Huo ukawa mwisho wa enzi wa Simba, baada ya miaka mitano ya mfululizo wa ubingwa. Ilikuwa na wachezaji mahiri kama kina Athumani Mambosasa, Daudi Salum, Mohamed Kajole. Nico Njohole, Thuwein Ally, Adam Sabu, Jumanne Hassan 'Masimenti', George Kulagwa, Abdallah Mwinyimkuu, Martin Kikwa, Mohamed Bakari 'Tall' na wengine wengi ambao huko nyuma si tu walilitetemesha soka la Tanzania, bali Afrika nzima.
Baadhi ya wachezaji hao walikuwepo mwaka 1974 Simba ilipofika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika na hata wale waliokwenda kupindua mechi nchini Zambia kwa timu ya Mufulira Wanderers mwaka 1979, ilipokwenda kushinda ugenini mabao 5-0 na kusonga mbele, wakati wiki mbili nyuma ilitoka kufungwa mabao 4-0 nchini Tanzania. Ni moja kati historia zisizofutika kwenye soka la Afrika.
Pamoja na umahiri wao wote, baada ya kipigo na kuukosa ubingwa, viongozi wa klabu ya Simba wakafanya maamuzi magumu. Wakawapa mkono wa kwaheri wachezaji wengi wa timu hiyo, wenye majina makubwa, na kuanza kuingiza damu changa lakini wenye uwezo wa kusakata kabumbu, timu ikaanza kukaa sawa.
Hata msimu huu hali ni hiyo hiyo. Ukiwaangalia wachezaji wengi wa Simba ni wale wale walioipa Simba mafanikio makubwa miaka minne nyuma, Ubingwa wa Tanzania Bara, Kombe la FA na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili. Wakapata majina makubwa.
Lakini ukweli lazima usemwe kuwa kwa sasa wengi wao viwango vyao vimeshuka. Si wale tena tunaowajua. Wamebaki na majina yao makubwa kutokana na kazi kubwa waliyoifanya huko nyuma.
Ikifika wakati mchezaji wa timu kubwa Afrika kama Simba, kutuliza mpira inakuwa tatizo, huwezi kushangaa timu ikifungwa.
Wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa wakitafuta mchawi kwa nini timu yao inafanya vibaya, wengine wakidai timu inakamiwa sana, wengine wakidai 'kamati za ufundi' hazifanyi kazi vizuri na vingine vinavyofanana na hivyo.
Lakini kwa jicho langu la kiufundi, pamoja na mambo mengi wanayoyasema, inawezekana yapo, timu kama ya Simba, wachezaji wake wakiwa fiti kama ile ya miaka miwili mitatu iliyopita, hata mtu afanye vipi, watakufunga tu.
Leo timu zote za Ligi Kuu haziogopi tena kucheza na Simba, wakati miaka miwili mitatu iliyopita si timu za Tanzania tu, hata Al Ahly, Mabingwa wa Afrika, walikuwa wanaogopa kucheza nayo.
Niwe mkweli tu, kuwa wachezaji kama John Bocco, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Chris Mugalu, wameshuka viwango sana na hawawezi tena kuisaidia timu hiyo, huku Bernard Morrison na Rally Bwalya wakicheza soka la kishule na kitoto zaidi badala ya kutafuta matokeo.
Sitaki kwenda mbali sana, na wala siwezi kuwapa lawama viongozi wa Simba kwa nini hawakufanya usajili kipindi cha dirisha dogo. Kile ni kipindi ambacho huwezi kupata wachezaji wazuri wa kusajili ambao hawana timu. Utabambikiwa tu.
Labda kwa sasa cha kufanya ni kocha kuanza kuwaamini kina Jimson Mwanuke, Yusuph Mhilu, Denis Kibu, Isael Mwenda, kuungana na wachezaji wengine wanaoonyesha uwezo na kuibeba timu kwa sasa kama Pape Sakho, Henock Inonga, Joash Onyango, Mohamed Hussein, Jonas Mkude na Clatous Chama.
Ipate ubingwa au isipate, hiyo ni kengele ya hatari kuwa sasa klabu inatakiwa kuondoa wachezaji wengi baada ya msimu kumalizika kwa sababu viwango vyao vimepungua sana kutokana na umri, kubweteka, kutojituma au kulewa mafanikio kwani kila kitu tayari wameshakipata, ubingwa na kufanya vema kimataifa.
Simba inatakiwa kufanya usajili mkubwa baada ya ligi kumalizika na kuondoa wachezaji wengi wa ndani ambao hawana msaada kabisa, pia kutafakari nafasi 12 za wachezaji wa kigeni, ilete wenye uwezo mkubwa na hadhi kama ya klabu hiyo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








