Au kwa maana rahisi ni kwamba, kwenye kila jambo gumu, kuna jambo zuri zaidi linakuja hapo mbeleni.
Hivyo ndivyo tunavyoweza kusema kwa sasa kwa upande wa Klabu ya Simba ambayo ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, lakini inapitia kipindi kigumu kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania bara.
Simba katika mechi tatu zilizopita za Ligi hiyo, imeambulia pointi moja, huku ikipoteza kwenye mechi mbili na hivyo kujikuta wakipitwa pointi 10 na vinara Yanga ambao ni watani zao wa jadi.
Ilianza kufungwa na Mbeya City kule kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, halafu ikatoka sare na Mtibwa Sugar pale Manungu Morogoro na baadae ikachezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa walima miwa Kagera Sugar.
Matokeo hayo ambayo ni mabaya kwa Simba kwenye Ligi Kuu sio kiashiria kizuri kuelekea kwenye mechi za michuano ya CAF Februari na hivyo ni lazima ichukue hatua za haraka kujipanga na kujiandaa vizuri.
Nipashe tukiwa kama mmoja wa wadau wakubwa wa soka hapa nchini, tunaona kwamba, pamoja na matatizo yote ambayo Simba inaonekana kupitia, lakini viongozi, wachezaji, wanachama na wapenzi wanatakiwa kutambua kwamba wana wajibu mwingine wa kijitathmini na kujipanga kwenye mechi za kimataifa.
Simba imepangwa kundi moja la D pamoja na timu za RS Berkane kutoka Morocco, ASEC Mimosa ya Ivory Coast na US Gendarmerie ya Niger na timu zote hizo zinafahamika sio za kuzichukulia kimzaha.
Nipashe tunaona kwamba, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenyewe wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia na kujituma kwenye mazoezi kwa ajili ya mechi hizo.
Simba inapaswa kujua kwamba ina jukumu kubwa la kuiwakilisha vizuri Tanzania katika mashindano hayo ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya Klabu barani Afrika ukiacha yale ya Ligi ya mabingwa.
Tunaamini kwamba, Simba ambayo ina wachezaji wenye vipaji inaweza kukabiliana vizuri na changamoto inazozipitia kwa sasa na kujipanga vizuri tayari kwa ajili ya michezo hiyo hatua ya makundi.
Nipashe tunaamini kuwa kujipanga na kujiandaa vizuri kwa Simba kunaweza kuwafanya wapate matokeo mazuri kwenye hatua hiyo na kusonga mbele kutoka hatua ya makundi.
Tuna imani viongozi wa Simba watalitazama hilo kwa umakini mkubwa kwenye maandalizi ya kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano hiyo ya CAF.










