Wanaosajiliwa Simba SC, Yanga wajiandae kisaikolojia

25Dec 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanaosajiliwa Simba SC, Yanga wajiandae kisaikolojia

HIKI ni kipindi cha usajili wa dirisha dogo, klabu mbalimbali zinasaka wachezaji ambao wataongeza makali kwenye timu zao.

Tumeona baadhi ya wachezaji wakitoka klabu hii kwenda nyingine. Katika kipindi hiki mpaka sasa Geita Gold imeonekana haitaki mzaha, kwani imeonekana kulitumia vizuri dirisha hili kwa kuwanasa William Lucian 'Gallas', Juma Nyosso, Ditram Nchimbi kutoka Yanga, na hadi jana ilikuwa kwenye hatua ya mwisho kukamilisha usajili wa Kelvin Yondani kutoka Polisi Tanzania.

Sijaona pilikapilika sana kwenye klabu ya Simba kutaka kusajili wachezaji wa Kitanzania. Inawezekana ina mpango huo, lakini inafanya kwa siri. Watani zao wa jadi, Yanga ipo kwenye hatua za mwisho kuwatangaza wachezaji Salum Aboubakar 'Sure' Boy' kutoka Azam na Dennis Nkane wa Biashara United.

Inavyoonekana ni suala la muda tu, kwani tayari meneja wa 'Sure Boy', Heri Mzozo, amethibitisha mchezaji huyo 'ameshaanguka' mkataba wa miaka miwili kwa Wanajangwani hao, huku Mwenyekiti wa Biashara United, Selemani Mataso akikiri walikuwa katika mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kukamilisha 'dili' la Nkane, mmoja wa wachezaji chipukizi na machachari.

Wote hao ni wachezaji wazuri, lakini linapokuja suala la kwenda Simba au Yanga kinakuwa ni kitu kingine kabisa.

Hapa simsemi Nkane na Sure Boy, peke yao, hata wachezaji wengine wa Kitanzania watakaosajiliwa na Yanga, na wale ambao tunawasikia wakisajiliwa Simba, wakae wakijua kwenda kwenye timu hizo si sawa na kujiunga na Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania, Geita Gold, Kagera Sugar, Prisons au timu nyingine.

Nikiandika hivi kuna ushahidi mwingi uliowahi kutokea nyuma na sasa, jinsi wachezaji waliovuma kwenye klabu mbalimbali, lakini wakaenda kukwama kwenye klabu hizo kubwa.

Hapo ndipo utawakumbuka kina Hussein Javu, Said Bahanuzi, Paul Nonga, Waziri Junior na wengine wengi ambao walifanya vyema sana kwenye klabu zao walizotoka, lakini walipofika Yanga walishindwa kuonyesha kiwango hata kile kile tu.

Kwa upande wa Simba, walisajiliwa wachezaji kama, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Novatus Lufunga, Juma Luizio, Charles Ilamfya na wengine ambao hawakufurukuta kama ilivyokuwa walikotoka.

Siyo wachezaji wote wanaosajiliwa na timu hizo huwa hawafanyi vyema, la hasha, ila kumekuwa na wimbi la baadhi ya wachezaji kushindwa kabisa kuonyesha viwango vyao wakiwa kwenye timu kubwa, hasa za Simba na Yanga.

Hapo ndipo zinaanza kuja zile dhana za imani za kishirikina kwa wachezaji wenyewe na baadhi ya mashabiki.

Ukiangalia kwa undani utakuta hakuna 'misumari', ila kuna vitu ambavyo wachezaji hao wanakutana navyo. Na hata kina Nkane watakutana navyo, hivyo wajiandae tu kisaikolojia.

Kujiweka vizuri kisaikolojia ndiko kutakakowafanya wawe kwenye viwango vyao, ili baadaye wasije tena kutolewa kwa mkopo.

Kwanza wajue wanakwenda kucheza kwenye timu zenye mashabiki wengi ambao hawana simile. Wanachotaka wao ni ushindi na mchezaji awe kwenye kiwango kile kile mara nyingi zaidi kuliko kuwa chini ya kiwango.

Wanachotakiwa kukifanya ni kufanya mazoezi mara mbili zaidi kuliko timu walizotoka, kwani sasa watakuwa wanakamiwa zaidi na timu watakazocheza nazo. Ni tofauti na walipokuwa wanacheza huko walikotoka, waliweza kuonyesha uwezo kwa sababu walichukuliwa poa na wachezaji wa timu pinzani, lakini sasa wapo Simba au Yanga ni mwendo wa kukamiwa mwanzo hadi mwisho, hivyo kama mchezaji hana pumzi, stamina na mazoezi ya kutosha, hawezi kupambana.

Mchezaji akiwa Simba au Yanga, hata kama uwezo wake ni kawaida, kutokana na maneno na kusifiwa na mashabiki anaweza kujiona uwezo wake ni mkubwa mno na kuanza kuvimba kichwa, kumbe kiuhalisia sivyo hivyo, badala yake uwezo unapungua siku hadi siku.

Hata Sure Boy, akae akijua pamoja na kwamba Azam ni timu kubwa, lakini anatakiwa kubadilika, Yanga haiwezi kuwa sawa na Azam kwa mashabiki.

Mara nyingi mchezaji akiwa Azam au timu nyingine anaweza kukosea mara nyingi, kukosa mabao mara nyingi, lakini kwa sababu haangaliwi inaonekana kawaida, lakini aina hiyo hiyo akiyakosa akiwa Simba au Yanga mjadala unaanza.

Hivyo ndivyo maisha yalivyo kwenye klabu hizi kubwa ambazo wachezaji wanaosajiliwa watakwenda kukutana nayo, kwa hiyo wajiandae kisaikolojia, kukabiliana na kelele za kushangiliwa na kuzomewa na mashabiki, kuhimili presha hizo,
kufanya mazoezi mara nyingi zaidi kuliko yale ya timu walizotoka kwa sababu watakamiwa sana, lakini pia wasitarajie kuingia tu watapata namba kirahisi, badala yake watatakiwa kutokwa machozi, jasho na damu ili kupata muda wa angalau kwanza kuingia kipindi cha pili, kabla ya kupata namba ya kudumu baadaye.