Katika dunia ya sasa, kumekuwapo na mabadiliko makubwa ya TEHAMA, ambayo inachukua nafasi kubwa ya kuharakisha maendeleo yakiwamo ya elimu.
Katika kufanikisha hilo, serikali inawekeza kwenye miundombinu ya mkongo wa taifa na kuusogeza hadi kila wilaya na kuondoa VAT kwenye vifaa vya TEHAMA, vifaa hivyo ni pamoja na vya kielektroniki simu janja na modemu, ili kuwajengea vijana mazingira bora ya kutumia teknolojia hiyo kujiajiri kwa ajili ya maendeleo yao na taifa.
Si hapo tu bali inasema, inatarajia pia kujenga chuo bora zaidi cha kisasa cha TEHAMA, ili kuongeza kasi, ubunifu na ufanisi katika matumizi ya teknolojia hiyo, kwa kuwa ndiyo ni msingi wa taifa endelevu.
Chuo kinachotarajiwa kujengwa na serikali kutatoa kipaumbele katika masuala ya utafiti na ubunifu kwenye TEHAMA, kwa kusajili na kuwatambua vijana wote wanaojishughulisha na teknolojia hiyo.
Ni wazi kwamba, serikali inataka kunyanyua ubunifu wa vijana, hivyo ni vyema vijana wenyewe wakachangamkia fursa hiyo, kwa kuonyesha uwezo wao wa teknolojia hiyo ambayo ina nafasi kubwa katika dunia ya leo.
Hiyo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba, serikali yake itatoa kipaumbele katika kusaidia vijana watakaojiunga pamoja kwenye shughuli mbalimbali za utafiti na ubunifu kwenye TEHAMA.
Ni katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwishoni mwa mwaka jana wilayani Chato mkoani Geita anasema, dunia ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda, shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinafanyika kwa TEHAMA.
Kwamba, chuo hicho ambacho Rais anasema kitakuwa kinaongoza kwa ubora Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, kitawajengea pia uwezo wa kimataifa, kujiingizia kipato na kwa maendeleo ya Taifa.
Uamuzi huo wa serikali unaonyesha ni jinsi gani imeamua kuweka nguvu kwenye teknolojia hiyo ili kwenda na wakati hasa katika karne ya 21 ambayo ni ya sayansi na teknolojia ili kuboresha huduma mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa, dunia ya sasa, kumekuwapo na mabadiliko makubwa TEHAMA ambayo sasa inachukua nafasi kubwa kwa ajili ya kuharakisha shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo elimu.
TEHAMA imerahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwamo za elimu, lakinipia kupunguza upotevu wa muda na gharama za kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine kufuata mahitaji mbalimbali.
Kwa sasa, kila mtu anahitaji uelewa wa msingi wa teknolojia hiyo na jinsi inavyofanya mambo mbalimbali ikiwamo kuwa wanafunzi wazuri, kufundisha watu jinsi ya kuwa na uwezo wa kuitumia.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba, katika karne ya 21, TEHAMA inahitajika katika stadi muhimu na mifumo ya elimu, lakini kwenye sekta mbalimbali kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.
Katika viwanda na kwenye jamii ya kisasa kwa ujumla, inaelezwa kuwa teknolojia hiyo ina majukumu muhimu ya kimkakati kama njia mojawapo ya kuharahisisha shughuli za kila siku.
Hivyo, kutokana na umuhimu huo, Tanzania haijabaki nyuma, badala yake inachukua hatua kusonga mbele kwa kuwekeza katika teknolojia hiyo hasa kwa mkakati wa kujenga chuo kikubwa cha TEHAMA, lakini kutumia teknolojia hiyo kuendeleza vijana kupata ajira.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







