Tukio hilo lilitokea jana wakati wa mechi ya Ligi Kuu kati ya Simba na Azam FC, Wekundu wa Msimbazi wakishinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Wakati wengine wakidai penalti ilistahili kurudiwa, kuna walisema kuwa hata ingerudiwa ingekoswa pia. Wapo walienda mbali zaidi kuwa hata ingerudiwa mara tano, mpigaji angekosa. Utani uliendelea baadhi wakasema hata wangebadilisha mpigaji, hali ingekuwa vile vile, wangekosa tu.
Simba imekuwa ikikosa penalti kwa namna ya kushangaza. Imekuwa ikitengeneza sana adhabu ya penalti kutokana na kuwa na wachezaji wasumbufu na wenye kasi, lakini zinapopatikana, kuzitumia ndiyo inakuwa tatizo.
Inavyoonekana kwa sasa ni kwamba timu hiyo haina mpigaji penalti maalum na wengi wao wanabahatisha. Bwalya, ambaye alipata penalti kwenye mechi dhidi ya Polisi Tanzania na kuipa timu yake ushindi wa bao 1-0, ndiye aliyekosa juzi.
John Bocco, ambaye kwa misimu yote aliyojiunga Simba ndiye tegemeo kubwa kwa upigaji mikwaju hiyo, siyo tu kwamba anaonekana kupoteza namba kwenye kikosi cha kwanza, lakini pia hata upigaji wake nao umeanza kuwa si wa uhakika.
Alikosa penalti kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu, Simba ikicheza dhidi ya Biashara United katika Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara na kuifanya timu yake kukosa ushindi kwa kutoka suluhu, lakini mpigaji mwingine maalum Erasto Nyoni ambaye ni nadra sana kukosa, naye alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting, ingawa Simba ilishinda mabao 3-1.
Inavyoonekana ni kwamba wapiga penalti wa kutegemewa wa Simba, Bocco na Nyoni, wamepoteza namba lakini uwezo wa kupiga penalti pia. Kwanza kabisa tuelewe kuwa kupiga penalti ni kipaji. Kuna wachezaji hata kama wana uchezaji wa kawaida tu, lakini linapokuja suala la kupiga tuta ni mafundi.
Simba kwa miaka mingi nyuma ilikuwa ndiyo timu iliyokuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kupiga penalti, kiasi cha timu nyingi kuhofia hata kwenda nayo hatua ya matuta, ikiwamo hata watani zao wa jadi, Yanga.
Nakumbuka Simba ilicheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 1993, ambao ilifika fainali, moja ya timu iliyoitoa ni Santos ya Afrika Kusini, ambapo ilishindwa kwa mikwaju 11-10 ya penalti.
Ni mechi ambayo wachezaji wote wa Simba hadi kipa walitumbukiza mpira ndani ya wavuni, huku Santos wakikosa moja, Wekundu wakisonga mbele.
Kwa sasa sijui kama inaweza kuwa hivyo. Simba ipo kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo benchi la ufundi wanaweza kukaa na wachezaji wao kuangalia ni jinsi gani wanaweza kufanya ili kutokosa ovyo penalti.
Ikumbukwe hata kwenye mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho, Simba ilikosa penalti, Bernard Morrison akipiga penalti dhaifu iliyookolewa na kipa kama ilivyopigwa kwa Bwalya juzi.
Kocha Mkuu Pablo Franco, sasa akae na kuangalia mazoezini ni mchezaji gani ambaye anaweza kumpa jukumu la kupiga adhabu hiyo, kwani Simba inaweza kufika mbali, robo fainali au nusu fainali, halafu inapata penalti dakika za mwisho, upigaji wenyewe ndiyo ule, hivyo kuwasababishia majonzi na simanzi mashabiki wake.
Timu hiyo ina wachezaji wazuri wa kupiga penalti ambao ninawafahamu, lakini kwa bahati mbaya mara nyingi hawaanzi, pia huwa hawapewi jukumu la kupiga kwa sababu si maarufu.
Wachezaji hao ni Israel Mwenda, Gadiel Michael, na Hassan Dilunga. Ni wapigaji wazuri sana wa mikwaju ya penalti, lakini kwa sababu hizo ndiyo maana hawapigi.
Selemani Matola ambaye ni kocha msaidizi, anaifahamu Simba ile ya zamani ambayo ilikuwa na mafundi wa kupiga penalti wakati anacheza mpaka sasa, aongee na kocha Pablo waanze kulifanyia kazi suala hilo, kwani halionekana kubwa sana kwa sababu mechi nyingi ilizokosa timu ilikuwa inashinda, lakini siku ikitokea hasa kwenye mechi za kimataifa timu ikapoteza, ndipo kushtuka wataona kuwa kuna tatizo hilo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








