Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo alipokuwa alipokuwa akizungumza na majaji, wanasheria na mahakimu katika viwanja vya Maisara wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Alisema wakati umefika kwa majaji na mahakimu kuongeza nguvu katika usikiliza kesi na kusimamia haki katika kesi zinazofikishwa mahakamani.
Alisema kitendo cha kesi nyingi kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa na kutolewa hukumu, kinapunguza heshima ya mahakama hasa washitakiwa wanapoachiwa katika mazingira ya utata licha ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha.
Alisema mahakama ni mhimili muhimu na una kazi kubwa kutafsri sheria na kusikiliza kesi kwa wakati na majukumu hayo yanapaswa kuzingatiwa ili kuimarisha misingi ya utawala wa sheria.
Alisema kuna kesi zinazolalamikiwa na wananchi kama vile za dawa za kulevya na unyanyasaji wa kijinsia ambazo hupelekwa mahakamani huishia hewani na wahusika kuonekana mitaani wakitamba.
Balozi Seif alisema ushahidi wa wazi katika baadhi ya kesi zinazopelekwa hutolewa na wahusika lakini kinachojitokeza kwa baadhi ya majaji na mahakimu kueleza kuwa ushahidi bado haujakamilika.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo, Balozi Seif aliwakumbusha watendaji wa mahakama kuchukua hatua za haraka katika kutoa uamuzi ili kupunguza mlundikano wa majalada ya kesi mezani kwao.










