TAKUKURU isisubiri maelekezo ya viongozi

09Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TAKUKURU isisubiri maelekezo ya viongozi

RAIS Samia Suluhu Hassan alimaliza ziara mkoani Mara juzi akiwa ameagiza wakaguzi wa ndani katika mkoa huo wabadilishwe vituo  vya kazi kutokana na kuwapo na ufujaji wa fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali, hivyo kusababisha utekelezaji wa miradi mkoani humo kuchelewa.

Aidha, katika kuhitimisha ziara hiyo, mjini Bunda juzi, Rais pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) mkoani Mara kuhakikisha inafuatilia kupambana  ili kudhibiti matukio ya ufujaji wa fedha yanayoendelea ndani ya halmashauri.

Kwamba, ndani ya mkoa miradi kadhaa pesa zinafujwa, pesa zinaliwa na hakuna ripoti unayopita hadi mwaka ndio mkaguzi anasema, halmashauri  haikufanya vizuri, kwamba madudu hayo hayaonekani kwa sababu wakaguzi wa ndani ni sehemu ya wafujaji wa fedha hizo.

Pia Rais Samia aliombwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kutopeleka Sh. bilioni 24 kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Musoma hadi atakapojiridhisha kuwa zinakwenda kutekeleza kazi iliyopangwa, kutokana na kuwapo shaka ya matumizi yake.

Kutokana na maelekezo ya Rais, tunadhani kwamba ipo haja kwa TAKUKURU kuangalia uwezekano wa kuwa inachukua hatua mapema kuokoa fedha za Watanzania badala ya kusubiri malalamiko ya wananchi kwa viongozi.

Tunaamini kwamba njia nzuri, ni watumishi wa taasisi hiyo kuwa  na utaratibu wa kufuatilia miradi yote ya  maendeleo mara tu inapoanza kutekelezwa, ili kujua hatua kwa hatua jinsi fedha za umma zinavyotumika.

Kwa njia hiyo na nyingine zinabuniwa na taasisi hiyo, inaweza kusaidia kuwabana wajanja wachache wanaojinufaisha kwa fedha za umma kutekeleza miradi chini ya kiwango na kuisababishia serikali hasara.

Rais anasema kazi ya taasisi hiyo ni kuzuia rushwa, na anaitaka ifanye  kazi mara tu miradi inapoanza kwenye maeneo yao. Nasi tunaamini kwamba kwa utaratibu huo, fedha za umma zinaweza kuokolewa.

Watumishi wa taasisi kusubiri wananchi wapige kelele ndipo wafanye uchunguzi, tunaona kama watakuwa wamechelewa na watakuwa hawajapambana au hawajazuia rushwa kwa mujibu wa majukumu yao waliyopewa kisheria.

Kwa maelekezo ya Rais, kuzuia vitendo vya rushwa, ndio kazi ya taasisi hiyo, siyo kusubiri ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndipo ianze kufukuzana kwenda kuwadhibiti waliofanya makosa. Nasi tunamuunga mkono.

Tunaamini kwamba, TAKUKURU ina watumishi wenye taaluma mbalimbali ambao wanaweza kutumika katika vita dhidi ya rushwa na kusaidia kukomesha vitendo hivyo katika jamii ili kusaidia kuharakisha maendeleo.

Waswahili wana msemo kwamba; 'ukiona mwenzio ananyolewa, na wewe tia maji'. Hivyo tunadhani watumishi wa taasisi hiyo kote nchini watakuwa wamejifunza kutokana na maelekezo ya Rais kwa wenzao wa Mara.

Imani yetu katika hilo, inatokana na ukweli kwamba karibu maeneo yote nchini, mawaziri na viongozi wetu wakuu wa kitaifa akiwamo Rais katika ziara zao wamekuwa wakipokea malalamiko ya wananchi kuhusu kukwama kwa miradi ya maendeleo ingawa serikali inajitahidi kupeleka fedha.

Ni matarajio yetu kwamba, watumishi wa taasisi hiyo nchini watazingatia maelekezo hayo na kusimamia miradi yote ya maendeleo ikiwamo ya ujenzi wa barabara, shule, zahanati, maji na mingine mingi tangu inapoanza.

Hatua hiyo inaweza kusaidia watumishi wa TAKUKURU kubaini ubadhirifu wa fedha za umma na kuwachukulia hatua wahusika badala ya kusubiri kuletewa ripoti mezani ndipo wafuatilie.

Rushwa si tu adui wa haki, bali pia inachelewesha maendeleo, ndiyo maana  tunashauri kuwapo kwa uvumbuzi na ubunifu wa kukabiliana nayo katika miradi ya maendeleo, kwa kufuatilia utekelezaji wake tangu mwanzo.