Taarifa ya benki hiyo ilieleza kuwa tawi jipya sasa lipo Plot no 24, Block “56”, Narung’ombe/Sikukuu Street, Kariakoo.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, akiwa mgeni rasmi ambapo Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Kevin Wingfield, akizungumza kwenye uzinduzi huo, alisema hatua hiyo ya kimkakati inalenga kuendelea kuwahudumia wafanyabiashara walioko Kariakoo na maeneo ya jirani.
“Tawi letu la Kariakoo limekuwapo kwa zaidi ya miaka 10. Tumechagua kubaki eneo la Kariakoo kwa sababu tunafahamu umuhimu wa mchango wa wafanyabiashara wa Kariakoo kwa uchumi wa Taifa pamoja na nchi jirani.”
Wingfield aliongezea kuwa kupitia tawi hili jipya benki itaendelea kushughulika na mahitaji ya kifedha ya wateja wake wakiwamo watu binafsi, wajasiriamali, na biashara.
Kwa upande wake, Makalla aliipongeza Benki ya Stanbic kwa jitihada zao za kuhakikisha wakazi wa Kariakoo wanapata huduma za kifedha kwa urahisi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Rejareja wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga, alisema benki hiyo yenye historia kubwa ya kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 25 nchini ina utaalamu na uwezo wa kuchochea uwekezaji ndani ya Tanzania na kukuza uchumi wa Tanzania na jirani.
Mtiga aliongeza kwamba wateja watafurahia ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya fedha waliojikita katika kuwasaidia kufanikisha ndoto zao.










