Tukio hilo linatokea miezi kadhaa ikiwa wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na Mwenge, hawajasahau machungu waliyokutana nayo kutokana na kuunga kwa masoko hayo.
Moto huo umeteketeza mali nyingi na kuwaacha wafanyabiashara hao watupu, walitoka hatua ya juu kurudi chini huku wenye mikopo wakibaki njiapanda.
Baada ya kuungua kwa Soko la Kariakoo, iliundwa timu ya uchunguzi ambayo hadi sasa haijatoa matokeo, huku kukiwa na mipango ya kuboresha zaidi kwa siku zijazo.
Maeneo haya yote yamewaumiza wafanyabiashara wadogo ambao wameuanza mwaka kwa majonzi kwa kupotelewa na mali zao zote na sasa wanashindwa kurudi kwenye maeneo husika kuendelea na biashara.
Wengi walionekana kukaa chini huku wasijue la kufanya, wakilia vilio vya uchungu na baadhi wakitaka kupenya kwenye moto ili kuokoa chochote, lakini walishindwa.
Kwa ujumla janga hili na mengine yameharibu mwelekeo wa maisha ya wengi, wapo ambao mtaji mzima umeteketea, wamepoteza kila kitu na sasa hawajui waanzie wapi na watatoa wapi mtaji.
Wapo waliokopa kwenye taasisi za fedha wanatakiwa kurejesha fedha, au wapo kutokana na biashara hiyo wanasomesha watoto wao, wanalipa kodi za nyumba na kupata mahitaji yote ya msingi, lakini kwa hali ilivyosasa maisha yao yamesimama.
Tayari imeundwa timu ya kuchunguza tukio hilo na wafanyabiashara wamekatazwa kurudi kwenye eneo hilo, na jana palitokea mvutano baina yao na polisi kwa kuwa walitaka kurudi kujenga vibanda vingine kuendelea na bishara ya kutafuta riziki ya siku.
Timu hiyo inayojumuisha Ofisi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Uokoaji na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Aidha, wafanyabiashara hao walipinga uchunguzi kuchukua siku 14, wakidai ni nyingi kwa kuwa wanataka kuendelea kutafuta riziki kwenye eneo hilo.
Tunapongeza hatua za awali zilizochukuliwa na serikali, lakini ni muhimu wakavaa viatu vya wafanyabiashara hao kuona namna ya kuwawezesha kuendelea na biashara zao kuliko mamia ya watu kurudi nyumbani bila kuzalisha kwa muda mrefu.
Maswali ni mengi juu ya chanzo cha moto kwenye masoko haya, matokeo ya uchunguzi unaofanyika, jitihada za kukabili majanga ya moto hata kwenye maeneo ya miji ambayo kuna miundombinu mizuri.
Ni muhimu wafanyabiashara hawa wakasaidiwa kwa kuwa wanatafuta riziki, wanachangia kwenye uchumi wa nchi, wasiachwe hewani bila kujua mwelekeo kama tulivyoona kwenye masoko mengine.










