Kwenye shule zilizotembelewa maisha yalionekana kuendelea kama kawaida bila kuchukuliwa tahadhari zozote za kujikinga na UVIKO-19 kwa kufuata mwongozo ulitolewa na Wizara ya Afya.
Baadhi ya shule zilikuwa hazina vyombo vya maji tiririka, sabuni, vitakasa mikono wala uvaaji wa barakoa kwa wanafunzi, walimu, watumishi wengine na wananchi wanaofika maeneo hayo.
Hali hiyo ni tofauti na hamasa inayotolewa kila siku ya kujikinga na UVIKO-19 kutokana na uwezekano mkubwa wa ugonjwa huo kusambaa kwa haraka ikiwa tahadhari haitachukuliwa.
Kwa sasa jitihada zinafanyika kuhakikisha wananchi wengi wanachanja ili kupunguza kasi ya ugonjwa huo watakaoupata, lakini bado watu wengi hawajajitokeza kuchanja.
Madhara ya UVIKO-19 ni makubwa kiuchumi na kiafya, kwa kuwa wapo ambao maisha yao yameharibika kabisa kutokana na ugonjwa huo, kwa kurudi katika hali ya umaskini.
Kwa waliopatwa na ugonjwa huo hata wakipona madhara ya muda mrefu hubaki mwilini na mara kadhaa baadhi ya wagonjwa wamejitokeza kueleza licha ya kupona, bado hawajarudi kwenye afya zao njema.
Zipo taarifa za kisayansi zilizothibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kuwa watoto wanaweza kusambaza ugonjwa huo kirahisi kwa kuwa wanahamisha virusi kutoka eneo moja kwenda lingine.
Hadi sasa hakuna ushahidi wa kisayansi wa watoto kuambukizwa virusi hivyo, lakini upo uwezo wa watoto kuambukiza watu wazima nyumbani na ndiyo maana wanatakiwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono.
Ni muhimu utaratibu wa wanafunzi kunawa mikono mara kwa mara ukarejeshwa kwa kuwa mbali na kusaidia kujikinga na corona inawasaidia kujikinga na maradhi mengine ikiwamo ya homa ya matumbo.
Pia husaidia usafi wa mara kwa mara kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, hivyo ni muhimu kuhamasisha wanafunzi kunawa na kujikinga na ugonjwa huo ili kuwakinga watu wa nyumbani mwao.
Tunafikiri ni muhimu walimu nao wakawa wanavaa barakoa kama inavyotakiwa ili waendelee kuwa salama, kwa kuwa taarifa za kisayansi zinaonyesha kuwa watu wazima kuanzia miaka 35 kuendelea wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo kuliko wengine.
Ni muhimu walimu na watumishi wengine wakahakikisha wako salama muda wote, pia wachanje ili watakapopata ugonjwa huo usiwe mkali.
Upo ushahidi wa kisayansi kuwa waliochanja wanaweza kupata corona, lakini ugonjwa hautakuwa mkali kama ambaye hakuchanja na uwezekano wa kupona ni mkubwa.
Lazima kuhakikisha usalama wa kila mmoja wetu katika mazingira yoyote ili kuepuka gharama za matibabu na kuumia kiuchumi kutokana na ugonjwa huo.










