Ukatili huo umeendelea kuumiza jamii kimya kimya, kutokana na kwamba kitendo hicho kinafanywa kati ya watu wawili kwa siri kubwa, lakini madhara yake yanabaki kuwa ya muda mrefu kwa aliyeombwa rushwa hiyo.
Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ni miongoni mwa waathirika wa rushwa hiyo inayosababishwa na lifti za madereva wa bodaboda, bajaji na daladala, ili wawahi shule au nyumbani au wakati mwingine kupata urahisi fulani.
Wale wote wanaopitia rushwa ya ngono husababisha pia kupata mimba ambazo hazikutarajiwa na wengine huenda huwa wanatoa mimba hizo. Inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa mara nyingi huwa si jambo salama.
Kutokana na hali hiyo, kumekuwapo kampeni mbalimbali zinazofanywa na wadau wa kupinga vitendo hivyo, ikiwamo inayoitwa 'Safari Salama kwa Wasichana na Wanafunzi Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana'.
Ni kampeni inayoendeshwa na Wanawake na Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), kwa kutoa elimu kuhusu rushwa hiyo kwa madereva wa bodaboda, bajaji na daladala ili waachane na vitendo hivyo.
Madereva hao wanadaiwa kushiriki katika rushwa ya ngono kwa kutumia lifti kama mtego kwa wanafunzi, hasa wale wanaotembea umbali mrefu kufuata elimu, ambao baadhi yao huangukia katika mitego ya madereva hao.
Katika kuhakikisha rushwa ya ngono inayosababishwa na lifti za madereva hao inakoma, shirika hilo limeanzisha kampeni katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, jijini Dar es Salaam.
WAJIKI inataka wasichana na wanafunzi wa kike kwa ujumla wabaki salama wakitimiza malengo na safari yao ya maisha bila kikwazo kinachosababishwa na rushwa ya ngono.
Elimu ya kupambana na rushwa ya ngono, inahusisha madereva hao kupitia vikundi vyao chini ya udhamini wa Taasisi ya Women Tanzania Trust Fund (WTF), ambayo inaunga mkono juhudi za WAJIKI.
Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza, anasema shirika lake limefanikiwa kuanzisha vikundi 108 vya madereva hao vyenye wanachama 3,741 katika wilaya hizo tatu wakiwa na jukumu la kuelimisha wenzao.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, vikundi vya madereva hao ambao ni wanachama wa WAJIKI wanaelimisha wenzao ili wajue madhara ya rushwa hiyo na kuepuka kuwarubuni wanafunzi.
Binafsi ninaamini kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo ni vyema kila mmoja kuona umuhimu wa kuunga mkono kampeni ya 'Safari Salama kwa Wasichana na Wanafunzi Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana.'
Hatua hiyo inaweza kuleta matokeo chanya kwenye vita dhidi ya rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wasichana, inayosababisha baadhi yao kutofikia malengo na hata wakati mwingine kuathiri afya zao.
Rushwa hiyo bado inaendelea kuumiza jamii kimya kimya, kwa kuwa kitendo hicho kinafanywa kati ya watu wawili kwa siri kubwa lakini madhara yake yanabaki kuwa ya muda mrefu, kwa aliyeombwa rushwa hiyo.
Cha kukumbuka ni kwamba, madereva wanapomtamani wanafunzi au wasichana kingono, hutumia nyenzo waliyo nayo wakiwasafirisha kwa malengo ya kuwalaghai na kupata rushwa tajwa ya ngono.
Hivyo, suala la mapambano dhidi ya rushwa hiyo, inawasha taa ya ukombozi kwa wasichana na wanafunzi kwa ujumla na inapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote, ikifaa iongelewa na makundi yote, ili ikomeshwe kwa mafanikio ya kijamii.
Watu wanaotakiwa kuwapa huduma ya usafiri wanafunzi, ndiyo ambao huwaomba rushwa ya ngono na mwisho wa siku wanawaachia madhara ya kiafya. Kampeni ya 'Safari Salama kwa Wasichana na Wanafunzi Bila Rushwa ya Ngono’ inawezekana na iwe chachu ya mabadiliko kwetu sote.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







