Akizungumza wakati wa usafirishaji wa zao hilo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, alisema serikali imeanza kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wakulima wanatafutiwa masoko ya uhakika.
“Leo tumetimiza jambo moja la kusafirisha parachichi kuelekea India ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia. Lakini pia hii yote imetekelezwa ikiwa ni uhusiano mzuri kati ya Tanzania na India, lakini pia viongozi wa nchi hizo kukubaliana kusafirisha bidhaa hii,” alisema Mavunde.
Mavunde alisema Novemba 25, mwaka jana viongozi wa serikali za Tanzania na India walikutana na kufanya mazungumzo ya namna bora ya kusafirisha zao hilo.
Alisema baada ya pande mbili kufikia muafaka, Idara ya Afya ya Mimea India ilitoa tangazo maalumu lililokuwa likitoa ruhusa kwa Watanzania kuanza kusafirisha parachichi kuelekea India.
“Leo tani zaidi ya mbili zinasafirishwa, sasa wakulima waanze kulima kwa tija ili tusafirishe bidhaa nyingi zaidi na bora, Tanzania tunazalisha tani 40,000 za maparachichi kwa mwaka lakini uwezo wa kusafirisha ni tani 9,000,’ alisema.
Kwa mujiobu wa Mavunde, kwa sasa Wizara ya Kilimo iko katika maandalizi ya kuanzisha kituo maalumu cha kupokea parachichi kutoka kwa wakulima, ambacho kitakuwa na kazi ya kuchambua parachichi na kuziweka katika ubora kisha kusafirishwa kwenda nchi mbalimbali.
“Tunataka parachichi zetu zisomeke zinatoka Tanzania. Katika mazao ya mboga parachichi tunaipa kipaumbele cha kwanza, hivyo wakulima wajitokeze kwa wingi katika kulima,” alisema Mavunde.
Mfanyabiashara aliyekuwa akisafirisha parachichi hizo, Sameer Gupta, alisema alianza mchakato wa kuomba ridhaa ya kusafirisha bidhaa hiyo tangu mwaka 2018.
Alisema kusafirishwa kwa parachichi kutoka Tanzania kwenda India kutaongeza mapato na kuinua uchumi wa Tanzania sambamba na kuitangaza kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi, alisema; “Tumejitahidi kwa miaka mitatu kupata mzigo mkubwa kama huu. Tukienda India huwa tunarudi na mzigo wa tani nane hadi 12, lakini tunapokwenda tunakuwa na mzigo mdogo sana”
Matindi alisema ATCL iliangalia soko la India linataka nini na kubaini kwamba parachichi ndiyo zao lenye soko kubwa.
Alisema shehena hiyo ni ya pili kusafirishwa na ATCL na kwamba katika kipindi cha Januari wanatarajia kusafirisha tani 20 kwenda India.










