhusu mikusanyiko.
Kama ambavyo wataalamu wa sheria wameona mambo mengi ikiwamo kuipa shida Mahakama na kuilazimu kwenda bungeni kupitia kumbukumbu za Bunge, ili kujua mbunge au wabunge walimaanisha nini kwenye jambo husika.
Ikiwa wananchi wengi watajitokeza kutoa maoni yao itasaidia kuwa na sheria shirikishi, lakini haitakuwa na malalamiko kwenye utekelezaji.
Kwa ujumla kuna mambo mengi ambayo yameibuliwa na LHRC yanaonyesha kuna tatizo kubwa kwenye namna ambavyo suala la ugaidi linatazamwa, sheria inayotungwa siyo kwa ajili ya wabunge bali kila Mtanzania hivyo ikiachwa na kupita ilivyo kutakuwa na shida kubwa.
Mathalani, madhara kwa nchi itakuwa ni pamoja na kutambulisha duniani kuwa ina magaidi wengi hivyo watalii, wawekezaji kuogopa kuja, huku taasisi za fedha kutoleta fedha kwa nchi ambayo imejitangazia kuwa na magaidi wa ndani.
Maofisa hao walisema ni muhimu sana sheria hiyo inapotungwa isiangalie matukio yaliyoko au yaliyowahi kutokea nchini, bali utekelezaji wa sheria husika, ili kuhakikisha hakuna madhara kwenye haki za binadamu.










