Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana mgawanyo wa fedha hizo, wakati wa uzinduzi wa mpango wa serikali wa kuinua uchumi kwa kutumia fedha hizo.
Kwenye sekta ya elimu fedha hizo zitajenga vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari lengo likiwa ni kuwezesha wanafunzi wote kuendelea na masomo bila kikwazo.
Kwa sasa ujenzi wa vyumba vya madarasa unaendelea maeneo mbalimbali nchini, na nguvu imeelekezwa huko ili ikifika Januari kusiwe na zimamoto kama ilivyojitokeza miaka mingine na kusababisha wanafunzi kuchelewa kuingia kidato cha kwanza.
Tunaamini kila halmashauri imejipanga vyema kwa kuangalia makadirio ya miaka ya nyuma ya ufaulu wa wanafunzi na vyumba vya madarasa vinavyotakiwa, na haitarajiwi kuanza kukimbizana kubadili shule za msingi kuwa sekondari, kiasi cha miundombinu kuelemewa.
Miaka ya nyuma wananchi walijenga shule hizi kwa fedha zao na mwamko ulikuwa mkubwa kwenye baadhi ya maeneo, lakini kwingine ilikuwa ngumu kwa kuwa wananchi hawakuona umuhimu wa kuchanga.
Sasa serikali imekuja na suluhisho ni wajibu wa kamati za shule kufuatilia kwa karibu ujenzi wa miundombinu hiyo ili iwe ya kiwango, thamani ya fedha ionekane ili hata kama tutashiriki kulipa deni kama nchi tutakuwa tunafuta jasho kupitia miundombinu inayodumu.
Mara nyingi mchakato wa ununuzi husababisha gharama ya ujenzi kuwa kubwa na wakati mwingine kushangaza au thamani ya fedha kutoonekana, hivyo ni muhimu kufuatilia ili tuwe na majengo imara na sio baada ya mwaka mmoja hayafai kutumika.
Tunaamini kwa maandalizi haya sasa wanafunzi watasoma bila tatizo kwa kuwa sasa suala la miundombinu litabaki kuwa historia, kinachotakiwa ni kuboresha upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada pamoja na walimu wa kutosha.
Upatikanaji wa vitabu muhimu ni shida kwenye shule za umma ambako elimu ni bure na wazazi wengi hawana utayari wa kununua kwa ajili ya watoto wao, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha vinapatikana na wanafunzi wanafundishwa kwa kadri ya mitaala na ratiba zilizopo.
Kwenye shule nyingi za umma tatizo kubwa ni ubora wa elimu inayotolewa ambayo imebeba mambo mengi kama utayari wa walimu kufanya kazi kwa ubunifu, kujitoa na kuipenda kazi na sio kwa ajili ya kupata mshahara pekee.
Lakini, wanaosimamia walimu kuhakikisha wanatoa motisha mara kwa mara kwa kuwa kazi wanayofanya ni kubwa, lakini wakati mwingine malipo ni madogo na hakuna stahiki nyingine kama ilivyo kwenye taasisi nyingine.
Kwenye shule hizi ndiko tunapata mawaziri, wakurugenzi wa taasisi mbalimbali na viongozi wengine muhimu, wote wamepikwa na mwalimu sasa ni wajibu wa kuboresha miundombinu sambamba na maslahi ya walimu, ili tusiishie kuwa na majengo mazuri, lakini bidhaa (wanafunzi) wanaotoka humo hawaendani na uwekezaji uliofanyika.
Tunaamini baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa sasa nguvu kubwa itakuwa ni kuboresha makazi ya walimu, ambayo ni tatizo kubwa kwa sasa kwa kuwa wengi wamejikuta wanapangiwa vituo vya kazi ila hawana pa kuishi.
Bila kuwa na walimu wenye maeneo mazuri ya kuishi na familia zao wakatuliza akili, ni ngumu kuwa na wanafunzi watakaofaulu vizuri kwa kuwa ufaulu wa wanafunzi unategemea sana kazi kubwa iliyofanywa na walimu katika kujenga ubongo wao.
Tunatarajia kuona mafanikio endelevu kwa fedha hizo ambazo ni deni litakalolipwa na Watanzania kwa miaka mingi ijayo.










