Maofisa hao, Daniel Ngoma na George Magoti wa Takukuru na Godwin Mnubi wa uhamiaji, wanadaiwa kumuua Evarist Ngiba (56) mkazi wa Mwanga Vamia, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Wanadaiwa kutenda mauaji hayo Januari 26, mwaka huu, saa 11 jioni katika eneo la Mjimwema ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alithibitisha kukamatwa na kushikiliwa kwa maofisa hao.
“Tumewakamata maofisa hawa kuhusiana na tukio hili. Mpaka sasa watuhumiwa wako mahabusu katika kituo chetu kikuu cha polisi, mpaka hapo tutakapomaliza uchunguzi na baadaye kuendelea na hatua zingine,” alisema.
Alisema maofisa hao wanashikiliwa na polisi kutokana na kutuhumiwa kufanya mauaji ya Ngiba aliyekuwa akituhumiwa kuwa mwizi.
Kamanda Mtui alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kumpiga Ngiba katika sehemu mbalimbali za mwili wake hivyo kupata maumivu makali na kufariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni.
.
Naye Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Mussa Misalaba, alipoulizwa na kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha kukamatwa kwa maaofisa wawili wake lakini alisema hajui lolote kuhusiana na tuhuma dhidi yao.
Kwa upande wake, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Maurice Kitinusa, alipoulizwa na Nipashe, alitihibitisha kupata taarifa hizo licha ya kutoeleza kwa undani.










